na Asha Bani
KATIBU
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi, amemteua Profesa
Alexander Songorwa kuwa Mkurugenzi mpya wa Idara ya Wanyamapori, akichukua
nafasi ya Obeid Mbangwa, aliyetimuliwa kazi na Khamis Kagasheki.
Msaidizi
wa Mbangwa ni Bonaventura Midala na watendaji wengine ambao walisimamishwa kazi
baada ya kubainika kuhusika katika kashfa ya utoroshaji wanyamapori hai kupitia
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda nje.
Taarifa
ya Katibu Mkuu kwa vyombo vya habari, iliyotolewa jana na msemaji mkuu wa
wizara hiyo, George Matiko, ilieleza kuwa kabla ya utezi huo, Prof. Songorwa
alikuwa Profesa Mshiriki katika Usimamizi wa Wanyamapori, Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) cha Morogoro na alikuwa Mkuu wa Idara hiyo ya
usimamizi wa Wanyamapori chuoni hapo.
Tarishi
pia amemteua Profesa Jafari Kideghesho kuwa Mkurugenzi Msaidizi, kuiongoza
sehemu ya matumizi endelevu ya wanyamapori.
Uteuzi
huo umefanyika baada ya vigogo watatu kugundulika kuhusika katika kashfa hiyo
ambapo wanadaiwa kusafirisha wanyamapori hai 116 na ndege 16 Novemba 24 mwaka
2010, kwenda nje ya nchi kupitia KIA.
Wengine
waliohusika katika sakata hilo ni Simon Charles Gwera, Ofisa Uwindaji wa
Kitalii Cites na Utalii wa Picha – Arusha, na Frank Mremi, Ofisa Uwindaji wa
Kitalii Cites na Utalii wa Picha-Arusha.
Taarifa
ya uteuzi huo ilifafanua kuwa Katibu Mkuu ameufanya kwa mamlaka aliyonayo kwa
mujibu wa kifungu cha 6(1) (b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka
2002 ambapo utekelezaji wake utaanza mara moja kuanzia kesho.
Akielezea
wasifu wa Prof. Songorwa, alisema ana shahada ya kwanza (B.Sc.) ya sayansi
katika zoolojia na ekolojia ya wanyamapori ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam
(mwaka 1987), shahada ya uzamili (MSc) katika Mipango na Maendeleo Vijijini ya
Chuo Kikuu cha Guelph, Ontario, Canada (1994).
Aidha,
anayo shahada ya uzamivu (PhD) katika Uhifadhi Maliasili ya Chuo Kikuu cha
Lincoln, New Zealand (1999) kabla ya kujiunga na SUA mwaka 2001, Prof. Songorwa
alikuwa mwajiriwa wa Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili kuanzia
mwaka 1982.
Akiwa
wizarani hapo alikuwa akitumikia nafasi mbalimbali zikiwemo Askari Wanyamapori,
Mkuu wa Kanda na msaidizi wa mkuu wa mradi katika Pori la Akiba la Selous.
Naye
Prof. Kideghesho si mgeni katika Idara ya Wanyamapori ambapo kabla ya kujiunga
na SUA mwaka 1999 alikuwa mwalimu katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori
Mweka (CAWM-Mweka) Moshi kuanzia 1993.
Kitaaluma
Prof. Kideghesho ana shahada ya kwaza (B.Sc.) katika Kilimo ya SUA (1993),
Shahada ya Uzamili (MSc) katika Biolojia ya Uhifadhi ya Chuo Kikuu cha Kent,
Uingereza (1996), na Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Chuo Kikuu cha Sayansi na
Teknolojia cha Norway kilichopo mjini Trondheim (2006).
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment