Home »
» KINGELEZA CHAMPONZA: NENO NEGATIVE LAMFANYA AJIUE AKIDHANI ANA VVU
KINGELEZA CHAMPONZA: NENO NEGATIVE LAMFANYA AJIUE AKIDHANI ANA VVU
Na Zubeda Mazunde
KATIKA kile kinachoonesha watu wengi hawapo tayari kupokea matokeo ya vipimo
vya Virusi vya UKIMWI (VVU), mkazi wa Tegeta, jijini Dar es Salaam, Bw. Juma
Hussen (18) amejiua baada ya kupima VVU na vipimo vyake kuonesha yupo Negative.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Bw. Charless Kenyela, aliwaambia waandishi
wa habari jana, kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 7 mchana, ambapo marehemu
alikunywa sumu aina ya NUVAN 500CC, akidhani kwamba kipimo kikionesha Negative
maana yake ana virusi vya UKIMWI.
Alisema baada ya mtu huyo kwenda kupima afya yake hospitalini (hakuitaja jina)
alipewa karatasi inayoonesha kufanya kipimo hicho cha HIV na majibu yake
kuonekana yupo Negative.
Kwa mujibu wa Bw. Kinyela majibu hayo ya kuonekana Negative yalimpa hofu, kwani
aliamini kuwa Negative maana yake ni kuwa na virusi vya UKIMWI, wakati si
kweli.
Bw. Kenyela aliendelea kusema kuwa mtu huyo aliacha ujumbe kwenye note book
yake unaosema kuwa; " Nawaaga ndugu zangu nimeamuwa kunywa sumu hii kwa
sababu nimekutwa na ugonjwa huu wa virusi vya UKIMWI, na ugonjwa huu
aliyeniambukiza ni Asha."
Alisema wasamaria wema walimkuta mtu huyo akiwa hajafariki, hivyo kukimbizwa
kwenye zahanati ya Mico ambapo alifariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Bw. Kinyela pembeni mwa mtu huyo ilikutwa note book yenye ujumbe
huo na chupa ya sumu aliyokunywa.
Alisema mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala
jijini Dar.
Chanzo: Majira
0 comments:
Post a Comment