Home » » HALIMA MDEE AMVAA MCHUNGAJI RWAKATARE, NI KATIKA SAKATA LA HEKALU LAKE LINALOTAKIWA KUVUNJWA, ASEMA VIONGOZI WA AINA HIYO AIBU KWA TAIFA, ADAI ITATAFSIRIWA SERIKALI IMEWEKWA MFUKONI

HALIMA MDEE AMVAA MCHUNGAJI RWAKATARE, NI KATIKA SAKATA LA HEKALU LAKE LINALOTAKIWA KUVUNJWA, ASEMA VIONGOZI WA AINA HIYO AIBU KWA TAIFA, ADAI ITATAFSIRIWA SERIKALI IMEWEKWA MFUKONI




Goodluck Hongo

MBUNGE wa Kawe na Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Halima Mdee, ameshangazwa na hatua ya Serikali kukaa kimya, bila ya kuchukua hatua za kubomoa nyumba ya Mchungaji Getrude Rwakatare, iliyopo Mbezi, jijini Dar es Salaam, inayoelezwa kujengwa kwenye viwanja ambavyo ni kinyume cha sheria.


Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na mbunge huyo Dar es Salaam jana, ilieleza kuwa nyumba hiyo ya Mchungaji Rwakatare, ilistahili kubomolewa.

"Nyumba ambayo ilipaswa kuwa imebomolewa kwa sababu imejengwa kwenye viwanja ambavyo ni kinyume cha sheria kujenga katika maeneo hayo, kuvunja sheria kwa uwazi namna hii, huku wengine wakichukuliwa hatua kwa kuvunja sheria hiyo hiyo, si tu ni ’double standards’, bali kunaweza kutafsiriwa ni kuitia serikali mfukoni," alisema Bi. Mdee.

Aliongeza kuwa wananchi wanaofahamu ukweli wa mambo, wakiwa bado wanahoji chinichini juu ya upendeleo wa kitabaka ulio wazi, hivi karibuni wameshuhudia kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari, ikiripotiwa kuwa Mchungaji Rwakatare, amehamia kwenye nyumba yake. 

"Kitu kibaya zaidi ni kwamba kiongozi huyo alishataarifiwa tangu mapema juu ya ubatili wa kujenga katika eneo hilo, kupitia kwa mtu mmoja (jina linahifadhi) kabla hata ujenzi wa nyumba hiyo haujaanza," alizidi kulalamika Bi. Mdee. 

Aliongeza kuwa viwanja hivyo vilipatikana na ujenzi huo kuwezekana baada ya eneo la bahari na mto kujazwa kifusi na mawe!

Alisisitiza kuwa ujenzi katika eneo hilo ni kuvunja sheria za nchi zinazohusu utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya jamii nzima.

"Mchungaji Rwakatare aliendelea kujificha nyuma ya mgongo wa mtu huyo, akijifanya  hahusiki kabisa na kilichokuwa kikiendelea katika eneo husika," alisema Bi. Mdee

Aliongeza kuwa Januria 4, 2011 Wizara ya Ardhi kupitia barua yenye Kum. Namba LD/297571/18 iliandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuhusiana na uvamizi wa kiwanja namba 2019 na 2020 Mbezi Kawe. 

Bi. Mdee alisema katika barua husika pamoja na mambo mengine, ilibainisha kuwa wizara imefanya ukaguzi katika viwanja tajwa, baada ya kupata malalamiko juu ya uharibifu wa mazingira unaoendelea katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa Bi. Mdee barua hiyo ilieleza kuwa ukaguzi walioufanya umeonesha kuwa ujenzi unaofanyika katika eneo husika hauruhusiwi na unakiuka Tangazo la Serikali (GN) No. 76 ya mwaka 1992. 

Alisema kupitia barua hiyo, wizara ilimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kuchukua hatua za kubomoa/kuondoa uendelezaji batili uliokuwa ukifanyika katika viwanja Na 2019 na 2020 Mbezi Kawe.

Kwa mujibu wa mbunge huyo barua hiyo ilisainiwa na Bw. Sadoth K. Kyaruzi, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara.

Aliongeza kuwa uthibitisho mwingine ni barua ya Septemba 30, 2011 kutoka NEMC kwenda kwa Bw. Frank Mushi. Kwa kujibu wa Bi. Mdee barua husika, ilitoa maelekezo kwa Mushi kuvirudisha katika hali yake ya kawaida, viwanja namba 2019-2020 kwa mujibu wa vifungu 55(2) (a) (e), (3) na 151 (1) ,(2) (a), (b), (3) ,(4) (b) na (f) vya Sheria ya Mazingira, sura 191 ya mwaka 2004.

"Barua husika inabainisha kwamba timu ya wataalam NMC, Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Kinondoni ilitembelea eneo husika kufuatia malalamiko kutoka kwa viongozi na wakazi wa Kawe Beach," alisema Bi. Mdee akinukuu barua hiyo na kuongeza;

"Timu hiyo ilibaini kwamba eneo la Mto Ndumbwi, pamoja na bahari lilikuwa linajazwa mawe na vifusi hali iliyosababisha kupatikana kwa viwanja na 2019 na 2020. Ambapo ndani ya viwanja hivyo lilikuwa linajengwa jumba kubwa kinyume kabisa na vifungu 55(2)(a) , 55(2) (b) , 55(2)(d) na 55(2)(e) vya Sheria ya Mazingira. Ilibainika pia kuwa mikoko ilikatwa kinyume na s.63(1) ya Sheria ya Mazingira."

Alisema NEMC iliagiza kusitishwa ujenzi mara moja, kuvunja majengo yote yaliyoko kwenye viwanja vyenye mgogoro ndani ya siku saba tangu amri husika kutolewa Septemba 30, mwaka jana.

" Licha ya amri zote hizo, mazuio yote hayo, matamko ya mawaziri yaliyotawaliwa na mbwembwe nyingi, ujenzi uliendelea, nyumba imekamilika. Sasa inatumika. Wakati kigogo huyo amehamia kwenye nyumba yake kwa matangazo na mbwembwe, Mto Ndumbwi, bahari na mazingira kwa ujumla yameharibiwa vibaya! Bila kusahau kuwa  wananchi wengine wamebomolewa nyumba zao kwa kutumia sheria hizo hizo," alisema Bi. Mdee.

Alisema  Serikali inatakiwa kuangalia  hali hiyo kani inaweza kutafsiriwa ni kuitia serikali mfukoni hasa katika mwendelezo wa tafsiri wanayoipata wananchi kuwa imetekwa na kuwekwa mfukoni na watu wachache wenye uwezo.

Alisema ni dhahiri kuwa kuna watu ambao wako juu ya sheria za nchi, huku wanyonge wakishughulikiwa.

Chanzo: Majira

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa