Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku tatu wa Baraza la Vijana (TYC) wa
kujadili Rasimu ya Katiba Mpya, Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam. Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta
ametaka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
ichunguze kashfa ya matumizi tata ya Sh8 bilioni zilizotumika wakati wa
Mkutano wa Smart Partnership Dialogue uliohusisha viongozi kadhaa wa
Afrika ambao ulifanyika nchini hivi karibuni.
Akifungua mkutano wa siku tatu wa Baraza la Vijana la Katiba Tanzania
Dar es Salaam jana, Waziri Sitta alidai kwamba fedha hizo zimefujwa na
baadhi ya watumishi wa Serikali ambao walijitengenezea kampuni bandia
ambazo hazijasajiliwa.
“Shilingi bilioni nane zimekwenda kutokana na kampuni hewa baada ya Rais
kuwakaribisha wageni nchini hivi karibuni.... kisa Rais kapata wageni
watu wametengeneza kampuni hewa za mapambo, machapisho na fedha
zimeliwa,” alisema Sitta na kuongeza: “Hivi sasa uchunguzi unaendelea,
lakini hatuwezi kuwa kila siku ni uchunguzi tu na wakati mwingine
uchunguzi umekuwa hauna matokeo.”
Alisema watumishi kama hao hawafai kwa kuwa wanatumia nafasi muhimu kwa nchi kujinufaisha wao binafsi.
Mkutano wa Smart Partnership Dialogue ulifanyika Dar es Salaam kuanzia Juni 28 hadi Julai Mosi mwaka huu.
Alisema walifahamu kuhusu ufisadi huo baada ya Katibu Mkuu Kiongozi,
Ombeni Sefue kueleza kuwa kuna utata kwenye fedha hizo na kwamba kampuni
tatu hewa zililipwa fedha wakati hazijasajiliwa kwa Wakala wa Usajili
wa Biashara na Leseni (Brela).
“Kuna kampuni kama tatu, hizi nasikia zimeshachukuliwa hatua kwa kuwa ni
hewa lakini bado... lazima CAG afanye ukaguzi kwa hizo Sh8 bilioni,”
alisema Sitta.
Sitta ambaye amekuwa akijipambanua kuwa ni mmoja wa kundi la viongozi
wanaopinga ufisadi, alisema watumishi wa jinsi hiyo, hawafai kwa kuwa
wanatumia nafasi muhimu kwa nchi kujinufaisha binafsi.
“Pamoja na yote, kampuni zina watu, lazima na wao wachukuliwe hatua.
Wahusika wote ninaamini wanafahamika sasa isifikie hatua tunaambiwa
uchunguzi usiofikia mwisho,” alisema Sitta.
Hata hivyo, Balozi Sefue hakupatikana jana kuelezea tuhuma hizo ambazo
hivi karibuni ziliripotiwa na gazeti moja la kila wiki kwani simu yake
iliita bila ya majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu na
baadaye simu yake haikuwa tena hewani.
Aendelea kuponda Serikali Tatu
Sitta aliendelea na msimamo wake wa kupinga mapendekezo ya Tanzania kuwa
na Serikali Tatu akisema wanaopigania hilo wana masilahi binafsi.
Sitta ambaye aliwahi pia kuwa Spika wa Bunge, alishawahi kutoa msimamo
wake kuhusu Serikali Tatu kama zilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba katika Rasimu ya Katiba akisema hakuna nchi duniani yenye
utawala wa marais watatu na endapo Tanzania itakuwa hivyo, itaweka
rekodi ya kuwa ya kwanza.
Sitta ambaye mara kadhaa ametajwa kuwa miongoni mwa wanasiasa wanaotaka
kuwania urais mwaka 2015, alisema Katiba ina masilahi ya watu aina
mbalimbali lakini hatari anayoiona ni kwa wale wenye masilahi binafsi
ambao wanaweza kuathiri mchakato huo kwa kuwa wanafikiria urais.
“Tunaweza kuwa na Serikali Tatu bila kuwa na marais watatu. Tukiwa na
Serikali Tatu tuwe na rais mmoja na labda naibu rais au makamu wa rais
au waziri mkuu, haiwezekani tukawa na marais watatu kwani hiyo ni
gharama kubwa,” alisema.
“Kuna wakati nilisema hiki ni kioja fikiria rais anasafiri kwenda nje
halafu unasikia huyu ni wa Tanganyika huyu ni wa Muungano na huyu ni wa
Zanzibar hata watu watatushangaa.”
Aidha, Sitta aliwaambia vijana hao kuwa hakubaliani na pendekezo la kuwa na mawaziri 15 katika Serikali ya Muungano.
“Utakuwaje na mawaziri 15 na wabunge wengi kujadili mambo saba ya
Muungano? Kwa nini tusiwe na mawaziri saba kwa ajili ya kusimamia mambo
hayo?”
Alisema ni vyema vijana wakajadili hayo mambo kwa kuwa ni wao
watakaonufaika au kinyume chake na Katiba Mpya kwani takwimu zinaonyesha
kwamba walio na umri wa chini ya miaka 35 nchini ni asilimia 70.
Waziri Sitta alisema vijana wanahitaji kuwezeshwa zaidi kwa kuwa
mchakato wa Katiba Mpya bado ni mrefu na wao ndio wanatakiwa kufaidika
nao.
Alisema baadhi ya viongozi wa kijamii na kisiasa ambao ni walafi
wamekuwa wakiwanunua kwa masilahi yao binafsi... “Vijana wa Tanzania ni
baridi sana kwani baadhi yenu mnakubali kununuliwa kitu ambacho ni
hatari kwa kuwa mnakaribisha Tanzania isiyotawalika.”
“Haiwezekani nchi ina wenye uwezo kupita kiasi huku wengine wakiwa
hohehahe, lazima vijana muwe wanaharakati wa kupigania utawala bora na
kuiepusha nchi isije ikaingia kwenye matatizo ya kutokuwa na amani.”
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment