Na Asifiwe George, Dar es Salaam
MKAZI wa Dar es Salaam, Saidi Mohamed, amejikuta matatani baada ya kudaiwa kufanya utapeli na kujipatia Sh 2,870,000 kutoka kwa watu watatu tofauti. Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Katibu Mwenezi wa Chama cha Wapangaji Tanzania (TTA), Simoni Kwezi, alisema mtu huyo alifikishwa katika ofisi zao zilizopo Magomeni Novemba 12, mwaka huu na watu watatu ambao wote walihitaji kupanga katika nyumba ya Mohamed.
Alisema kwa mujibu wa maelezo ya watu hao, walikuwa wakihitaji chumba kwa ajili ya makazi na kufanikiwa katika nyumba ya Mohamed, ambaye ni mtuhumiwa na alipokea fedha zao kwa nyakati tofauti kwa lengo la kuwapangisha chumba na kuingia nao mkataba.
Alisema kitendo hicho si cha kiungwana, kwa kuwa ni jambo la kushangaza kwa mtu kupokea kodi kwa wapangaji watatu tofauti kwa chumba kimoja.
Aliwataja walalamikaji hao kuwa ni Michael Melkiory ambaye alitoa Sh 1,320,000, Alawiy Mohamed alitoa Sh 950,000 na Manhe Jonathani 600,000 na wote waliahidiwa kupata chumba hicho.
“Hali hiyo ilijitokeza siku ambayo mmoja wao alihamia katika chumba hicho, ndipo walipobaini kuwa Mohamed amewatapeli.
“Walivyomtafuta katika simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani na ndipo waliamua kwenda kwa Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa na kisha kuelekezwa katika ofisi hizo kwa ajili ya kupata suluhisho la tatizo lao,” alisema Kwezi.
Alisema walalamikaji hao wana haki ya kulalamika kwa kuwa walipata usumbufu mkubwa.
Mtuhumiwa alikubali kosa na kuahidi kuwa angewalipa wapangaji wawili na alimpendekeza kumpangisha mpangaji mmoja aliyekuwa na familia.
Hata hivyo, wapangaji wote watatu waligoma na kumtaka mtuhumiwa huyo kuwalipa fedha zao wote kwa pamoja na kwa wakati na mtuhumiwa alipelekwa kituo cha polisi Magomeni kwa upelelezi zaidi.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment