na Edson Kamukara
UKOSEFU
wa umakini serikalini, umeendelea kuliingiza taifa kwenye gharama zisizo za
msingi ambapo sasa mahakimu wakazi 370 wanalazimika kulipwa mishahara bila
kufanya kazi, Tanzania Daima limebaini.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa mahakimu wakazi 300 waliajiriwa Juni
mwaka huu katika ajira mpya kwa masharti kwamba wangefanya kazi kwenye mahakama
za mwanzo.
Baadaye
Septemba mwaka huu, mahakimu wengine 70 waliapishwa na kupandishwa kutoka
mahakama ya mwanzo kuwa mahakimu wakazi na hivyo kufanya idadi yao kufika 370
ambao hulipwa takribani sh 700,000 kila mmoja kwa mwezi.
Hata
hivyo, katika kile kinachoonekana kama kukosekana kwa umakini katika utendaji
serikalini, sheria iliyopo sasa kuhusu utendaji wa mahakimu hao ilipaswa
kufanyiwa marekebisho kwanza kabla ya wao kuajiriwa.
Kwa
mujibu wa sheria ya sasa ya mahakimu na mahakama sura namba 11 kifungu cha
sita, ni kwamba hakimu mkazi hana mamlaka ya kukaa katika mahakama ya mwanzo
bali mahakama ya wilaya na ya hakimu mkazi (mkoa).
Wakizungumza
na gazeti hili, baadhi ya mahakimu hao waliilalamikia serikali kwa kukurupuka
kuwapa ajira bila kufanyia marekebisho sheria, na hivyo kuhoji ni kwanini
wasipangiwe kazi kwenye mahakama zenye hadhi yao hadi sheria itakapokuwa
imebadilishwa.
“Kwa
kweli kitendo hiki cha kulipwa mshahara pasipo kufanya kazi ni kama kuhujumu
uchumi wa nchi, lakini pia serikali imeamua kuharibu taaluma zetu,” kilisema
chanzo chetu.
Kwa
sasa mahakimu hao wanaripoti tu kwenye vituo vyao vya kazi na kusaini kitabu
cha mahudhurio kisha kuondoka kwa vile hawana kazi maalumu ya kufanya katika
mahakama hizo.
“Mikoa
kadhaa kama Mwanza na Pwani, majaji wenye uelewa wanawapangia kazi mahakimu
hawa kwenye mahakama stahiki. Lakini bado si maeneo yote wanafanya hivyo.
“Serikali
ni kweli ilikuwa na nia njema ya kuboresha mfumo wa mahakama ili hawa wasomi
wahudumie huko, lakini kwanini wasirekebishe sheria kwanza?” kiliongeza chanzo
hicho.
Waziri
wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe pamoja na Naibu wake, Angela Kairuki
hawakuwa tayari kupokea simu na hata walipoandikiwa ujumbe mfupi wa maneno vile
vile hawakujibu, hivyo juhudi za kuwatafuta ili wafafanue zinaendelea.
CHANZO MTANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment