Na Benjamin Masese, Dar e s Salaam
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua za El nino zinatarajia kunyesha Oktoba hadi Desemba mwaka huu. Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Dk. Kijazi, mvua hizo zitasababishwa na hali ya joto la bahari katika ukanda wa tropikali wa Bahari ya Pasifiki kuwa juu ya wastani na kuashiria uwepo wa mvua hizo.
Hata hivyo, alisema El-nino ya mwaka huu haitafikia kiwango cha ile iliyonyesha mwaka 1997 na kusababisha madhara makubwa kwa wananchi.
Pamoja na hayo, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari mapema, ili kuepuka madhara yaliyowahi kutokea katika mvua zilizowahi kunyesha.
“Kwa maana hiyo, naziomba wizara zinazohusika na masuala ya nishati, maji, afya, maafa, kilimo na nyingine, zichukue tahadhari mapema, ili kuepusha athari zitakazoweza kujitokeza kwa sababu mvua hizo zinatarajiwa kusababisha upepo mkali utakaokuwa ukivuma kutoka Kaskazini Mashariki hadi Mashariki na kusababisha matukio ya vimbunga.
“Wanasayansi kutoka taasisi za hali ya hewa walioko katika nchi za Pembe ya Afrika, Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania, walikutana Zanzibar Agosti 29 mwaka huu, kujadili uelekeo wa mvua za msimu katika ukanda huu.
“Pamoja na mambo mengine, tathmini ya kina iliyofanyika katika mifumo ya hali ya hewa na athari zake, imeonyesha kuwa na viashiria vingi vya kuwapo kwa mvua ikiwa ni pamoja na hali ya joto la bahari kupanda maeneo ya Bahari ya Hindi.
“Hivyo, tunazidi kuziomba wizara na taasisi zinazohusika na maji, nishati, mamlaka za miji, sekta za afya, idara ya maafa na wanahabari kuchukua tahadhari mapema, sambamba na kufuatilia taarifa zitakazokuwa zikitolewa na TMA mara kwa mara.
“Hakika kila mmoja akishirikiana na mwingine kwa kutekeleza majukumu yake kutokana na utabiri huu, tutaepusha magonjwa, vifo na mambo mengine yasiyofaa,” alisema Dk. Kijazi.
Dk. Kijazi alisema kuwa, Kanda ya Ziwa Victoria mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya mwezi huu na zitakuwa juu ya wastani katika mikoa hiyo.
Alisema ukanda wa Pwani ya Kaskazini pamoja na Visiwa vya Pemba na Unguja, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya Oktoba na zitakuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo hayo.
Alisema kwamba, nyanda za juu Kaskazini Mashariki, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya Oktoba na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Kanda ya Magharibi mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya Oktoba katika Mkoa wa Kigoma, lakini katika mikoa ya Tabora, Rukwa na Katavi, zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya Novemba.
Dk. Kijazi alisema Kanda ya Kati, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Novemba na zitakuwa za juu ya wastani pia Nyanda za Juu Kusini Magharibi mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Novemba, ambapo zitakuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Maeneo ya Kusini na Pwani ya Kusini, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Novemba na zitakuwa wastani hadi juu ya wastani katika mikoa hiyo.
“Mwelekeo wa utabiri huu, umezingatia zaidi kipindi cha msimu wa miezi mitatu na hali ya mvua katika maeneo makubwa, lakini TMA itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa pamoja na uwezekano wa kutokea vimbunga katika Bahari ya Hindi.
“Katika mvua hizo, tunatoa ushauri kwa wale watu wa mifugo, wanyama pori, kilimo na usalama wa chakula, kutumia mvua hizo kwa manufaa ili kuepusha kuleta athari za kiuchumi na kijamii,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwamba, viwango vya mvua chini ya asilimia75 ya wastani kwa kipindi kirefu, hutafsiriwa kama chini ya wastani wakati viwango vya kati ya asilimia 75 na 125, hutafsiriwa kama mvua za wastani na vile vilivyo zaidi ya asilimia 125 hutafsiriwa kama juu ya wastani.
Alisema kwamba, wakati Tanzania ikiwa na mvua nyingi, maeneo mengine duniani yanakuwa na ukame mkubwa.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:
Post a Comment