Na Gabriel Mushi, Dar es Salaam
WAKAZI wa Mikoa ya Kilimanjaro na Mwanza,
wanatarajia kufaidi zaidi usafiri wa anga baada ya Shirika la Ndege la Fastjet
kuzindua huduma zake nchini kwa gharama nafuu ya Sh 32,000 kutoka Dar es Salaam
kwenda katika mikoa hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi
wa mauzo ya tiketi za safari hizo, Ofisa Mkuu wa Masoko wa shirika hilo,
Richard Bodin, alisema wakazi wa mikoa mingine watapata huduma hiyo kila
itakapowezekana.
Alisema kwamba, shirika hilo limekuja kuwekeza kwa mara ya kwanza katika Bara
la Afrika na kuchagua Jiji la Dar es Salaam ili kukuza masoko na kurahisisha
usafiri kwa wakazi wake.
“Uzinduzi huo wa tiketi ni hatua muhimu katika juhudi za kampuni kuwezesha
usafiri wa ndege kwa Watanzania kwa sababu wapo wengi ambao awali walikuwa
hawamudu gharama za safari za ndege.
“Kwa usafiri wa anga kutoka Dar es Salaam kuelekea Kilimanjaro na Mwanza
zitakuwa ni Dola 20 za Marekani sawa na Sh 32,000 kwa wasafiri watakaowahi kwa
sababu iwapo wakichelewa baada ya kodi zitapanda hadi kufikia Dola za Marekani
70 hadi 75.
“Fastjet ambayo imeinunua Kampuni ya 540, imechagua Mkoa wa Dar es Salaam kuwa
kituo chake cha kwanza cha uendeshaji barani Afrika ambapo safari za ndege
zitaanza kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuanzia
Novemba 29 mwaka huu.
“Tiketi za Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro na Mwanza zimeanza kuuzwa leo
(jana), safari nyingine za ndani na Kanda ya Mashariki mwa Afrika zitaanza
baada ya wiki kadhaa.
“Kwa ujumla, hiki ni kipindi cha kihistoria kwa safari za anga Tanzania na hasa
Bara la Afrika kwa sababu tumedharimia kuhakikisha usafiri wa anga kwa upande
wa bara hili unakuwa ni kitu ambacho kila mtu anaweza kukimudu tofauti na
awali,” alisema Bodin.
Kutokana na ujio wa safari hizo, alisema shirika hilo linatarajia kuajiri zaidi
ya watumishi 600 ili kukabiliana na tatizo la ajira nchini.
“Lakini pia tumejipanga kukabiliana na soko kwa sababu aina hii ya usafiri wa
gharama nafuu tumeuanzia katika nchi za Bara la Ulaya na mpaka sasa unaendelea
hivyo tuna uzoefu nao.
“Katika kuhakikisha tunaingia kwenye soko kwa nguvu zote, tunatarajia kuleta
ndege tatu aina ya A319 zitakazoanza kutoa huduma mara mbili kwa siku kwa kila
mkoa na zitakuwa zikitoa huduma za ubora wa kimataifa,” alisema.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment