Home » » KUNA UWEZEKANO KUWEPO KWA MVUA KUBWA JANUARI HADI MACHI

KUNA UWEZEKANO KUWEPO KWA MVUA KUBWA JANUARI HADI MACHI



 
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania, TMA, imesema katika kipindi cha Januari hadi machi mwaka huu, kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa vipindi vifupi vya mvua kubwa zinazoambatana na upepo mkali na kuzitaka Mamlaka zinazohusika kuendelea kuchukua tahadhari kuhakikisha usalama wa Wananchi na mali zao.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. AGNES KIJAZI amesema mbali na mvua hizo pia kuna uwezekano wa kuwepo kwa mvua zilizoko nje ya msimu katika mwezi wa Januari, mwaka huu na kwamba zikitumika vizuri zinaweza kusaidia upungufu wa mvua uliojitokeza katika kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka 2012.

Dk KIJAZI ameongeza kuwa pamoja na kuzitaka Mamlaka husika kuchukua tahadhari hizo kuna haja kwa jamii kuzingatia matumizi mazuri ya maji hususani katika maeneo ya mito inayotiririsha maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme ili kuepuka uwezekano wa kuwepo kwa upungufu wa maji katika mabwawa hayo.
Katika hatua nyingine Dk. KIJAZI amesema katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba mwaka jana palijitokeza hali isiyoyakawaida baada ya hali ya joto la bahari iliyotarajiwa katika ukanda wa tropikali ya mashariki mwa bahari ya pasifiki kuendelea kushuka kwa kasi kutoka juu ya wastani hadi wastani, hali ambayo imewalazimu wataalam wa hali ya hewa kuendelea kuchunguza chanzo cha hali hiyo.

Wakati tahadhari hiyo ikitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini wananchi wenye makazi katika maeneo ya mabondeni wameanza kuonja chungu ya mafuriko baada ya maji kujaa kwenye maeneo ya jirani na makazi yao na kuanza kuingia ndani katika baadhi ya maeneo.
Clouds Fm imepita katika maeneo mbalimbali ya jiji likiwemo eneo la Kinondoni Mkwajuni na kukuta maji yakiwa yamezizingira baadhi ya nyumba zilizopo katika eneo hilo huku yakiwa na taka za aina mbalimbali ambazo pia zinaweza kuhatarisha afya za wakazi hao.
Kufuatia hali hiyo baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wamewashauri wakazi wa mabondeni kusikiliza ushauri wa Serikali na kuhama katika maeneo hayo kabla hawajapata madhara huku wenyewe wakijitete kuwa wanaishi kwenye makazi hatarishi kutokana na ugumu wa maisha.

Katika hatua nyingine Clouds Fm imetembelea kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo jijini Dar es Salaam na kukuta hali ya usafiri kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiendelea kama kawaida licha ya kuwepo kwa hitilafu ya kukatika kwa daraja katika mkoa wa Singida.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa