Home » » MSHITAKIWA ATISHIA KUUA WANAHABARI DAR

MSHITAKIWA ATISHIA KUUA WANAHABARI DAR

na Nasra Abdallah
MMOJA wa washitakiwa katika kesi ya wizi wa madini ya shaba yenye thamani ya sh milioni 400, inayomkabili Katibu wa zamani wa klabu ya Simba, Hassan Hassanol (43), na wenzake watatu ametishia kuwaua waandishi wa habari waliokuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakitimiza wajibu wao.
Mtuhumiwa aliyewatishia kuwaua waandishi wa habari ni Dk. Najim Msenga (50), baada ya mpiga picha wa Kampuni ya Mwananchi Communication, Venance Nestory, kumpiga picha alipokuwa akitoka mahakamani.
Mbali ya Nestory, waandishi wengine waliotishiwa maisha ni Rose Japhet (TBC), Njumai Ngota (Uhuru), Regina Kumba (Habari Leo), Tausi Ally (Mwananchi) na mwandishi wa habari hizi.
Baada ya kuona anapigwa picha, Dk. Msenga, alisikika akisema kuwa atawaua waandishi hao kwa madai kuwa wamekuwa wakiwafuatilia sana na kutamba kuwa yeye haogopi sheria.
Mbali ya kauli hiyo, pia alianza kuwarushia matusi, hali liliyomlazimu mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo, Salim Shekibala, kwa kushirikiana na maofisa wa mahakama kuingilia kati.
Kutokana na tukio hilo, waandishi hao walikwenda kutoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi na kufungua RB yenye namba CD/RB/9831/2012 CD/IR/3572/2012 ya kutishiwa kuuawa kwa maneno.
Awali, wakili wa serikali katika kesi hiyo, Teophili Mutakyawa, alimuomba Hakimu Devota Kisoka kuongeza shitaka la nne ambapo linamuhusu mshitakiwa wa pili na wa tatu ambapo ingebidi kusoma upya maelezo ya awali na thamani ya mali iliyoibwa.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Majura Magafu, alipinga ombi hilo kwa madai kesi ikishaanza kusikilizwa haitakiwi kufanyika kwa uchunguzi mwingine.
Kutokana na mabishano hayo, Hakimu Kisoka, aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 25, mwaka huu atakapotoa uamuzi kuhusu suala hilo.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa