na Betty Kangonga
MMILIKI wa
Hoteli ya Coral ya jijini Dar es Salaam ametakiwa kulipa fidia ya sh milioni 10
kwa kuharibu mazingira ya viumbe wa baharini, huku akipewa siku 7 kuondoa
kifusi cha mchanga kilichojazwa katika eneo la ufukwe wa bahari ya Hindi.
Akizungumza
wakati alipotembelea eneo hilo, Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Mazingira
(NEMC), Manchare Suguta, alisema kuwa mmiliki huyo amekiuka utaratibu na kuamua
kufanya ukaushaji wa bahari kinyume na sheria.
Suguta alisema
kuwa kibali kilichotolewa na NEMC kwa mmiliki huyo ni kwa ajili ya kujenga
ukuta wa matundu wa mita moja na upana mita moja, lakini badala yake akaamua
kuongeza kifusi sehemu asiyotakiwa hatua inayoashiria kuvunja makubaliano ya
awali.
Alisema kuwa
hatua iliyofanywa na mmiliki huyo ni kosa kwa kuwa NEMC haijawahi kutoa kibali
kingine cha kujaza kifusi katika ufukwe huo, hivyo alimtaka kufika katika ofisi
za NEMC ili kulipa faini hiyo.
Suguta alisema
kuwa kutokana na hilo akamtaka mkandarasi mshauri wa ujenzi huo kuhakikisha
anafuata maelekezo na kusimamia kwa dhati sheria za ujenzi katika fukwe za
bahari.
Mkandarasi
anayesimamia ujenzi wa ukuta huo, Donald Mpenihaka, alisema kutokana na maelezo
ya NEMC mmiliki huyo atakuwa amefanya kosa.
Awali
Mkurugenzi wa Coral Hotel, Kelvin Patel, alibishana na mwanasheria wa NEMC hadi
pale mkandarasi alipoamua kuingilia kati na kumtaka kukubali kosa hilo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment