Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe jana alihojiwa tena na Jeshi la Polisi, lakini
akaendelea na msimamo wake kwa kugoma kuwasilisha ushahidi wake kuhusu
mlipuko wa bomu uliotokea mkoani Arusha Juni 14, mwaka huu.
Mbowe alifika Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam kuitikia wito wa jeshi
hilo kumtaka awasilishe ushahidi wake aliosema kuwa anao, lakini
aligoma akisema atautoa pale tume ya kijaji itakapoundwa na Rais Jakaya
Kikwete kama alivyoomba.
Kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alitaka kuundwa kwa tume
huru ili kuchunguza mlipuko huo uliotokea alipokuwa akihitimisha hotuba
yake katika mkutano wa mwisho wa kampeni za udiwani kwenye Viwanja vya
Soweto, Arusha.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema jana kuwa
Mbowe alikwenda polisi baada ya kuandikiwa barua ya kumtaka afike
kuwasilisha ushahidi. Alifika lakini aligoma kutoa ushahidi huo.
“Alikwenda tu kuitikia wito wa polisi uliomtaka awasilishe ushahidi,
lakini amegoma kufanya hivyo na amewaeleza polisi kuwa hatafanya hivyo
hadi Rais atakapounda tume ya kijaji kama alivyomwandikia barua,”
alisema na kuongeza: “Anachosubiri sasa ni majibu ya Rais kuhusu barua
yake.”
Mnyika alisema baada ya maelezo hayo, Mbowe alitakiwa kuyaweka
kimaandishi kupitia kwa wakili wake Peter Kibatala na kuyawasilisha
polisi ifikapo kesho.
Akizungumzia suala hilo, Wakili Kibatala alisema: “Mbowe ameachiwa baada
ya majadiliano ya kisheria kati yangu na Kamanda Advocate Nyombi.
Tumekubaliana kujibu kwa maandishi wito wa polisi walioutoa kwake
wakimtaka awasilishe ushahidi wa kuhusika kwa polisi katika mlipuko wa
bomu Arusha na kisha kuyafanyia kazi hayo kisha kutuarifu.”
Msemaji wa Polisi SSP, Advera Senso alipoulizwa kuhusu suala hilo
alisema anafuatilia kujua kama kweli Mbowe alihojiwa na kama kutakuwa na
habari ya kuwajulisha wananchi ataitoa baadaye.
Wiki iliyopita jeshi hilo lilimhoji Mbowe kwa madai kuwa kauli zake
alizozitoa baada ya mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho ni za
uchochezi.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alihojiwa kutokana na madai aliyosema
kwamba polisi ndiyo waliohusika na ulipuaji wa bomu Arusha, pia polisi
kusaidia CCM kwenye uchaguzi na kumtuhumu Rais Jakaya Kikwete kuhusika
na mauaji ya Arusha kutokana na kukaa kwake kimya.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment