Home » » SALAAM ZA MAASKOFU WA KKKT KWA WATANZANIA WOTE KUHUSIANA NA MATUKIO YA KUCHOMA MOTO MAKANISA YA KIKRISTO ENEO LA MBAGALA – DSM.

SALAAM ZA MAASKOFU WA KKKT KWA WATANZANIA WOTE KUHUSIANA NA MATUKIO YA KUCHOMA MOTO MAKANISA YA KIKRISTO ENEO LA MBAGALA – DSM.


SALAAM ZA MAASKOFU WA KKKT KWA WATANZANIA WOTE KUHUSIANA NA MATUKIO YA KUCHOMA MOTO MAKANISA YA KIKRISTO ENEO LA MBAGALA – DSM.

             Wapendwa Katika Bwana,
Waumini wa KKKT, Wakristo Wote na Watanzania kwa Ujumla.

Neema na Iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba na Bwana wetu Yesu Kristo, Amina.

Sisi
maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), tumepokea
kwa mshtuko mkubwa taarifa za matukio ya uchomaji wa makanisa katika
eneo hili la Mbagala. Tumekuwa katika mkutano wetu wa Mwaka wa Lutheran
Mission Cooperation (LMC) huko Moshi pamoja na vyama vyote vya
Kimissioni vya Ulaya na Marekani. Tumelazimika kukatisha mkutano huo ili
kufika hapa Mbagala. Tumekuja kwa madhumuni makubwa matatu:
  1. Tumekuja
    kuwapa pole na kusimama pamoja nanyi katika uchungu mkubwa mlio nao.
    Machozi yenu ni machozi yetu. Machozi yetu ni machozi ya Kristo mwenyewe
    aliye Bwana wa kanisa linaloteswa. Jipeni moyo kwa kuwa yeye aliushinda
    ulimwengu (Yohana 16:33).
  2. Tumekuja
    kuonyesha majonzi yetu makubwa kwa vitendo vya uvunjifu wa amani,
    kuporomoka kwa umoja na mshikamano wa watanzania. Huu ni msiba mkubwa,
    na wenye msiba ni watanzania wote, wenye dini na wasio na dini.
  3. Tumekuja kushiriki pamoja nanyi kupokea matumaini ya Tanzania mpya. Katika
    majivu haya yaliyotokana na kuchomwa kwa madhabahu ya Mbagala, Tanzania
    mpya itazaliwa. Majivu haya na machozi yenu ni rutuba ya Tanzania mpya
    itakayojali upendo, uvumilivu, ustahimilivu, umoja, mshikamano, uhuru wa
    kuabudu na dola isiyo na dini.

Katika ujio huu wa maaskofu hapa Mbagala, hatukuja hapa kufanya haya yafuatayo:
  1. Hatukuja
    kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaokashifu dini za wenzao, wawe
    na ruhusa kutoka mamlaka zilizo juu au kama wanajituma wenyewe.
  2. Hatukuja
    kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaodhalilisha misahafu ya dini;
    wawe wametumwa, kutegeshewa na mamlaka zozote au kwa misukumo ya utashi
    wao binafsi ili kupata kisingizo cha kugombanisha madhehebu ya dini.
  3. Hatukuja
    kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaochoma makanisa na kuiba mali
    za makanisa kwa kisingizio cha kumtetea Mungu. Kisasi cha dhambi hiyo
    tunamwachia Mungu mwenyewe aliyedhihakiwa na walionajisi madhabahu yake.

Wapendwa
wana KKKT na watukuka sana, wana na mabinti wa Tanzania ya Julius
Kambarage Nyerere; kilichotokea Mbagala katika wiki ya kuadhimisha siku
ya Baba wa Taifa, ni kebehi si kwa Baba wa Taifa bali ni kebehi kwetu
sisi wenyewe tunaokalia kiti alichokalia Baba wa Taifa. Yeye amelala
baada ya kazi njema. Apumzike kwa amani na tunu zake zifufuke katika
majivu haya yaliyotokana na kuchomwa kwa amani na mshikamano wa Tanzania
aliyoijenga.

Kilichotokea Mbagala ni mateso ya kimbari, yaani
mateso ya Kanisa (Persecution). Mateso haya ni matokeo ya mbegu ya
magugu iliyopandwa katika bustani njema na sasa magugu hayo yanazaa
matunda machungu. Dalili za mateso ya kimbari kama ilivyo kwa mateso ya
kanisa; zilianza kitambo na hazikushughulikiwa na waliomrithi Baba wa
Taifa. Dalili hizo ni kama hizi zifuatazo: 
  • Uchochezi
    wa wazi kuwa taifa hili linaendeshwa na unaoitwa “mfumo Kristo”, na
    kuwa Baba wa Taifa alaaniwe kwa yote aliyolitendea taifa hili.
  • Ubishi
    usio na tija juu ya idadi ya waumini wa dini mbalimbali hapa nchini na
    hata kudiriki kushawishi na kugomea zoezi la sensa ya watanzania. Lengo
    la ubishi huu ni mbegu inayoweza kuratibisha na kurasmisha mateso ya
    kimbari na mateso ya kanisa.
  • Matumizi mabaya ya baadhi
    vyombo vya habari, vyenye lengo la kujenga hofu ya kudumu na migawanyiko
    ya kidini miongoni mwa watanzania
  • Ukimya wa vyombo vya
    dola juu ya vitendo vya uvunjaji wa sheria ya matumizi ya vyombo vya
    habari. Kwa vyovyote vile, uvumilivu wa dola hauna maslahi mapana kwa
    mustakabali wa taifa letu na ni mateso ya kimbari, mateso kwa kanisa, na
    kwa wantanzania wote; wawe wengi dhidi ya wachache au wachache dhidi ya
    wengi.
  • Madai yasiyo ya kawaida na ya mara kwa mara kwa serikali inayodaiwa kutokuwa na dini. Madai hayo ni kama:

  1. Kulazimisha
    uvaaji wa alama za kidini katika taasisi za umma ili kurahisisha na
    kuratibisha tofauti za watanzania. Tunajiuliza: Likitokea la Mbagala
    katika mashule yetu na vyuo vya umma, watachomwa wangapi na kuuawa
    wangapi?
  2. Madai yanayojirudiarudia kutaka balozi za nchi
    fulani kufungwa hapa nchini. Madai haya yanaashiria kutaka balozi za
    nchi fulani tu ndiyo ziwe hapa nchini.
  3. Madai na mashinikizo ya Uanzishwaji wa mahakama za kidini hapa nchini
  4. Mashinikizo ya kidini yanayoingilia mifumo ya kitaaluma na kisheria.
  5. Mashinikizo ya kidini juu ya mfumo wa uteuzi wa watendaji wa serikali na katika ofisi za umma,
  6. Kuhoji
    na kupotosha juu ya ushirikiano wa serikali na mashirika ya dini katika
    utoaji wa huduma za kijamii hususan afya na elimu hapa nchini

Wapendwa
wana KKKT na Wapendwa watanzania wote. Hata kama wanaofanya mambo haya
ya kusikitisha wametunukiwa hadhi ya kuitwa kuwa ni “wana harakati”,
tofauti na wanaharakati wanaotambuliwa na watanzania walio wengi,
tunawiwa kuonya kwa uvumilivu wote kuwa uana harakati wao usitumike
kuvunja nchi na sheria za nchi. Tanzania yenye amani na mshikamano ni
tunda la dini zote, makabila yote, itikadi zote za vyama, rangi zote na
hali zote za kiuchumi. Hata wasio na dini wanachangia amani ya nchi hii.

Kwa
macho na masikio yetu, tumeendelea kushuhudia vitendo vya uchomaji
makanisa huko Zanzibar, Mwanza, Mdaula, Mto wa Mbu, Tunduru, Rufiji,
Kigoma na sasa Mbagala. Wakati wote uvumilivu wa wakristo huenda
umetafsiriwa kuwa ni unyonge na woga. Ikumbukwe kuwa hata wanyonge na
waoga, hufika wakati wakasema “sasa basi” pale wanapodhalilishwa kupita
kiasi. Hatuombei wakristo wafikishwe hapo.

Tumeshuhudia wizara
zetu zikivamiwa mchana kweupe na kushinikiza kuachiwa kwa watuhumiwa wa
uhalifu; tumeshuhudia vituo vya polisi vikichomwa moto; mahakama
zikilazimishwa kufunga shughuli zake, misikiti ikitekwa, uhai wa
viongozi wa dini ukitishiwa hadharani na viongozi wastaafu wakizabwa
vibao hadharani kwa sababu ya zinazoitwa harakati za kidini. Tumefikia
kuhoji, watu hawa wavamie nini ndipo hatua zichukuliwe? Wachome nini
ndipo viongozi wenye dhamana ya kulinda mali na uhai washtuke? Wamwue
nani ndipo iaminike kuwa watu hawa ni tishio kwa usalama wa taifa letu?

Sisi
tulioitwa kwa njia ya nadhiri na viapo vitakatifu, tunawasihi sana
waumini wa dini zetu na watanzania kwa ujumla, wenye wajibu wa kututii
na wasiolazimika kututii, kuzingatia kuwa Mwenyezi Mungu analipenda
taifa hili na watu wake. Kamwe hawezi kuliacha liangamie.

Kwa
Wakristo wote, huu ni wakati wa kuendelea kufunga na kuomba kwa ajili ya
amani ya taifa hili. Mkristo wa kweli ni yule aliye tayari kuteswa kwa
ajili ya Kristo na kanisa. Wakristo hatuko tayari kuua, kutesa, kulipiza
kisasi ili kumtetea Kristo. Mungu wetu hatetewi kwa kuua wengine na
kuchoma madhabahu ya dini nyingine.

Katika mateso haya, kanisa
litaimarika zaidi; na katika majivu haya ya Mbagala, Tanzania mpya
itazaliwa na ukombozi wa kweli utapatikana. Tunawataka wakiristo wote
kusamehe na kuendelea kuwa raia wema. Kushiriki kikamilifu katika kuleta
mabadiliko ya kweli kwa kupitia njia sahihi zilizowekwa. Wakati wengine
wanaweka mikakati ya kuchoma madhabahu, wakiristo tuweke mikakati ya
kuomba na kushiriki vema katika haki zetu za uraia. Pamoja na kuwa
wapole kama njiwa, imetupasa pia kuwa na busara kama nyoka (Mathayo 10:16).

Daima tukumbuke kuwa, “KUSHINDANA
KWETU SISI SI JUU YA DAMU NA NYAMA BALI NI JUU YA FALME NA MAMLAKA, JUU
YA WAKUU WA GIZA HILI, JUU YA MAJESHI YA PEPO WABAYA KATIKA ULIMWENGU
WA ROHO” (Waefeso 6: 12).


Ni sisi Maaskofu wenu kwa Neema ya Mungu,
  1. Askofu Dr. Alex G. Malasusa – Mkuu, KKKT na D/Mashariki na Pwani
  2. Askofu Dr. Stephen Munga –Mkuu, D/Kaskazini Mashariki
  3. Askofu Dr. Martin Shao – Mkuu, D/Kaskazini
  4. Askofu Dr. Thomas Laizer – Mkuu- D/Kaskazini Kati
  5. Askofu Dr. Benson Bagonza- Mkuu, D/Karagwe
  6. Askofu Isaya J. Mengele – Mkuu, D/Kusini
  7. Askofu Levis Sanga – Mkuu- D/Kusini Kati
  8. Askofu Elisa Buberwa – Mkuu –D/Kaskazini Magharibi
  9. Askofu Andrew Gulle – Mkuu, D/Mashariki ya Ziwa Victoria
  10. Askofu Michael Adam –Mkuu, D/Mkoani Mara
  11. Askofu Renard Mtenji – Mkuu, D/Ulanga-Kilombero
  12. Askofu Dr. Israel-Peter Mwakyolile – Mkuu, D/Konde
  13. Askofu Job Mbwilo – Mkuu, D/Kusini Magharibi
  14. Askofu Dr. Owdenburg Mdegella- Mkuu, D/Iringa
  15. Askofu Jacob Ole Mameo- Mkuu, D/Morogoro
  16. Askofu Zebedayo Daudi – Mkuu, D/Mbulu
  17. Askofu Paulo Akyoo – Mkuu, D/Meru
  18. Askofu Charles Mjema – Mkuu, D/Pare
  19. Askofu Mteule Amon Kinyunyu- Mkuu, D/Dodoma
  20. Askofu Mteule Dr. Alex Mkumbo- Mkuu, D/Kati

Mbagala, Dar es Salaam,
Oktoba 18, 2012

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa