Home » » JWTZ WALIPUA MIZINGA KIGAMBONI

JWTZ WALIPUA MIZINGA KIGAMBONI


na Hellen Ngoromera
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limetangaza kupiga mizinga 21 leo kuanzia saa 3.00 asubuhi katika maeneo ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, hivyo kuwataka wananchi kutokuwa na hofu kwani haitakuwa na madhara yoyote kwao.
Taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya jeshi hilo iliyotolewa jana, imeeleza kuwa mizinga hiyo itapigwa mara baada ya kuwasili kwa meli za kivita tatu kutoka nchini Japan.
Meli hizo kutoka Jeshi la Wanamaji la Japan zinazoongozwa na Kamanda wa Mafunzo wa Vikosi vya Wanamaji, Hidetoshi Funchinoue, atakayefuatana na mabaharia 1,176 zitawasili leo asubuhi.
Imeelezwa kuwa lengo la ugeni huo ni kufanya ziara ya kimafunzo kwa maofisa wanafunzi waliomaliza masomo katika chuo cha Japan Maritine Self Defence Forces (JMSDF).
“Mara zitakapowasili meli hizo katika bandari ya Dar es Salaam itapigwa mizinga 21 na pia kiongozi wa meli hizo atazungumza na waandishi wa habari. Sherehe za mapokezi ya meli hizo zitaudhuriwa na Balozi wa Japan nchini na makamanda wa JWTZ,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya kuwasili ujumbe wa meli hizo utatembelea bandari ya Dar es Salaam, kwa Meya wa Jiji na Makao Makuu ya Navy, Kigamboni.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa