Home » » SKAUTI WAKANA KUBEBA DAWA ZA KULEVYA

SKAUTI WAKANA KUBEBA DAWA ZA KULEVYA


na Irene Mark
CHAMA cha Skauti Tanzania, kimekanusha tuhuma za kufanya biashara ya dawa za kulevya na kuwasafirisha watoto wa vigogo kwa upendeleo.
Badala yake viongozi wa chama hicho wamesema tuhuma hizo zinalenga kuvuruga uchaguzi mkuu wa chama chao unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Hivi karibuni wakati wa kuwasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa kwa bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (CHADEMA), aliliambia Bunge kwamba chama hicho kimeacha majukumu yake na kujiingiza kwenye biashara ya dawa za kulevya na kusafirisha watoto wa vigogo.
Katika majibu yake jana, Kamishna Mkuu Msaidizi (Kazi Maalumu) wa Skauti Taifa, James Mwanyato, alizifananisha tuhuma hizo na changamoto huku akisisitiza kwamba kauli hiyo ni dalili za kutaka kuvuruga uchaguzi wao mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.
“Huyo mbunge hajawahi kuja hapa kutuuliza wala kututembelea hata mara moja, tumeshtushwa na tunasikitishwa na tuhuma zake… hajawahi kufika kwetu tunachoamini ni kwamba hiyo ni changamoto inayoelekezwa kwetu na watu wasiotutakia mema.
“Yote yaliyosemwa tunamwachia rais wa chama chetu ambaye kwa mujibu wa Katiba ya Skauti ni Waziri wa Elimu, yeye atatoa ufafanuzi zaidi. Zaidi ya miaka minne hatujafanya uchaguzi, Skauti Mkuu wa mwisho hapa alikuwa mzee Iddi Kipingu, ambaye amemaliza muda wake mwaka jana.
Alisema kuwa kwa zaidi ya miaka miwili hawajawahi kupeleka skauti nje ya Bara la Afrika na kwamba wanapiga vita dawa za kulevya kwa kushirikiana kwa karibu na tume husika.
Kwa mujibu wa kamishna huyo, utaratibu wa kuwapata vijana wanaokwenda kuiwakilisha nchi huanzia shuleni, ambapo wanachama wote hushirikishwa, aidha wasafiri wote hupita uwanja wa ndege na kukaguliwa.
Alisema haijawahi kutokea kijana yeyote skauti wa Tanzania aliyewahi kukamatwa au kuhisiwa kuwa na dawa za kulevya hivyo kuwaomba wananchi kupuuza uzushi wa mbunge huyo.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa