Na
Mwandishi wetu
Matengenezo
ya rada ya kuongozea ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere (JNIA) iliyoharibika mwanzoni mwa Oktoba, mwaka huu, yamekamilika, huku
mtaalamu kutoka Afrika Kusini akiifanyia ukaguzi wa kina zaidi.
Matengenezo ya rada hiyo yaliyofanywa na mtaalamu kutoka nchini Kenya,
yalikamilika juzi.
Hadi kufikia jana, mtaalamu mwingine kutoka Afrika ya Kusini alikuwa anaikagua
ili kubaini tatizo linalosababisha vifaa vilivyomo ndani ya rada hiyo
kuharibika kila mara, pamoja na kuikagua kama matengenezo hayo yalifanyika
vizuri.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege, Fadhili Manongi, alisema matengenezo ya kifaa
kilichoharibika yamekamilika.
Alisema zoezi linalofanyika kwa sasa (jana), ni kuifanyia uchunguzi wa kina
unaofanywa na mtaalamu kutoka Afrika Kusini.
“Matengenezo yamekamilika jana (juzi) jioni na leo (jana) mtaalamu kutoka
Afrika Kusini anaikagua. Tunatarajia kuiwasha majira ya jioni. Kuna rada aina
ya “Primary” na “Secondary”. Sasa primary inafanya kazi. Ila Secondary
tumeizima na tunatarajia kuiwasha jioni,” alisema Manongi.
Rada hiyo iliharibika kufuatia kifaa kilichopo kinachotumika kusambazia umeme
kiitwacho UPS au “Power Suply” kuungua zaidi ya wiki mbili iliyopita na tatizo
ndani ya rada hiyo lilianza kuonekana tangu siku walipoifanyia ukarabati
(Agosti 18, mwaka huu) kwa kuanza kuonyesha taa nyekundu ikiashiria kuna
hitilafu ndani ya chombo hicho.
Chanzo:
Nipashe
0 comments:
Post a Comment