Home » » CHOO HALMASHAURI YA JIJI CHAFURIKA

CHOO HALMASHAURI YA JIJI CHAFURIKA

na Shehe Semtawa
BAADHI ya wateja na wafanyakazi wa ofisi za Halmashauri ya Jiji Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, afya zao ziko hatarini kupata maradhi ya mlipuko kutokana na choo cha hoteli iliyomo katika jengo hilo kufurika hadi kutiririsha kinyesi nje.
Wakizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, walisema wanastaajabishwa na hali hiyo ya hatari ikiendelea kwa zaidi ya miezi mitano bila kutafutiwa ufumbuzi.
Mmoja wa wateja hao, Khamisi Khalfan alisema kutokana na uchafu huo kukithiri na kuhatarisha afya zao baadhi yao wanatarajia kuacha kwenda kujipatia huduma katika hoteli hiyo.
Mfanyakazi mmoja wa ofisi hiyo aliyekataa kutajwa, alisema tatizo hilo linafahamika muda mrefu, lakini inatia hofu kuwaona viongozi wakikaa kimya kama vile hawana taarifa za uchafu.
“Unajua hiki choo tangu kuanza kufurika ilikuwa mwenzi wa nne ambapo hata mkurugezi mwenyewe wa jiji alifika kujionea hali hiyo, lakini hajachukua hatua,” alisema.
Alisema Agosti, mwaka huu, mkurugenzi aliwaahidi waendeshaji wa hoteli hiyo kuwa ofisi yake ingelifanyia kazi haraka tatizo hilo, lakini hadi leo bado halijapatiwa suluhu.
Alipoulizwa msemaji wa jiji, Gaston Makwembe, kuhusu suala hilo, alisema yuko kwenye ziara ila waulizwe wenye hoteli hiyo, mkataba wao unasemaje.
Mmoja wa viongozi katika hoteli hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alikiri kufurika kwa choo hicho, lakini hakuwa akijua mkataba unasemaje iwapo choo kingefurika nani angehusika kukifanyia usafi, zaidi alisema asubiriwe mkurugenzi wa hoteli hiyo.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa