na Nasra Abdallah
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imesitisha utoaji wa huduma kwa mabasi yote yanayomilikiwa na Kampuni ya Sabena ambayo hufanya safari katika njia za Dar es Salaam – Tabora, Tabora – Mbeya na Mwanza – Mbeya.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku chache tangu basi aina ya Scania Namba T 570 AAM mali ya kampuni hiyo kupapata ajali katika barabara kati ya Tabora na Mbeya, eneo la Kitunda Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.
Basi hilo ambalo lililokuwa likiendeshwa na Ally Nassor, Mwarabu, liliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya watu 17, wakiwemo watoto 5 wanaume 6 na wanawake 6 na kujeruhi wengine 78.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Meneja Mawasiliano kwa Umma wa Sumatra, David Mziray, alisema kwamba taarifa za awali zinaeleza kuwa, chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi ambapo dereva alishindwa kulimudu basi hilo, hivyo kuacha njia na kupinduka.
Pia, ilibainika kuwa, basi hilo lilikuwa limebeba abiria kupita uwezo wake, hivyo kutokana na tukio hilo, Mzirai alisema kuwa Sumatra inatilia mashaka sifa za madereva wa mabasi ya kampuni hiyo hasa ikizingatiwa kuwa, katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja, mabasi ya kampuni hiyo yamehusika katika ajali zisizopungua nane na kusabababisha vifo vya watu 22 na majeruhi zaidi ya watu 76.
“Hivyo, ili kujiridhisha na sifa za madereva pamoja na viwango vya ubora wa mabasi ya kampuni hiyo, Sumatra kupitia kifungu namba 15 cha Sheria namba 9 ya mwaka 2001, imesitisha mabasi hayo kutoa huduma.
“Usitishwaji wa huduma hizo unaanza rasmi Agosti 13, 2012 kwa lengo la kutoa nafasi ya kufanyia ukaguzi sifa na leseni za madereva wa mabasi hayo pamoja na viwango vya ubora wa mabasi ya kampuni hiyo. Aidha, hakutakuwa na vibali vya muda vitakavyotolewa kwa njia hizo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema kuwa, ukaguzi huo utafanywa na mkaguzi wa magari kutoka Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama marabarani na mabasi hayo yataruhusiwa kuendelea kutoa huduma katika njia hizo mara baada ya Sumatra kupokea taarifa za ukaguzi zinazothibitisha kuwa yanakidhi viwango vya ubora.
Wakati huohuo, Sumatra imeyafungia kwa kipindi cha miezi miwili mabasi yenye namba T 994 ASN na T 258 ANG kwa kosa la kutokutoa taarifa za ajali zilizosababishwa na mabasi hayo kama ulivyo utaratibu.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment