Home » » CCT yavishukia viwanda vya ARV’s

CCT yavishukia viwanda vya ARV’s



na Happiness Mnale
JUMUIYA ya Kikristo Nchini (CCT), imevijia juu viwanda vya kuzalisha dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi (ARV’s) duniani, na kusema vina siri ya tiba ya ugonjwa huo, lakini vimeamua kukaa kimya.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa semina ya siku mbili ya waandaaji wa vipindi vya redio na runinga vitakavyohusiana na masuala ya kuondoa unyanyapaa, Makamu Mwenyekiti wa CCT, Askofu Valentino Mokiwa, alisema siri hiyo ni ya kushindwa kuzalisha dawa za kutibu kabisa ugonjwa huo, ili waweze kuendelea kufanya biashara kupitia ARV’s.
Alisema ugonjwa huo umetumika kuwanufaisha watu wenye viwanda kwa kuufanya ni mradi.
Aidha, aliwataka watafiti wa Kikristo kuongeza kasi ya kuleta tiba na kuondoa hofu ya ugonjwa huo.
Akizungumzia suala la unyanyapaa; Mokiwa alisema kanisa litahakikisha linaondoa hali hiyo kwani lina wajibu kwa jamii.
Pamoja na hayo, aliitaka serikali kutunga sheria za kumlinda mwathirika kutokana na unyanyapaa, hasa maeneo ya maofisi.
Naye Rogers Steven, ambaye anaishi na virusi vya ukimwi alisema ameishi na ugonjwa huo kwa miaka 15 sasa.
Alisema amekutana na hali ya juu ya unyanyapaa ndani na nje ya familia, na kuwataka Watanzania kuwafariji wagonjwa kwa kuwaonyesha upendo.





Mwanamke aibiwa mtoto
na Efracia Massawe
MKAZI wa Buguruni kwa Mnyamani, jijini Dar es Salaam, Hadija Omari (37), ameibiwa mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili na nusu na mwanamke asiyefahamika.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Hadija, alisema mwanae huyo aitwaye Sabrina Hamisi, aliibwa Novemba 11, mwaka huu.
Hadija, alisema siku hiyo akiwa katika biashara yake ya mama lishe eneo hilo, alifika mteja mwanamke na kuagiza chakula na kumwandalia, kisha kutoka nje.
Alisema aliporudi ndani katika hali ya kushangaza hakumkuta mteja huyo wala mtoto wake.
Mama huyo alisema kuwa, ametoa taarifa Kituo cha Polisi Buguruni na kupewa jalada lenye namba BG/MNY/RB/ 1922/12.
Anamuomba msamaria yeyote atakayefanikiwa kumuona mtoto huyo kuwasiliana naye kwa simu namba 0718203086 na 0654988856 au afike katika ofisi za gazeti hili zilizopo Mtaa wa Mkwepu maeneo ya Posta, Dar es Salaam.

CHANZO MTANZANIA DAIMA 


0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa