Waziri wa Mambo ya Ndani,Emmanuel Nchimbi
BUNGE
jana lilipitisha Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo
liliidhinisha jumla ya Sh741 bilioni, huku Sh579 bilioni zikiwa kwa
ajili ya matumizi ya kawaida na Sh163 bilioni kwa miradi ya maendeleo.
Hatua hiyo ya Bunge ilifuatia mjadala wa hotuba ya Waziri wa Mambo ya
Ndani na ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Hotuba
hizo mbili zilizua malumbano makali kati ya wabunge wa chama tawala na
wale wa upinzani, huku kila upande ukibeza fikra na mawazo ya upande wa
pili pasipo kuangalia uzito wa hoja hizo. Tunaweza kusema kwamba
malumbano hayo yaliegemea hasa katika itikadi za kisiasa, hivyo
kudhoofisha au kuzima hoja za msingi zilizowasilishwa na baadhi ya
wabunge wa kambi hizo mbili.
Ni
bahati mbaya kwamba wabunge bado wanaendekeza itikadi za vyama badala
ya kujadili hoja kwa uzito wake kwa lengo la kuweka mbele masilahi ya
taifa badala ya matakwa ya vyama wanavyoviwakilisha bungeni.
Hii
ni kansa inayoendelea kulitafuna Bunge letu, kwani wabunge
wanaposhindwa kutenganisha hoja zenye masilahi kwa taifa na zile zenye
masilahi kwa wanasiasa wanakuwa hawawatendei haki wananchi hata kidogo.
Tunazungumzia
suala hili kwa uchungu mkubwa kutokana na unyeti wa Wizara ya Mambo ya
Ndani, ambayo pia inalisimamia Jeshi la Polisi. Kwa sababu jeshi hilo ni
roho ya nchi, tungetegemea wabunge wa kambi hizo mbili kuweka kando
tofauti zao na kuupa mjadala wa hotuba zote mbili z
a Bajeti ya wizara hiyo uzito unaostahili.
Ni
vigumu kuamini kwamba wabunge wengi hawajatambua kuwa, kutokana na
matukio makubwa ya kihalifu yanayoikumba nchi yetu hivi sasa,
tunalihitaji Jeshi la Polisi pengine kuliko wakati mwingine wowote
katika historia ya taifa letu.
Amani
iliyokuwa imetamalaki kiasi cha dunia kuiona nchi yetu kama kisiwa cha
amani sasa inatikiswa na maadui wa ndani wakishirikiana na washirika wao
kutoka nje. Tukio la bomu jijini Arusha mwishoni mwa wiki, ambapo watu
kadhaa walikufa na wengine kujeruhiwa ni kielelezo cha hali hiyo.
Hivyo,
tunalishangaa Bunge kutoona umuhimu wa kutenga fedha za kutosha kwa
ajili ya kuliimarisha jeshi hilo ambalo ni dhaifu. Hali tuliyomo
inatulazimu kuajiri askari wasiopungua 50,000 badala ya 3,000
waliotangazwa katika hotuba ya Waziri juzi. Askari mmoja bado anahudumia
watu 1010 badala ya 450 kwa kiwango kinachokubalika sasa.
Kuendeleza
lawama kwa jeshi hilo hakutatusaidia iwapo haitakuwapo dhamira ya
kuliimarisha na kuhakikisha lina askari wenye weledi, waliopewa elimu na
mafunzo stahiki.
Matumizi
ya FBI kwa matukio ya uhalifu sio mkakati endelevu, badala yake jeshi
hilo lifundishwe kupambana na wahalifu, lipewe vifaa vya kutosha na vya
kisasa. Serikali iwe na dhamira ya kuondoa unyonge kwa askari wetu kwa
kuwapa makazi mazuri, usafiri, bima ya maisha na mishahara stahiki.
Hayo yote yamo ndani ya uwezo wetu, kinachohitajika ni utashi tu wa kisiasa.
Ili
kuhakikisha kwamba jeshi hilo na vyombo vingine vya dola vinakuwa huru
na adilifu, Katiba Mpya itakayoundwa itamke bayana kwamba jeshi hilo na
Idara ya Usalama wa Taifa ni vyombo vya umma, hivyo visifungamane na
upande wowote. Hatua hiyo itavikomboa vyombo hivyo kutoka katika makucha
ya wanasiasa.
MWANANCHI GAZETI
0 comments:
Post a Comment