Home » » WANAOCHAPISHA RAMANI ZA TANZANIA WASAKWA

WANAOCHAPISHA RAMANI ZA TANZANIA WASAKWA

na Betty Kangonga
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imetangaza kufanya msako kwa watu wanaochapisha ramani za Tanzania kinyume na taratibu ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa wizara hiyo, Dk. Selassie Mayunga, alibainisha hayo jijini Dar es Salaam jana na kuongeza kuwa wizara hiyo ndiyo yenye mamlaka kisheria ya kuchapisha ramani hizo na kuzisambaza.
“Tunatangaza rasmi ramani hizo ni feki hazitakiwi kutumiwa na watakaobainika kuzisambaza sheria itafuata mkondo wake,” alisema Mayunga.
Alisema watashirikiana na Jeshi la Polisi kuwakamata wahusika na kuziondoa ramani hizo kwenye mzunguko.
Aidha, alileleza kuwa jambo la kusikitisha ni kuwa hata taasisi za umma na binafsi zinatumia ramani hizo bila kufahamu kufanya hivyo ni kinyume na sheria.
“Ramani halali ni ile iliyotolewa na kuchapishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tu na si vinginevyo,” alisema.
Katika hatua nyinginge, wizara hiyo imetoa ramani mpya itakayojumuisha mikoa na wilaya zilizotangazwa na serikali hivi karibuni.
Mwaka jana serikali ilitangaza mikoa mipya minne ambayo ni Njombe, Geita, Simiyu, Katavi na wilaya 19.
Mkurugenzi huyo alisema taasisi za serikali na watu binafsi wanatakiwa kuwasiliana na wizara hiyo kwa ajili ya kupata ramani hizo halali.
Wakati huohuo, wizara hiyo imesema migogoro mingi ya ardhi inasababishwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wapima ardhi wanaofanya kazi zao bila kufuata taratibu na sheria.
Mkurugenzi huyo alisema watumishi watakaobainika kufanya makosa hao watafukuzwa kazi mara moja.
“Fanyeni kazi kwa kufuata misingi ya sheria, atakayekiuka hatakuwa miongoni mwetu,” alisema Dk. Mayunga.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa