Home » » MASHINDANO YA MASHUA AFRIKA KURINDIMA DAR

MASHINDANO YA MASHUA AFRIKA KURINDIMA DAR

na Elizabeth John
MASHINDANO ya ubingwa wa Afrika wa mbio za mashua, yanatarajiwa kurindima jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 18 hadi 26 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mahusiano wa Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola Kwanza, Evance Mlelwa, alisema mashindano hayo yatashirikisha vijana wa kike na kiume kati ya miaka 18 hadi 15.
Mlelwa alisema mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Coca-Cola, ni makubwa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na yatashirikisha wachezaji takriban 80 kutoka nchi 11.
Alizitaja nchi zitakazoshiriki kuwa ni Algeria, Angola, Misri, Kenya, Msumbiji, Shelisheli, Afrika Kusini, Tunisia, Zimbabwe, Oman na visiwa vya Re-Union.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukilalamika kukosa medali katika michezo mbalimbali ya kimataifa zikiwemo fainali za Olimpiki, hivyo ni dhahiri kuwa kwa kuandaa mashindano haya, itakuwa ni mwanzo wa maaandalizi ya michezo ijayo ya Olimpiki,” alisema.
Akizungumzia ushiriki wa Tanzania katika michuano hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Mashua Tanzania (TSA), Philimon Nassari, alisema timu yake itakuwa na wachezaji 20 ambao watakuwa wakinolewa na makocha Jeppe Bregendahl na Tarick Nielsen.
Aliwataja nyota watakaounda timu hiyo, ni Magali De Brauwer, Timothee Maret, Lenno Telemans, Casey Deetlefs, Alexandera Pennanen-Kok, Emma Cunningham, Hassan Juma, Max Pennanen-Kok, Michael Kelly, Karim Samweli, Tulsi Patel, Danielle Stanley na Mervin Fugelsnes.
Wengine ni Adil Bharmal, Niels Sulzer, Vedastus Burahara, Sahil Patel, Mnanzi Juma, Imamu Ramadhani na Saidi Mkomba.
“Kimsingi, mafanikio ya mashindano hayo yanategemea sana na watu kujitolea, hususan katika udhamini, nichukue nafasi hii kuwashukuru wadhamani wote. Pia nashukuru msaada uliotolewa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Baraza la Michezo la Taifa (BMT),”
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wapigamakasia Tanzania, Michael Sulzer alisema, mashindano hayo ambayo yanaandaliwa kwa ushirikiano na Chama cha Kimataifa cha mchezo huo (IODA), yako kwenye kalenda ya chama hicho na pia yatatumika kupata wachezaji watakaoiwakilisha nchi kwenye michuano ya dunia, itakayofanyika baadaye mwaka huu na yale ya Kanda ya Tano Afrika.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa