Home » » IMF: PATO LA TAIFA KUFIKIA ASILIMIA 7

IMF: PATO LA TAIFA KUFIKIA ASILIMIA 7

na Eliwaza Emmanuel na Eveline Mosi
IMEELEZWA kuwa uchumi wa nchi umeanza kuimarika kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi zinazondelea ambapo pato la taifa kwa mwaka huu linatarajiwa kukua kutoka asilimia 6.5 na kufikia 7.
Akizungumza wakati wa tathimini iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Paolo Mauro, alisema mfumko wa bei umekuwa ukipungua taratibu kutoka katika kiwango cha juu kilichokuwa kimefikiwa mwaka 2011.
Alisema kuwa nakisi ya bajeti kwa mwaka 2011/12 ya asilimia 5 ya pato la taifa ilikuwa chini ya kiwango kilichokubaliwa.
Mauro alisema kuwa makusanyo ya mapato yalikuwa mazuri na matumizi ya serikali yaliweza kudhibitiwa ingawa si madeni yote yaliyotokana na matumizi ya fedha ambayo yamelipwa.
Hata hivyo, alisema mfumko wa bei wa asilimia 15 ambao ulihusisha bei za vyakula na asilimia 9 kwa nishati katika kipindi cha Agosti mwaka huu bado upo juu ya viwango vinavyotakiwa.
“Urari wa biashara ya bidhaa, huduma, mapato ya uchumi na uhamisho wa mali nje ya nchi unakisiwa kuwa asilimia 16 ya pato la taifa,” alisema.
Alisema kuwa changamoto iliyopo katika suala la umeme ni deni la Shirika la Umeme nchini (TANESCO) ambalo limeendelea kukua kutokana na mpango wa dharura wa kuimarika upatikanaji wa mishati hiyo kwa mwaka 2011.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa