Home » » BALOZI KAGASHEKI AELEZA MASAIBU YA WIZARA YAKE

BALOZI KAGASHEKI AELEZA MASAIBU YA WIZARA YAKE

Na Thobias Mwanakatwe

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema alivyoingia katika wizara hiyo amekumbana na madudu ya ajabu likiwemo suala la wawekezaji wanaoomba kujenga hoteli za kitalii kufanyiwa urasimu na hivyo kukata tamaa kuwekeza katika sekta ya utalii nchini.

Ametoa siri hiyo juzi wakati akizungumza kwenye kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV.

Kagasheki alisema mambo aliyokumbana nayo katika sekta ya utalii ni wawekezaji wanaoomba kujenga hoteli za kitalii wanafanyiwa urasimu na watendaji wa mashirika yanayotoa vibali ambapo wanachukua zaidi ya miaka mitatu kutoa vibaji vya ujenzi wa hoteli hizo.

Alisema katika kipindi cha uongozi wake hatakubali kuona hali hiyo inajitokeza kwani pamoja na kwamba ipo sheria inayokataza mashirika ya umma kutoingiliwa lakini katika suala la utoaji wa vibali vya ujenzi wa hoteli za kitalii atalazimika kuingilia kati.

Alisema jiji kama la Mombasa na Nairobi nchini Kenya hoteli za kitalii zimejengwa kila kona  na ndiyo maana nchi hiyo idadi ya watilii wanaoingia kwa mwaka ni 1,200,000 wakati Tanzania inapokea watalii 800,000 tu ambapo tunakaribiana na nchi kama Rwanda ambayo inapokea watalii 600,000.

Kagasheki alisema atahakikisha ifikapo mwaka 2015 idadi ya watalii wanaoingia nchini inafikia 1,000,000 ili kusaidia kuongeza mapato la nchi.

Alisema suala la kutangaza sekta ya utalii bado ni tatizo nchini ambapo katika kipindi cha mwaka jana fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutangaza utalii zilikuwa ni dola za Marekani milioni 2.5 tu wakati Kenya ni dola milioni 24 na Afrika Kusini ni milioni 75.

Kuhusu faru wa JK waliouwawa, alisema tukio la kuuawa faru wawili walioletwa nchini na Rais Jakaya Kikwete linasikitisha kwani kilichotokea ni uzembe na lilifanywa kwa makusudi.

Kagasheki alisema uchunguzi wa mauaji ya faru hao umefanyika ambapo wapo watendaji waliochukuliwa hatua na imebainika kuna mtandao mkubwa wa watu waliohusika katika hujuma hiyo.

Akizungumzia biashara ya wanyama hai, alisema serikali imeisitisha kwa muda ili kupitia sheria upya na baada ya kufanyia marekebisho sheria biashara hiyo itarejeshwa.


 
Chanzo: Nipashe

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa