Home » » HUWEZI KUWA MSAFI UKIWA JALALANI

HUWEZI KUWA MSAFI UKIWA JALALANI

NA SOPHIA YAMOLA
TOKA kubadilishwa kwa baraza la mawaziri mwezi Aprili mwaka huu, huku baadhi ya mawaziri wakiachwa kuteuliwa kwa kashifa mbalimbali za kushindwa  kusimamia majukumu waliyopewa kwenye wizara zao, kwa kashifa za ufisadi wa pesa za umma na kushindwa kusimamia na kutekeleza majukumu ya kazi.

Kumekuwepo na maswali mengi yasiyokuwa na majibu juu ya utenda kazi kwa baadhi ya mawaziri, ambao siku chache tu baada ya kuingia ofisini wanaonekana kuchapa kazi huku wananchi wakishindwa kuelewa kwa kufanya hivyo wanaweza kuisafisha serikali na ufisadi uliopo serikali na kurejesha heshima ambayo tayari wananchi hawana imani tena.

Hivi sasa  mawaziri wanajitahidi kuonyesha wanapambana na ufisadi kwenye wizara na idara zilizo chini yao, ili kuhakikisha wanarudisha heshima ya serikali kwa kuwasimamisha kazi wakurugenzi na maofisa wa ngazi za juu kwenye taasisi za umma, ambao wamebainika na tuhuma za ubadhilifu wa fedha na kushindwa kuendesha idara walizokabidhiwa.

Mawaziri waliobadilishwa wizara zao na wengine kuingia kwa mara ya kwanza kwenye baraza la mawaziri, wanaonekana kufanya kazi kwa bidii huku wakijipambanua kama wapinga ufisadi toka kuteuliwa kushika nyadhifa hizo.

Mfano wa mawaziri wanaofanya kazi kwa kasi kubwa, ni waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe ambapo awali alikuwa naibu waziri wa Ujenzi, waziri wa maliasili na utalii Balozi Hamissi Kaghasheki, kabla ya uteuzi wake alikuwa naibu  waziri wizara ya mambo ya ndani na waziri wa nishati na madini Profesa Sospetar Mhongo ambaye aliteuliwa na rais kama mbunge wa kuteuliwa na kisha kumteua kuwa waziri kamili wa wizara hiyo.

Toka uteuzi wa Dk. Mwakyembe kuongoza wizara hiyo, amemsimamishwa kazi, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ndege Tanzania (ATCL) Paul Chizi, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Ephrahim Mgawe na pia alivunja bodi ya reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) wote wakihusishwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi huku wakishindwa kusimamia na kulisababishia shirika kushindwa kujiendesha lenyewe.

Kwa upande wake Balozi Khagasheki Aliwasimamisha kazi maofisa 10 waandamizi katika wizara yake kupisha uchunguzi, huku akitangaza kuaza kazi rasmi ya kusafisha wizara hiyo.
Huku Profesa Mhongo akimsimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa shirika la umeme Tanzania (TANESCO) Willium Mhando na maofisa wengine wa ngazi za juu wa shirika hilo, ambapo ama kwa uzembe au kwa maslahi yao binafsi wamelisababishia shirika hasara kubwa.

Mawaziri hao wachache wanaonekana kufanya kazi kwa uzalendo, ukiachilia mbali waziri wa ujenzi John Pombe Magufuli na waziri wa Aridhi Nyumba na maendeleo ya makazi Profesa Anna Tibaijuka, ambapo awali walionekana kuchapa kazi bila woga wowote lakini kwa sasa inaonekana kama ilikuwa ni nguvu ya soda.

Mimi sipingani nao kabisa na namna ya uchapakazi wao wanaouonyesha, kwani kwa  kipindi cha muda mfupi toka kuteuliwa kushika nyadhifa hizo, wameonyesha uzalendo na uchungu mkubwa walionao kwa nchi yao, huku wakisema wako tayari kwa lolote hata kama ni kifo.

Hoja yangu ni kwamba je, hawa mawaziri wanaweza kusafisha ufisadi unaozidi kuitafuana serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)? Na kurudisha heshima kwa wananchi, Au wako katika hatua za kutapatapa kuokoa jahazi ilihali limezama?

Mawaziri hawa wanajitahidi sana kuonyesha uzalendo wao kwa taifa, kwa kufanya kazi bila woga huku wakihakikisha wanapambana na mafisadi walio kwenye wizara zao.
Lakini ukiangalia rekodi za nyuma, hatua hizi za mawaziri waliotangulia walianza kama wao na kuishia nguvu za soda, kwani wote waliotangulia walishindwa kusafisha kabisa uozo huo walioukuta ambapo hivi sasa umeota sungu.
Ili maendeleo yaweze kupatikana ni lazima wizara zote ziwe bega kwa bega kuhakikisha zinafanya kazi kwa pamoja, huwezi kuwa msafi katikati ya jalala lazima tu utachafuka hata kama sio nguo ulizovaa basi viatu.

Kwa huu ufisadi ambao umekuwa ukiibuliwa Nashindwa kuelewa serikali kwa kipindi chote ilikuwa wapi kuhakikisha inawasimamisha na kuwachukulia hatua kali za kinidhamu, wakurugenzi na maofisa wa ngazi za juu ambao ni wezi wa pesa za wavuja jasho huku lengo lao ni  kujinufaisha wao na familia zao?

Je, kati ya wizara 29, ni wizara tatu tu ndio mawaziri wake wamewasimamisha kazi  wakurugenzi na maofisa wa ngazi za juu kwa kosa la kufuja pesa za umma, au baadhi ya mawaziri wameshindwa kuokoa jahazi ambalo tayari limezama, na wameamua kuacha kila abilia ajitahidi kujiokoa mwenyewe na anayeshidwa afe ndani ya maji?
Lakini hoja yangu ni kwamba hawa hawawezi kupambana na mafisadi ili hali wako kwenye mfumo ule ule wa kifisadi. Ama kwa hakika watakwamishwa na vigogo wenye ushawishi mkubwa serikalini ambao ndio vinara wa ufisadi nchini.
Baadhi ya wizara zimeshakata tama na hazina tena namna ya kujinasua ili angalau kuonyesha matumaini kwa wananchi, mfano mzuri ni wizara ya Elimu,  wizara ya Afya na wizara ya Kilimo, hizi ni baadhi tu ya wizara ambazo ni mhimili mkubwa kwa taifa lakini hazijui zianzie wapi kujinasua.

Ni ngumu kukubali kuwa kwa mfumo ule ule wa awali wa uendeshaji wa serikali, hawa mawaziri wanaweza kupambana na ufisadi uliokithiri na kuota mizizi, pia huwezi kuwa msafi katikati ya jalala.
Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa