Bakari Kiango
SERIKALI imeanisha mikakati mipya itayosaidia kukabiliana na tatizo la uhaba wa
mafuta na kwa kuanzia limetoa mwongozo kwa Shirika la Maendeleo la Petroli
Tanzania(TPDC), kuhakikisha wakati wote linahifadhi mafuta ya akiba.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa hatua hiyo
inakuja ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa mafuta, kama lilivyoshuhudiwa
siku za hivi karibuni na kuwasababishia wananchi usumbufu.
Profesa Muhongo ambaye alikuwa akizungumza kwenye kipindi cha dakika 45
kinachorushwa na Kituo cha ITV, alisema kuanzia sasa TPDC itahakisha iinaweka
akiba ya mafuta kukabili dharura yoyote inayoweza kujitokeza.
“ Kuanzia sasa serikali inaanzisha utaratibu mpya, tunataka kuona shirika letu
hilo linakuwa na mafuta ya akiba wakati wote ile mambo kama yale yakijitokeza
basi linaingilia kati na kusaidia,” alisema Muhongo.
Alieleza kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha inaondokana kabisa na tatizo la
ukosefu wa mafuta na inaendelea kuchunguza mwenendo wa soko, ili kujiwekea
mipango endelevu itayosaidia kukabiliana na tatizo lolote.
Kauli ya Waziri Muhogo imekuja siku chache tu baada ya maeneo mengi kukabiliwa
na uhaba wa nishati ya mafuta aina ya petroli yaliyoadimika kwa muda wa wiki
moja.
Hali ililiripotiwa kuwa mbaya katika mikoa kadhaa ikiwemo Dar es Salaam,
Njombe, Ruvuma na mikoa iliyoko Kanda ya Ziwa na ile ya Kaskazini.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(Ewura), ilisema tatizo
la uhaba wa nishati hiyo ilitokana na kuchelewa kuwasili kwa meli
zilizotegemewa kushusha mafuta.
Hata hivyo mamlaka hiyo imewatoa hofu wananchi ikisema kuwa meli kadhaa tayari
zimeanza kushusha mafuta na baadhi yamepelekwa mikoani hasa ile
iliyokumbwa na uhaba mkubwa.
Kwa upande mwingine Serikali ilitishia kuzifutia leseni kampuni zinazojihusisha
na uuzaji wa bidhaa hiyo kwa madai kuingia njama ya kutosambaza kwa makusudi
nishati hiyo.
Takwimu zinaonyesha kuwa mahitaji ya pertoli nchini kwa siku ni lita
1.7ml, dizeli 3.5ml, mafuta mazito1.1ml na 200,000 na mafuta ya taa ni
400,000.
Kuhusu gesi Muhongo alisema wizara yake imeka utaratibu maalumu kwa wachimbaji
wadogo, ili waweze kunufaika na madini kuliko kulalamika Serikali
haiwajali wachimbaji hao.
Kwa mujibu wa Muhongo wizara itaanzisha vipindi maalumu kuhusu mambo ya gesi
kupitia vyombo vya habari, ili kuwaelimisha wananchi na itakuwa kwa mwaka
mzima.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment