Wanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM), wanaomuunga mkono Mwenyekiti mpya wa Taifa wa Umoja huo, Khamis Sadifa Juma na viongozi wenzake, wakimtwanga mmoja wa wanachama waliojitokeza kumpinga mwenyekiti huyo kwa mabango(wa pili kushoto), wakati alipowasili makao makuu ya umoja huo Dar es Salaam jana, akitokea mkoani Dodoma alipochaguliwa kushika nyadhifa hiyo. Picha na Rafael Lubava
SHAMRASHAMRA za kumpokea Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) , Khamis Sadifa Juma jijini Dar es Salaam jana ziligeuka uwanja wa vita baada ya makundi yanayopingana kuchapana makonde.
Tafrani hiyo ilianza baada ya kundi moja la vijana waliokuwa wanane kutokea likiwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kupinga ushindi wa mwenyekiti huyo, wakati utambulisho wa ugeni huo ukiendelea katika ofisi za makao makuu ya UVCCM, zilizopo jijini Dar es Salaam.
Baada ya kundi hilo kujitokeza na mabango yao, ndipo vijana wa upande wa Mwenyekiti (Juma), walipoanza kuwakimbiza na kufanikiwa kuwakamata baadhi yao.
Kukiwa hakuna msaada wa Polisi, vijana hao walilishambulia kundi hilo kwa muda, huku baadhi yao wakitiwa nguvuni na vijana hao na kuingizwa katika ofisi ya UVCCM huku waandishi wa habari wakizuiwa kuwahoji watuhumiwa wala kuingia ndani ya ofisi hiyo.
‘’Hatutaki waandishi humu ndani, tokeni na asiingie mtu, hawa tutashughulika nao wenyewe, wanatusumbua mno hawa kwa siku nyingi,” alisikika mmoja wa vijana hao akiongea kwa sauti ya juu.
Baada ya purukushani hizo zilizodumu kwa zaidi ya nusu saa, hali ya hewa ilitulia na ratiba iliendelea huku vijana wengine wanaomuunga mkono mwenyekiti wao wakichukua jukumu la kulinda usalama wa eneo hilo na kuwapeleka Kituo cha Polisi Mnazi Mmoja vijana wawili waliowakamata kwa mahojiano.
Mwenyekiti mpya wa UVCCM alitamba kuwa atapambana na watu wanaotaka kuvuruga umoja huo.
Alisema: “Mimi ni mwanajeshi nimekaa kwenye kambi nyingi za jeshi, hivyo naelewa nitakavyopambana nao.”
Viongozi wa Kitaifa
Hata hivyo, sherehe hizo hazikuhudhuriwa na kiongozi yeyote wa kitaifa wa CCM.
Akizungumza baada ya mapokezi hayo, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa aliwataka vijana kuwa na umoja akisema kuwa uchaguzi umekwisha na kilichobaki ni kujenga chama na kuhakikisha CCM inashinda katika chaguzi zote.
‘’Kilichobaki sasa ni kujenga chama, haipendezi kuendeleza uhasama ndani ya chama, sisi sote ni wamoja na tuache makundi kwani nayachukia na kuwachukia wale wanaoanzisha na kuendeleza makundi,’’ alisema Khamis Sadifa Juma.
Wiki iliyopita, baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa UVCCM mjini Dodoma, kundi la vijana kutoka mikoa mbalimbali walikutana na waandishi wa habari na kulalamika kwamba rushwa ilitawala uchaguzi huo, huku wakiwatuhumu viongozi wa UVCCM na baadhi ya makada wa chama hicho kwa kuhusika na vitendo hivyo.
Waliotajwa ni pamoja aliyekuwa makamu mwenyekiti wa umoja huo, Beno Malisa, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, Bashe na mtoto wa Lowassa, Fredy.
“Kama Rais Jakaya Kikwete kweli yuko makini na kauli zake ni za dhati, basi atengue matokeo ya uchaguzi huu maana kanuni zimekiukwa na kusema kweli rushwa ilitawala. Atumie nafasi yake kurejesha hadhi ya chama kwani huu uchaguzi ni batili,” alisema Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka Morogoro, Augustine Matefu.
Walidai kuwa Bashe, ndiye aliyekuwa mratibu wa uingizaji wa fedha katika eneo la mkutano ambazo zilitumika kugawanywa kwa wajumbe na kwamba Malisa na Shigela waligawa Sh1 milioni kwa viongozi wa mikoa kama hatua ya kumpigia kampeni mmoja wa wagombea walioshinda.
Hata hivyo, Bashe alikanusha tuhuma hizo akisema siyo kweli na kuongeza: “Mimi sijatumwa na Lowassa, wala sifanyi kazi na Lowassa. Nafanya kazi ya CCM, lakini nampenda sana Lowassa kwa sababu ni mmoja wa viongozi na makada wa chama, ambao wameonyesha mapenzi ya dhati kwa CCM na uvumilivu wa hali ya juu.”
Kada mwingine, Livamba Adinan Selemani alisema: “Vijana kweli tumempuuza Rais, kweli mtu ambaye hana hela hawezi kupata uongozi UVCCM, kwa maana nyingine nchi yetu inakwenda pabaya. Watu wachache wenye fedha wanaweza kuamua kufanya wanachotaka, hivyo ndivyo uchaguzi wetu wa vijana ulivyokuwa.”
Mjumbe mwingine, Kichanta Selemani alisema malalamiko ya viongozi wa UVCCM kuwapendelea baadhi ya wagombea yalifikishwa kwa Lukuvi lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
Wakati makada hao wa CCM wakizungumza na waandishi wa habari, lilitokea kundi jingine la makada wa chama hicho ambao walianza kuzozana na wenzao wakisema kuwa malalamiko yao yanatokana na kushindwa na kwamba walitaka kutumia “Viongozi wa ngazi za juu za CCM” kuwachagulia vijana viongozi.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment