WATUHUMIWA wanne wa shtaka la kula njama na kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine za uzito wa kilogramu 50, jana waliijia juu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kitengo cha kuzuia dawa za kulevya kwa kuchelewesha kwa kipindi cha miaka mitatu kukamilisha upelelezi dhidi yao.
Waliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Tanga, kwamba wanahisi ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na kitengo cha kupambana na dawa za kulevya zimekula njama za makusudi kuchelewesha kukamilisha upelelezi katika kesi yao ili waendelee kusota mahabusu hatimaye wafe.
Watuhumiwa katika kesi hiyo ni Ismail Shebe (38), Rashid Said (40), Majed Al Mand (36) na Assad Aziz (33) ambao waliyatoa malalamiko yao jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Seif Mwishehe Kulita mara baada ya kufikishwa mahakamani hapo na kuelezwa kwamba upelelezi dhidi ya mashataka yao bado haujakamilika.
Mara baada ya kutajwa kesi hiyo,Mawakili wa Serikali wanaoendesha kesi hiyo Saraji Iboru na Martenus Marando waliiomba mahakama hiyo kuiahirisha kesi hiyo kwa kuwa kitengo cha upelelezi cha Tume ya kudhibiti dawa za kulevya kilichopo Dar es Salaam bado hakijakamilisha upelelezi wake.
Wakili wa Serikali Saraji aliieleza mahakama hiyo kwamba ofisi ya Mwansheria wa Serikali inasubiri kitengo cha upelelezi cha dawa za kulevya kulifikisha kwake jalada la kesi hiyo lakini hadi jana lilikuwa halijawasilishwa.
Alisema hadi jana jalada la kesi hiyo lilikuwa halijafikishwa ili ufanyike mchakato wa kuihamishia kesi hiyo Mahakama Kuu kwa kuwa kisheria mahakama ya hakimu mkazi haina mamlaka ya kuisikiliza.
Baada ya kutoa maelezo hayo, mtuhumiwa namba tatu katika kesi hiyo,Majid Al Mand alinyoosha mkono na kuiomba mahakama iingilie kati kushinikiza upelelezi ukamilishwe haraka ili wafikishwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa kwani wamekaa muda mrefu mahabusu tangu mwaka 2010 walipokamatwa.
“Kama mimi nina familia inayonitegemea, kwa akili ya kawaida tu huwezi kutegemea kusikia kwamba upelelezi unachukua miaka mitatu na hadi leo tunapewa sababu hizo hizo ambazo tumekuwa tukipewa tangu tulipofikishwa mahakamani hapa,” alisema Al Mand.
Naye mtuhumiwa namba nne Assad alisema ni vyema ofisi ya Mwansheria Mkuu wa Serikali kama hadi sasa haijapata ushahidi dhidi yake ni vyema imwachie huru kwani anawekwa rumande wakati hana hatia wala hakukamatwa na dawa za kulevya.
Akizungumza baada ya kusikiliza malalamiko ya washtakiwa hao, Hakimu Kulita alisema hata Mahakama yake haipendezwi na kitendo cha kucheleweshwa kwa upelelezi dhidi ya kesi hiyo kwani ingependa ukamilishwe haraka ili ifikishwe Mahakama Kuu na kusisitiza kwamba haiwezekani watuhumiwa kuwekwa rumande miaka mitatu bila kusikilizwa kesi yao.
Akimjibu Hakimu,Wakili wa Serikali Martinus Marando aliahidi kuwasiliana na mamlaka zinazohusika ili kuwasilisha malalamiko haya.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 14 mwaka huu itakapotajwa tena ambapo washitakiwa wote wamerejeshwa rumande.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment