Home » » Alichofanya Rage chaishinda Yanga

Alichofanya Rage chaishinda Yanga




Ujasiri aliouonyesha Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage katika kupigania rasilimali za klabu yake mara tu alipoingia madarakani unaelekea kuwashinda vibaya viongozi wa sasa wa mahasimu wao wa jadi, Yanga.

Rage aliingia madarakani kwa ‘gia’ kubwa, akiwabana wapangaji wote wa jengo la klabu yao kwenye Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam na sasa mambo yanawaendea vyema kwani hatimaye ‘Wanamsimbazi’ wamekuwa wakipata malipo stahili ya Sh. Milioni 1.5 kwa kila ‘fremu’ kwa mwezi kwenye maduka yao zaidi ya 10, tofauti na awali ambapo fedha nyingi zilikuwa zikienda  kusikojulikana huku timu hiyo ikiambulia Sh. 200,000 tu kwa kila fremu moja kwa mwezi.



Hata hivyo, ujasiri huo unaelekea kuwashinda viongozi wa sasa wa Yanga waliongia madarakani kwa kishindo baada ya kukiri wazi jana kwamba hawajui jengo lao la Mtaa wa Mafia, lililopo katika eneo zuri pia la kibiashara lililopo Kariakoo jijini Dar es Salaam linaingiza kiasi gani cha fedha kwa mwezi;  na kwamba ni nani anayepokea malipo hayo kutoka kwa wafanyabiashara wanaoendelea na shughuli zao kwenye jengo hilo.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, ndiye aliyefichua taarifa hizo za kushangaza wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya klabu hiyo iliyopo katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam.

Sanga alisema kuwa uongozi wao haujui fedha zitokanazo na malipo kutoka kwa wapangaji waliopo kwenye jengo hilo zinakwenda wapi na tena, ni kiasi gani. Makamu huyo hakutoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na hatua zinazochukuliwa na uongozi kuhakikisha kuwa wanatekeleza vyema wajibu wao kwa kupigania na kuzilinda raslimali za Yanga ili zisiishishie kutunisha mifuko ya watu binafsi.

DENI MILIONI 135


Hata hivyo, licha ya uongozi huo wa Yanga kukiri kwamba haujui zinakokwenda fedha za kodi ya pango katika jengo lao la Mtaa wa Mafia ambalo ni chanzo kizuri cha mapato, uongozi huo umedai kuwa klabu yao sasa inadaiwa Sh. milioni 135 na taasisi na wadau mbalimbali waliofanya nao kazi.

Sanga alieleza kuwa uongozi wao uanasikitika kuona kwamba ada ya wanachama inayokusanywa kubaki kuwa ndogo, kiasi cha Sh. milioni 2.5 tu wakati ikifahamika wazi kuwa hicho ndiyo chanzo kimojawapo cha mapato wanayotegemea kuendeshea klabu.

Akasema kuwa wamepokea Sh. milioni 601 kutoka kwa wafadhili mbalimbali wanaoipenda timu hiyo.

Makamu mwenyekiti huyo alisema kwamba ripoti ya fedha ya mapato na matumizi ya klabu yao ni ya kuanzia Julai 15 hadi Oktoba 15 mwaka huu, kipindi ambacho uongozi wao ulianza kazi baada ya kuingia madarakani.

Sanga alisema kuwa kwa muda waliokaa madarakani, klabu yao imetumia Sh. milioni 598.6 huku akieleza kwamba kiasi kikubwa kilitumika wakati wa kusajili wachezaji walio nao.

"Huko mbele tunataka kupunguza gharama kwa kuweka mikakati ya kuandaa timu za vijana ambazo ndiyo tutazitumia kupandisha wachezaji na kumaliza tatizo hili kwa kiwango kikubwa," alisema Sanga.

Alisema viloevile kuwa kwa mwezi, Yanga hutumia zaidi ya Sh. milioni 65 kulipa mishahara ya wachezaji, benchi la ufundi na sekretarieti ambayo iko chini ya Katibu Mkuu, Lawrence Mwalusako.

"Uwiano uliopo ni mdogo. Kwa mwezi, wastani tunapata Sh. milioni 10, lakini matumizi yetu ni Sh. milioni 65… sasa bila ya kutegemea wafadhili hatuwezi kuongoza," alisema kiongozi huyo.

Alivitaja baadhi ya vyanzo vya mapato vya klabu hiyo kuwa ni fedha za viingilio vya mlangoni ambazo bado makato yamekuwa yakiwaumiza na kusema kwamba wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), katika kipindi cha miezi mitatu, wamewapa Sh. milioni 80 huku Sh. milioni 190 zikitokana na mapato ya mechi 11 za Ligi ya Bara walizocheza.

"Sitaitaja Vodacom kwa sababu haiko kwenye kipindi hiki tulichokifanyia hesabu, pia mapato ya mechi za Azam na Coastal Union hayajajumuishwa," aliongeza Sanga.

Aliweka wazi kwamba katika kipindi hicho cha miezi mitatu walichokaa madarakani, klabu yao haijapata fedha yoyote kutokana na mechi zao kuonyeshwa kwenye vituo vya televisheni na vile vile bado wanaofaidika na uuzaji wa bidhaa zenye nembo ya klabu hiyo ni watu binafsi na siyo klabu yao.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa