Home » » JOHN MNYIKA:KAULI TATA KUHUSU HALI TETE YA UMEME, UKWELI KWA UKAMILIFU UELEZWE

JOHN MNYIKA:KAULI TATA KUHUSU HALI TETE YA UMEME, UKWELI KWA UKAMILIFU UELEZWE


Mbunge wa Ubungo-Chadema, Mheshimiwa John Mnyika
--
Katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja kuanzia mwanzoni mwa
mwezi Septemba 2012 mpaka leo tarehe 21 Oktoba 2012  viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na
Madini na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wamenukuliwa na vyombo vya habari na
wakitoa matumaini potofu kwa wananchi kuhusu hali ya uzalishaji, usafirishaji
na usambazaji wa umeme nchini sanjari na
uboreshaji
wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO).

Viongozi na watendaji hao waliozungumza kwa nyakati tofauti na
kutoa kauli mbalimbali ni pamoja Waziri Prof. Sospeter Muhongo, Naibu Waziri wa
Nishati George Simbachawene, Katibu Mkuu wa Wizara Eliackim Maswi na Kaimu
Mkurugenzi wa TANESCO Felchesmi Mramba.

Kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini natoa
mwito kwa wanahabari na umma kuzipokea kwa tahadhari kauli hizo kwa kuwa
hazielezi ukweli kamili kuhusu hali tete ya umeme kutokana na kususua katika
utekelezaji wa Mpango wa Dharura wa Umeme kama nilivyohoji bungeni tarehe 27
Julai 2012.

Kwa mujibu wa nyaraka nilizo nazo za ndani ya Wizara ya Nishati
na Madini na TANESCO kuanzia mwezi Septemba mpaka mwezi Oktoba 2012 hali ya
uzalishaji na usafirishaji na usambazaji wa umeme imekuwa tete kwa sababu
mbalimbali ikiwemo upungufu wa upatikanaji wa mafuta na gesi asili kwa ajili
uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme na kasi ndogo ya uwekezaji kwa ajili ya
kupata ufumbuzi wa kudumu.

Hali hii imesababisha mpaka wakati mwingine umeme kutoka kwenye
mabwawa kuzalishwa zaidi ya kiwango kilichopangwa na kusababisha kushuka kwa
kina cha maji hali yenye kutishia uendelevu wa mabwawa haya kutokana  na maelekezo ya Wizara kwa TANESCO ya
kuhakikisha mgawo wa umeme hautangazwi kwa namna yoyote.

Kutokana na hali hiyo na kwa kuzingatia kuwa mamlaka na madaraka
ya Bunge kwa mujibu wa katiba ni kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi nimemwandikia
barua Spika wa Bunge ili Wizara ya Nishati na Madini iwajibike kueleza halisi
halisi katika mikutano ya kamati za bunge inayoendelea hivi sasa.

Aidha, kwa kuwa kwa sasa Nchi haina Kamati ya Bunge ya Nishati
na Madini ambapo Wizara ingelazimika kueleza ukweli kamili na halisi
nimemwandikia Spika atumie madaraka na mamlaka yake kwa mujibu wa Kanuni ya 116
na Kanuni ya 114 fasili ya 14 kukabidhi suala hilo lishughulikiwe na kamati
nyingine miongoni mwa Kamati za Kudumu za Bunge zinazoendelea na vikao vyake
hivi sasa.

Kwa barua hiyo nimependekeza pamoja na mambo mengine suala la
kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Dharura wa Umeme na
utekelezaji
wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO)
lishughulikiwe na kamati nyingine kwa haraka kwa kuzingatia maelezo na
maelekezo ya Spika aliyoyatoa bungeni wakati wa kuahirisha mkutano wa nane wa
Bunge.

Nitakabidhi sehemu ya nyaraka nilizonazo kwa Kamati ya Kudumu ya
Bunge itakayoelekezwa na Spika kushughulikia jambo hili lakini iwapo hatua za
haraka hazitachuliwa nitatoa baadhi ya nyaraka hizo kwa wanahabari na umma ili
Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO wawajibishwe kueleza ukweli kwa
ukamilifu.

Kwa upande mwingine, mapitio ya utekelezaji
wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) yahusishe pia
Kamati ya Kudumu ya Bunge itakayopewa jukumu hilo kuelezwa hatua iliyofikiwa
katika uchunguzi wa tuhuma za ufisadi katika TANESCO kwa kuzingatia kuwa siku
60 zimepita ambazo ilielezwa kuwa uchunguzi utakuwa umekamilika.

Ikumbukwe
kwamba mwanzoni mwezi Agosti Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT)
iliunda timu ya wakaguzi kufanya ukaguzi maalum wa hesabu za Shirika la Umeme
(TANESCO) kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma zilitajwa bungeni na
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani
tarehe 27 Julai 2012 na Waziri wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya
hoja ya Serikali tarehe 28 Julai 2012.

Aidha
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) nayo ilinukuliwa na baadhi ya
vyombo vya habari mwezi Agosti mwanzoni kuanza uchunguzi wa mchakato wa ununuzi
wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme wa dharura kutokana na
tuhuma mbalimbali zilizotolewa bungeni kuhusu ununuzi huo suala ambalo Kambi
Rasmi ya Upinzani ilitaka pia tarehe 27 Julai 2012 liundiwe kamati teule ya
Bunge ili uchunguzi wa kina uweze kufanyika.

Masuala haya ni muhimu yakafuatiliwa wakati wa vikao vya kamati
za kudumu za Bunge vinavyoendelea hivi sasa kwa kuzingatia wakati Mkutano wa
Nane wa Bunge uliopita pamoja na Spika kutangaza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Nishati na Madini imevunjwa alieleza kuwa majukumu yaliyokuwa yakishughulikiwa
na kamati hiyo yatashughulikiwa na kamati nyingine kwa mujibu wa madaraka na
mamlaka ya Spika.

Hivyo Spika anapaswa kuizingatia
barua yangu na kutoa pia kauli kwa umma ya kuwezesha mambo hayo na
mengine kushughulikiwa na Kamati nyingine ya Kudumu ya Bunge atakayoelekeza ili
kusiwe na kisingizio cha kutokuingizwa katika ratiba ya mkutano wa tisa wa
Bunge uliopangwa kuanza tarehe 30 Oktoba 2012.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
21 Oktoba 2012

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa