Home » » Wafanyakazi Tazara wazuia treni ya ‘Mwakyembe’ kusafirisha abiria Dar

Wafanyakazi Tazara wazuia treni ya ‘Mwakyembe’ kusafirisha abiria Dar



Wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) wameizuia treni ya abiria, maarufu treni ya “Mwakyembe” inayotoa huduma ya kusafirisha abiria jijini Dar es Salaam kuendelea kutoa huduma hiyo wakishinikiza walipwe malimbikizo ya mishahara yao.


Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu), Yusufu Mandai, aliliambia NIPASHE jana kuwa treni hiyo imezuiwa Stesheni ya Tazara, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 8:00 mchana.



Treni hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, inafanya safari zake kati ya Stesheni ya Tazara na Mwakanga, jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo imechukuliwa na wafanyakazi hao siku moja tangu walipotangaza mgomo wao wa kutoendelea na kazi kutokana na menejimenti kushindwa kuwalipa mishahara yao ya miezi miwili.

Mandai alisema sababu nyingine ni mkurugemzi wa wizara hiyo kutohudhuria katika kikao chao na kusema: “Afadhali hata angekuja na kusema chochote wangekuwa tayari kumsikiliza.”

NIPASHE ilifika katika Stesheni ya Tazara na kukuta shuguli zote za stesheni hiyo zikiwa zimesimama.

Baadhi ya wafanyakazi hao walisema hakuna shughuli yoyote itakayoendelea hadi hapo watakapolipwa mishahara yao.

Wakati huo huo, zaidi ya abiria 200 wamekwama katika Stesheni ya Tazara jijini Mbeya, kufuatia mgomo wa wafanyakazi wa mamlaka hiyo uliosababisha treni ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Kaprimposhi nchini Zambia kushindwa kufanya safari zake jana.

Wafanyakazi wa Tazara Tawi la Mbeya walianza mgomo wao jana saa 5:00 asubuhi baada ya kusikia kwamba, uongozi wa Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam umegoma kuzungumza na viongozi wa Trawu.

NIPASHE ilishuhudia wafanyakazi waliogoma wakikusanyika katika ukumbi wa mapumziko ya abiria na kuwatoa nje abiria waliokuwa wakisubiri usafiri kisha kuanza mkutano wao uliokuwa chini ya Mwenyekiti wa Trawu tawi la Tazara, Christopher Kaziyo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Kaziyo alisema wameamua kuungana na wafanyakazi wenzao nchini kwa lengo la kushinikiza uongozi wa Tazara kuwalipa wafanyakazi mishahara yao ya miezi miwili ambayo bado hawajalipwa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa