Home » » DK REGINALD MENGI AZUNGUMZIA UHUSIANO WA RUSHWA KUBWA NA DAWA ZA KULEVYA

DK REGINALD MENGI AZUNGUMZIA UHUSIANO WA RUSHWA KUBWA NA DAWA ZA KULEVYA

MMOJA wa wafanyabiashara maarufu nchini Dk Reginald Mengi amesema kwamba huwezi kutofautisha watoa rushwa wakubwa na mlipuko wa madawa ya kulevya ambayo kwa sasa yanatikisa nchi.
 
Dk mengi alisema hayo wakati akizungumza moja ya vikwazo vikubwa vya uwekezaji nchini katika mazungumzo ya sekta binafsi na umma kwenye uzinduzi wa taarifa inayozungumzia uwekezaji nchini kwa jinsi unavyoonwa na viongozi wa wafanyabiashara.
 
Katika taarifa hiyo iliyofanyiwa utafiti na Sekta Binafsi kwa ufadhili BEST AC, Programu iliyopo ofisi ya Waziri Mkuu, rushwa ni mojawapo ya vikwazo vya uwekezaji nchini.
 
Ripoti hiyo “Mitizamo ya viongozi wa biashara juu ya mazingira ya uwekezaji Tanzania “  ambapo ripoti yake imezinduliwa Julai 11 mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee, changamoto hizo zinatakiwa kufanyiwa kazi mapema na kwa kasi ili kuinusuru nchi.
 
Dk Mengi alisema mfano mzuri wa fedha za rushwa kutumika kuimarisha uingizaji wa mihadarati nchini au kuitoa ni kukamatwa kwa wasichana wawili wakiwa na dawa za kulevya zenye thamani ya shilingi bilioni 6.8.
Alisema mabinti hao hawana uwezo wa kupata fedha za kununulia mzigo wa thamani hiyo na kusema kwamba kazi hiyo inawawezeshwa na watoa rushwa wakubwa nchini ambao wanajulikana.
 
Alisema taifa hili linasumbuliwa na watoa rushwa wanne wakubwa ambao alisema kwamba hatawataja, pamoja na kuulizwa kutakiwa kufanya hivyo na mwenyekiti wa kikao cha mazungumzo.
 
Dk Mengi alisema kwamba mihadarati hiyo ni tatizo kubwa kwa taifa kwa sasa lakini inaweza kuondoka kama hatua za kijasiri za kuwakataa watu hao zitachukuliwa na wala isiwe kuwepo kwa utashi wa kisiasa pekee wakati uwajibikaji haupo.
 
“Taifa likubali kutengana na watoa rushwa wakubwa haraka na mara moja na taifa litaendelea kuishi” alisema Dk Mengi.
 
Dk Mengi alisema yeye ni mmojawapo wa watu wa Tanzania walioumia katika rushwa kwani amepoteza miradi miwili mikubwa kwa sababu hiyo.
 
Hata hivyo alisema kwamba watanzania wenyewe hawapendani na kukaripia matukio ya rushwa kwani hata alipolalamika kuhusu hoteli ya Kilimanjaro, yupo mtu aliyeuliza kwanini Mengi anataka kushika kila kitu.
Dk Mengi ambaye alisema kwa uchungu juu ya tatizo la rushwa na mihadarati alisema kwamba mwishoni anayeumia ni mtu wa kawaida  hasa maskini.
 
“Tukiachia hivi watu hawa watakamata nchi,...taifa litatawaliwa na mtu ambaye humjui,” alisema Dk mengi na kuongeza kuwa watu hao watakuwa na uwezo wa kufanya kila kitu wanachotaka .
 
Alisema Tanzania ikiwa miongoni mwa mataifa 14 yanayosifika kwa rushwa, wananchi wake ni lazima kuamka na kushiriki katika vita hiyo.
 
Naye Mtendaji wa Sekta Binafsi Godfrey Simbeye alisema kwamba wakati umefika wa kuweka sawa uwekezaji na kutilia maanani program ya kitaifa ya maendeleo kwa kushirikisha kikamilifu sekta binafsi.
Aidha aliitaka serikali kurejesha mauzngumzo kati yake na sekta binafsi ambayo mara ya mwisho yalifanyika mwaka 2009.
 
Mazungumzo hayo kwa kawaida mwenyekiti wake ni rais wan chi.
Taarifa hiyo ina mambo matano ambayo yameelezwa kuwa kikwazo cha uwekezaji. Mambo hayo pamoja na rushwa  tatizo la upatikanaji wa umeme wa uhakika, kodi na tozo nyingine, , menejimenti ya kodi na ugumu wa taasisi za fedha kuwezesha wajasirimali.
 
Chanzo: 

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa