Home » » Jaji Warioba: Huu sio wakati wa kupiga kura, tunatafuta hoja

Jaji Warioba: Huu sio wakati wa kupiga kura, tunatafuta hoja


Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba (kulia)
akizungumza na wajumbe wa kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala
wakati wa ziara iliyoanywa na wajumbe hao leo jumanne tarehe 16.Oktoba,
2012  ya kutembelea vitengo mbalimbali vilivyopo katika Makao Makuu ya
Tume hiyo Jijiini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria, Angellah Kairuki na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pindi Chana.


Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, (kulia)
akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria
na Utawala, Pindi Chana (katikati) wakati kamati hiyo iliyofanywa leo
jumanne tarehe 16. Oktoba, 2012 na kutembelea vitengo mbalimbali
vilivyopo katika  makao makuu ya Tume hiyo Jijini Dar es Salaam. Kushoto
ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki.


Katibu
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba akibadilishana mawazo na wajumbe wa
kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala wakati wa ziara ya wajumbe
hao iliyofanywa leo jumanne tarehe 16.Oktoba, 2012 na kutembela vitengo
mbalimbali vilivyopo katika Makao Makuu ya Tume hiyo, Jijini Dar es
Salaam. Kutoka Kulia ni wajumbe wa Kamati hiyo, Rashid Ali Abdalla,
Deogratius Ntukamazina, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki na Felix Mkosamali. (Picha na Tume ya Katiba


…………………………………………………


Na Mwandishi Wetu


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba Jaji Joseph Warioba amesisitiza umumihu wa wananchi kutoa
maoni maoni yao kuhusu Katiba Mpya badala ya kukimbilia kuwasilisha
maoni waliyolishwa na viongozi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia na
kidini.


Jaji Warioba ameyasema hayo leo
(Jumanne, Oktoba 16, 2012) katika mkutano kati ya Kamati ya Bunge ya
Katiba, Sheria na Utawala na uongozi wa Tume hiyo uliofanyika katika
ofisi za Tume jijini Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa Waziri Mkuu
Mstaafu huyo baadhi ya viongozi hao na wadau wengine wanadhani maamuzi
ya kazi ya kukusanya maoni inayofanywa kwa sasa na Tume yatamuliwa kwa
kura na hivyo kuwalisha wananchi maoni ili wayatoa kwa Tume kwa wingi.




“Wengine wanafikiri huu ni
wakati wa kupiga kura…hapana, sisi tunatafuta hoja,” alisema Mwenyekiti
huyo na kuwataka wadau mbalimbali kuwaacha wananchi watoe maoni yao
binafsi.




Awali akiongea katika mkutano
huo, Mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Muhambwe, Bw. Felix
Mkosamali alipendekeza Tume iwe inagawa kwa wananchi fomu maalum za
kujaza maoni yao siku kadhaa kabla ya Tume kufika ili kuwapa wananchi
fursa ya kuandika maoni kwa kina tofauti na sasa ambapo Tume hutoa
karatasi hizo kabla ya kuanza mkutano.


Akifafanua kuhusu hilo, Jaji
Warioba amesema uamuzi wa Tume kugawa fomu hizo mkutanoni unalenga
kupata maoni binafsi ya wananchi na kuongeza kuwa fomu hizo zikigawiwa
mapema kuna uwezekano mkubwa kwa wananchi kujaziwa maoni na watu
wengine.


“Uzoefu wetu umeonyesha hili la
watu kuelekezwa nini cha kusema ambacho kwa kwli hawavijui kwa kina,”
alisema katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Katiba
na Sheria Angellah Kairuki, Katibu wa Tume hiyo Bw. Assaa Rashid na
Naibu Katibu Bw. Casmir Kyuki.




Pamoja na ufafanuzi kuhusu
utoaji maoni binafsi ya wananchi, Mwenyekiti huyo pia aliwaeleza Wajumbe
wa Kamati hiyo  kuwa lengo la Tume ni kuhakikisha kuwa mchakato wote wa
uandikaji wa katiba unakuwa wazi na wananchi wanashiriki kikamilifu.


“Tukimaliza kukusanya maoni,
tutaingia hatua ya pili ya Mabaraza ya Katiba katika kila wilaya na
baadhi ya taasisi ambapo tunataka wananchi wenyewe katika maeneo husika
wachague nani awawakilishe katika mabaraza hayo,” alisema Mwenyekiti
huyo.


Ufafanuzi huu ulifuatia swali la
Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, Bi. Halima Mdee
aliyeomba ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
ambayo yanapitia rasimu ya Katiba itakayowasilishwa na Tume.




Akifafanua zaidi, Jaji Warioba
alisema Tume imepanga kufanya mikutano miwili katika kila wilaya ambapo
wawakilishi wa wananchi watajadili rasimu ya Katiba itakayowasilishwa na
Tume baada ya kukusanya maoni yao katika awamu ya kwanza.




“Ni hatua ambayo tunadhani
itahitaji fedha nyingi hasa katika kuwasafirisha hao wawakilishi wa
wananchi kuja katika mikutano…hatutaki kuona wananchi wanapata sababu ya
kutoshiriki hatua hii muhimu,” alisema na kuwaomba Wajumbe wa Kamati
kuzingatia hoja hizo pale Tume itakapoomba fedha zaidi.




Pamoja na maoni hayo, Wajumbe
hao pia waliieleza Tume umuhimu wa kuongeza utoaji elimu kwa umma kuhusu
masuala mbalimbali yanayohusu Tume na Katiba.




Kwa upande wake, Naibu Waziri
Kairuki alisema Serikali itaendelea kuipa Tume hiyo kila aina ya
ushirikiano ili itekeleze majukumu yake kwa ufanisi na kuwaomba Wabunge
hao kuendeleza ushirikiano wanaoipa Tume hiyo.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa