Home » » VYETI VYA WATUMISHI WA SERIKALI KUHAKIKIWA UPYA.

VYETI VYA WATUMISHI WA SERIKALI KUHAKIKIWA UPYA.

Serikali imeanzisha mfumo mpya wa kukusanya takwimu zote za kila mtumishi wa umma, ili kupata taarifa zote sahihi na kuhakikisha vyeti vinavyotumiwa na watumishi hao ni sahihi na halali.

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Sekretarieti ya Ajira katika utumishi wa umma na kuzungumza na watumishi wa sekretarieti hiyo.

“Vyeti vya kughushi si tatizo la Tanzania tu na sisi tunajipanga ili kuhakikisha kila anayeingia katika ajira ya utumishi wa umma, haingii na cheti cha kughushi na kila mtu awe na cheti halali,” alisema.

Alisema katika mfumo huo, watumishi watakaobainika kughushi watachukuliwa hatua za kisheria na watakaoenda kujiendeleza, vyeti vyao vipya vitatambuliwa.

“Mtumishi ambaye cheti chake si halali, anaweza kwenda kusoma ili apate cheti wakati tunajipanga kuhakikisha watumishi wote wanaoingia katika ajira mpya za utumishi wa umma, hawaingii na vyeti vya kughushi,” alisema.

Weledi, vyeo

Balozi Ombeni aliitaka Sekretarieti hiyo kuhakikisha wote wanaoingia katika utumishi wa umma, wanakuwa na weledi na si kuingia kwa kujuana, na kuwataka Watanzania wafahamu kwamba kila mmoja mwenye sifa, anayo nafasi sawa ya kufanya kazi katika utumishi wa umma.

“Watumishi wa umma mnatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuhakikisha kila mwenye sifa anapata kazi sawa na wengine. Mtu asinyimwe kazi kwa sababu ni mtoto wa fulani, apewe kazi kulingana na vigezo,” alisema.

Pia aliwaagiza watumishi hao kuwa wabunifu kuzishughulikia changamoto na kuzingatia Mfumo wa Kupima Utendaji wa Kazi (OPRAS).

Aliagiza watumishi hao waache kupandisha mtumishi cheo kwa kuwa ametimiza miaka mitatu, bali waangalie kama ametekeleza majukumu yake kikamilifu, kwa kuwa wapo ambao wanaofanya kazi ili wasifukuzwe au kupewa adhabu.

Katika hatua nyingine, Balozi Sefue aliiagiza Sekretarieti hiyo kuboresha uhusiano na vyuo vya elimu, ili vitoe kozi zenye ajira badala ya kutoa kozi nyingi zisizo na ajira.

Alisema uhusiano huo, utasaidia kupata taarifa sahihi za wanafunzi wanaomaliza katika vyuo kupitia kwenye mfumo wa kazi data, na kurahisisha kazi kwa watumishi hao.

Awali Naibu Katibu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti na Ubora katika Sekretarieti ya Ajira, Humphrey Mniachi, alisema bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa madereva wenye sifa stahili katika soko la ajira hapa nchini.

Kwa mujibu wa Mniachi, pamoja na kupokea maombi mengi, lakini mpaka sasa wamebaini kada hiyo ya madereva ndiyo inayoongoza kwa kuwa na vyeti vingi vya kughushi, hususan vya kidato cha nne.

Alifafanua kwamba kati ya waombaji 2,390 wa nafasi za udereva, waombaji 105 walibainika kutumia vyeti vya kughushi.
 
CHANZO JUMA MTANDA BLOG

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa