Home » » SUMATRA YAPIGA MARUFUKU USAFIRI WA NOAH

SUMATRA YAPIGA MARUFUKU USAFIRI WA NOAH

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imepiga marufuku usafirishaji wa abiria unaofanywa na magari aina ya Noah maarufu kama michomoko.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya wadau wa usafiri kutoa malalamiko yao juu ya hatua ya mamlaka hiyo kuruhusu magari ya aina hiyo, kusafirisha abiria hali inayosababisha ajali kila wakati.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano wa SUMATRA, David Mziray, alisema utolewaji wa leseni kwa magari hayo ulitolewa kwa ajili ya usafirishaji wa watalii hasa kwa Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Alisema wamiliki wa magari hayo hawakuzingatia masharti ya leseni ya usafirishaji kwa kuwa badala ya kusafirisha watalii na kujiingiza katika biashara ya usafiri wa umma na hivyo kuzusha migogoro kati ya wasafirishaji wa magari makubwa katika njia hizo na wamiliki wa Noah.

Alisema kutokana na mgogoro uliojitokeza wa wasafirishaji SUMATRA iliona ni vema kukutana na wadau wa usafiri katika mikoa husika kwa lengo la kujua hali halisi ya usafiri katika mikoa hiyo pamoja na kujua kero za wananchi kwa ujumla kuweza kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

“Katika mikutano hiyo, changamoto mbalimbali za masuala ya usafirishaji zilijadiliwa zikiwamo ajali za barabarani, upandishwaji holela wa nauli pamoja na vurugu za mara kwa mara, zinazosababishwa na waendeshaji wa magari ya Noah ambayo hayakuwa na leseni za usafirishaji.

“Baada ya kutathimini changamoto mbalimbali zilizojadiliwa katika mikutano hiyo, Mamlaka ilifanya tathimini ya utendaji kazi wa aina hii ya magari ya Noah na kubaini kuwa, kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa abiria na wasafirishaji wa mabasi makubwa wanaotoa huduma ya usafiri katika maeneo ambayo magari ya Noah yakitoa huduma.

“Baadhi ya malalamiko yaliyotolewa na abiria waliotumia huduma ya magari ya Noah ni pamoja na abiria kutozwa nauli kubwa zaidi ya viwango vilivyoridhiwa na mamlaka, abiria kuhoji umbali unaoruhusiwa kwenda magari hayo pamoja na uimara wa bodi ya magari hayo kwa kubeba abiria na mizigo.

“Baada ya SUMATRA kupokea malalamiko hayo Mamlaka ilifanya tathmini kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kubaini kuwa uwezo wa magari hayo, kutumika kama usafiri wa umma ni mdogo na hivyo kuifanya biashara ya usafirishaji kwa kutumia magari hayo kutokuwa na tija.

“Magari ya aina hiyo madirisha yake ni madogo na hayana milango ya dharura. Aidha, magari hayo hayakidhi matakwa ya kifungu namba 4.4.3 cha Kiwango Na. 598:1999 pamoja na Kifungu Namba 5.2.1 – 5.3.5 Kiwango TZS 598 (Part 3): 2010 cha TBS kwa magari ya abiria. Vifungu hivyo vinaeleza viwango vya bodi, madirisha na urefu katika gari la abiria,” alisema Mziray.

Alisema kutokana na hali hiyo, SUMATRA ilifikia uamuzi wa kusitisha utoaji wa leseni hizo baada ya kutathimini malalamiko na hoja mbalimbali zilizotolewa na wadau wa usafiri.

Aidha, alisema SUMATRA katika kusimamia sekta ya usafirishaji abiria kwa njia ya barabara, imetoa uamuzi wa hadi kufikia Januari 10, 2013 hakutakuwa na utoaji wa leseni za usafiri wa umma kwa msafirishaji mpya anayemiliki gari la Noah.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya magari aina ya Noah yatakayohitaji kufanya biashara ya usafirishaji abiria yataruhusiwa kwa kupewa leseni ya kutoa huduma ya usafiri kwa watalii tu.

Alisema kwa mmiliki wa Noah mwenye leseni ya usafirishaji, aliruhusiwa kuendeleza leseni hiyo na hadi Juni 30, mwaka huu ambapo mwisho wa leseni zote utakuwa ni Juni 29, mwaka huu.

Kutokana na hatua hiyo, alisema matumizi ya magari hayo yana hatari ya kudumaza au kudidimiza sekta ya usafirishaji kwa waagizaji wa mabasi makubwa kuacha kuagiza mabasi hayo yenye uwezo mkubwa wa kubeba abiria wengi kwa pamoja

Mbali na hatua hiyo, alisema magari mengi ya Noah yenye uwezo wa kubeba abiria wachache, yamebainika kuwapo kwa uwezekano mkubwa wa msongamano wa magari katika miji ya mikoa hiyo pamoja na abiria kukosa haki ya msingi ya kusafiri na mzigo usiozidi kilo 20, ambapo ni kinyume na kanuni Na. 23 (1) ya kanuni za leseni za usafirishaji magari ya abiria mwaka 2007.

“Pia iliamuliwa kuwa wasafirishaji wote wa leseni za Noah, watakaoendeleza leseni zao kila moja itaishia kwa utaratibu wake kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa leseni hizo kama kanuni inavyoelekeza.

“Misingi ya uamuzi wa SUMATRA imezingatia kifungu namba 5 cha Sheria ya SUMATRA, Sura ya 314, Mamlaka inalo jukumu la kisheria la kulinda maslahi ya watumiaji pamoja na watoa huduma wa sekta inazozidhibiti,” alisema Mziray.

Aidha, kifungu Namba 6 cha Sheria hiyo, kinaipa Mamlaka hiyo wajibu wa kuhakikisha huduma zinazotolewa na sekta inazozidhibiti, zinatolewa katika ubora unaokubalika na kwa gharama zinazostahili.

Kutokana na sababu za kiusalama, magari ya Noah hayakidhi viwango vya usalama kwa magari ya umma kwa kuwa hayakidhi matakwa ya kifungu namba 4.4.3 cha Kiwango Na. 598:1999 cha TBS kwa magari ya abiria.

Alisema SUMATRA inaendelea na kazi kuyaondoa mabasi madogo, yaani vipanya na kuhamasisha matumizi ya mabasi makubwa yenye faida kiuchumi kwa mtoa huduma na mtumia huduma.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa