na Chalila Kibuda
BAADHI ya wananchi wameitaka serikali kurudia zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya taifa ili wakazi wote wenye sifa mkoani Dar es Salaam wapate fursa ya kupata haki yao.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa wakati tofauti, walisema kuwa zoezi hilo lilikuwa limegubikwa na mazingira ambayo yalisababisha wengi kushindwa kujiandikisha.
Walisema kuwa ni wajibu wa serikali kuangalia namna ya kuweza kurudia zoezi hilo la vitambulisho vya taifa kutokana na unyeti wake kwa kila Mtanzania.
Mkazi mmoja, Juma Hamisi, alisema kuwa zoezi hilo linatakiwa kurudiwa ili kutoa haki kwa watu wote kujiandikisha, hivyo aliiomba NIDA kuongeza muda walau wa siku 10 zaidi.
Naye Mwanahamisi Mwanahapa, alisema kuwa zoezi hilo limefanywa kwa mazingira ya ubabe, kwa kutowasikiliza wananchi, na hivyo muda wa wiki moja ulioongezwa haukutosha.
Ofisa Habari wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Thomas William, alijibu malalamiko hayo, akisema kuwa zoezi hilo haliwezi kurudiwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba litarudiwa kwa makundi maalumu tu.
William alisema zoezi hilo liliongezewa muda, hivyo serikali haiwezi kufanya hivyo tena.
“Zoezi hilo litarudiwa kwa makundi maalumu ya wazee na watu wenye ulemavu ambao walikuwa wameshindwa kuandikishwa kutokana na hali zao,” alisema William.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment