Utangulizi
Ndugu wananchi;
Kama ilivyo
ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujalia
uzima na kutuwezesha kwa mara nyingine tena kutekeleza utaratibu wetu huu mzuri
tuliojiwekea wa Rais kuzungumza na taifa kila
mwisho wa mwezi.
Ndugu Wananchi;
Mwezi Julai,
2013 ulikuwa wa neema kubwa ya wageni kwa nchi yetu wakiwemo watu na viongozi
mashuhuri duniani. Natoa shukrani nyingi kwa Watanzania wenzangu kwa jinsi
tulivyowapokea wageni wetu zaidi ya 1,700.
Wamefurahi kuwepo kwao nchini na wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri
ya nchi yetu. Wageni wetu wamekuwa wa
manufaa makubwa kwa nchi yetu.
Wamesaidia kuitangaza Tanzania duniani na kuendeleza fursa za kukuza
utalii, biashara na uwekezaji nchini na kwingineko katika Afrika.
Mkutano
wa Smart Partnership
Ndugu wananchi;
Wageni wetu wa
kwanza ni wale waliokuja kuhudhuria Mkutano wa Global 2013 Smart Partnership
Dialogue uliofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Juni hadi 1 Julai, 2013. Mkutano huo
ulihudhuriwa na watu zaidi ya 800 kutoka mabara yote duniani wakiwemo
Watanzania. Miongoni mwa waliohudhuria
ni pamoja na wakuu wa nchi na Serikali, viongozi wastaafu, wanadiplomasia,
wawakilishi wa mashirika na taasisi za kimataifa, makampuni ya ndani na nje,
wafanyabiashara, wasomi, asasi za kijamii na watu wa makundi mbalimbali katika
jamii. Makampuni yetu 21 nayo yaliungana na makampuni mengine
28 kutoka nje ya nchi kushiriki
kwenye maonesho ya matumizi ya sayansi na teknolojia yaliyofanyika sambamba na
mkutano huo.
Ndugu
Wananchi;
Agenda kuu ya
majadiliano ya mwaka huu ilikuwa ni “Matumizi
ya teknolojia kama nyenzo ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi Barani Afrika
(Leveraging Technology for Africa’s
Social-Economic Transformation: The Smart Partnership Way). Tuliichagua mada hii kwa kuwa ni ukweli ulio
wazi kuwa matumizi ya sayansi na teknolojia
ndiyo chachu kubwa iliyoleta mageuzi na maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika
nchi. Ndiyo siri ya mafanikio katika nchi zilizoendelea na zinazopiga kasi kubwa
ya maendeleo duniani.
Bahati mbaya sana kumekuwa na maendeleo na matumizi madogo ya sayansi na
teknolojia katika Afrika. Ndiyo maana
nchi za Afrika ziko nyuma kimaendeleo ukilinganisha na zile zilizoendelea. Katika mkutano huo umuhimu wa kuendeleza na
kuongeza matumizi ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya maendeleo Barani Afrika
ulitambuliwa na kusisitizwa.
Mkutano ulihimiza na kusisitiza kuwa sera, mikakati na mipango ya
maendeleo ya nchi za Afrika zitoe kipaumbele kwa kuendeleza matumizi ya sayansi
na teknolojia. Nchi zetu zimehimizwa
kuwekeza katika elimu ya sayansi na teknolojia pamoja na kujenga uwezo wetu wa
ndani wa uvumbuzi, ubunifu, umiliki na uendelezaji wa sayansi na teknolojia.
Aidha, imesisitizwa kwa nchi zetu ziongeze
kasi ya kutumia sayansi na teknolojia katika shughuli mbalimbali za
kiuchumi na kijamii ili kuongeza ufanisi na kasi ya maendeleo.
Ndugu
Wananchi;
Jambo la kutia faraja kwetu nchini ni kwamba mambo yote hayo
tunayafanya. Tunachotakiwa sasa ni kufanya
vizuri zaidi na kuongeza uwekezaji na kasi ya kuendeleza matumizi ya sayansi na
teknolojia katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Tutaendelea kuboresha sera, kuboresha
mazingira ya uwekezaji na kwa ajili ya maendeleo ya sayansi na teknolojia
nchini.
Ziara ya Rais wa Marekani Nchini Tanzania
Ndugu wananchi;
Mgeni wetu wa
pili alikuwa Rais wa Marekani, Mheshimiwa Barack Obama, aliyefanya ziara nchini
kwetu kati ya tarehe 1 - 2 Julai,
2013. Lengo la ziara yake ilikuwa
kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Marekani na Tanzania. Kama mjuavyo, nchi zetu mbili zina uhusiano
wa kibalozi tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar mwaka 1964.
Uhusiano wetu
umepita katika vipindi mbalimbali na kwamba hivi sasa umekuwa mzuri zaidi
kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi zetu mbili. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la misaada ya
maendeleo kutoka Marekani na uwekezaji wa vitega uchumi na biashara navyo
vinakua. Pia ziara za kiserikali za
viongozi wa nchi zetu kutembeleana zimeongezeka. Kama mtakavyokumbuka, mwaka
2008 aliyekuwa Rais wa Marekani Mheshimiwa George W. Bush alifanya ziara ya
siku nne nchini. Pia Mawaziri mbalimbali
wa Serikali ya Marekani wametembelea Tanzania akiwemo Mheshimiwa Hilary Clinton
akiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliyekuja mwaka 2011.
Ndugu Wananchi;
Nchi ya
Marekani imekuwa mshirika wetu muhimu wa maendeleo katika nyanja
mbalimbali. Kwa upande wa afya kwa
mfano, tunapata msaada mkubwa katika mapambano dhidi ya malaria na UKIMWI. Katika maendeleo ya elimu, nako wanatusaidia katika
mafunzo ya wataalamu mbalimbali pamoja na upatikanaji wa vitabu vya sayansi na
hisabati kwa ajili ya shule za sekondari.
Kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia, Marekani inatusaidia katika
kuimarisha miundomuinu ya barabara, umeme na maji. Ujenzi wa barabara za Tanga – Horohoro,
Namtumbo – Songea – Mbinga; Tunduma – Sumbawanga na baadhi ya barabara za
Pemba, ujenzi wa njia ya pili ya kupeleka umeme Unguja kutoka Dar es Salaam,
ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia na usambazaji wa umeme katika Mikoa 10 ya
Tanzania bara ni miongoni mwa matunda ya msaada wa Mfuko huo. Pamoja na hayo, ipo miradi ya kuongeza maji
katika jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Morogoro ambayo inaendelea
kutekelezwa.
Ndugu Wananchi;
Wakati wa
ziara yake, Rais Obama alielezea na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali yake
ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi zetu. Alielezea kuridhika na hatua tuliyofikia ya kukuza
demokrasia nchini, utawala bora na kuwekeza katika maendeleo ya watu wetu. Aliahidi kuendelea kuunga mkono juhudi
zetu. Katika hili ameahidi kuongeza
misaada ya maendeleo na kiufundi katika sekta za afya, elimu, kilimo, barabara,
nishati na maendeleo ya vijana. Pia,
alithibitisha kwamba nchi yetu itaendelea kunufaika na ufadhili wa Awamu ya
Pili ya Mfuko wa Changamoto za Millenia.
Katika awamu hii, maeneo yatakayopewa kipaumbele hapa kwetu ni umeme na
barabara za vijijini. Mazungumzo ya
miradi itakayotekelezwa katika awamu hiyo yanaendelea vizuri.
Power
Africa
Ndugu Wananchi;
Rais Obama
alitumia fursa ya ziara yake nchini kuzindua mpango wa Serikali yake wa
kusaidia maendeleo ya sekta ya umeme katika Bara la Afrika. Mpango huu unaoitwa “Power Africa Initiative”
umetengewa kiasi cha dola za Marekani bilioni
7 na Serikali ya Marekani na makampuni binafsi ya nchi hiyo yameahidi
kuwekeza dola bilioni 9 katika
mpango huo. Kwa kuanzia, nchi sita za Afrika (Ethiopia, Ghana,
Nigeria, Tanzania, Liberia na Kenya) ikiwemo Tanzania zitahusishwa.
Bila ya shaka
Mpango huo ukikamilika utasaidia sana kuimarisha upatikanaji wa umeme barani
Afrika ambayo ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ni ukweli ulio wazi kuwa ukosefu wa umeme wa
kutosha na wa uhakika ni sababu kubwa inayokwamisha maendeleo ya haraka katika
nchi za Afrika. Hivyo basi, msaada huu
ni muhimu sana kwetu. Kwa ajili hiyo
nimeagiza Wizara ya Nishati na Madini iandae mkakati madhubuti wa namna
Tanzania itakavyoshiriki na kufaidika na mpango huo. Nataka mpango huo utakapoanza kutekelezwa
utukute sisi tupo tayari kutumia fursa zake.
Vile vile, ndugu
wananchi, katika ziara hiyo Rais Obama alielezea nia ya Serikali yake kutaka kuwepo
mpango wa kukuza ushirikiano wa biashara na uwekezaji baina ya nchi yake na
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Nimeelekeza Wizara husika yaani Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko nao watengeneze mkakati
utakaoonesha jinsi tulivyojipanga kufaidika na mpango huo. Lazima tujiandae vyema na mapema tunufaike
saiwa na mpango huo.
Ziara
ya Rais Mstaafu wa Marekani Nchini
Ndugu Wananchi;
Sambamba na
ziara ya Rais Obama, nchi yetu ilipata bahati ya kutembelewa tena na Rais
Mstaafu wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush na mkewe Laura Bush, tarehe 1
hadi 3 Julai, 2013. Kwa udhamini wa
asasi ya George W. Bush Foundation waliandaa Mkutano wa Wake wa Marais wa
Afrika uliofanyika hapa Dar es Salaam, tarehe 2 na 3 Julai, 2013. Mama Michelle Obama naye alishiriki mkutano
huo uliozungumzia kuimarisha maendeleo na afya ya wanawake Barani Afrika.
Katika mkutano
huo, pia, Mheshimiwa George W. Bush alizindua mpango wa kuimarisha mapambano
dhidi ya kansa ya shingo ya kizazi na matiti barani Afrika. Kufuatia Mpango huo, Serikali ya Marekani
imetoa dola milioni 3 na mashine 16
za Cryo Therapy zinazotumia baridi kali kuua chembechembe za kansa. Msaada huo ni muhimu hasa ukizingatia kuwa
kila mwaka hapa nchini zaidi ya Watanzania 21,000 wanapata maradhi ya
kansa. Kati ya hao asilimia 29.4 ni wanawake
wanaopata magonjwa ya kansa ya shingo ya uzazi na asilimia 6.2 wanapata kansa ya matiti. Naamini Mpango huu
utatusaidia sana katika kuimarisha mapambano dhidi ya maradhi haya
yanayowasumbua na kuua kina mama wengi nchini.
Nimeitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuweka utaratibu mzuri ili
msaada huo utumike ipasavyo na kuwanufaisha walengwa.
Ziara
ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Nchini
Ndugu Wananchi;
Tarehe 23
mwezi Julai, 2013 pia tulitembelewa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza,
Mheshimiwa Tony Blair. Katika mazungumzo
yetu Mheshimiwa Blair aliahidi kuisaidia nchi yetu kupitia taasisi yake ya
Africa Governance Initiative kusaidia kusambaza umeme wa jua katika shule zetu
za sekondari vijijini, maboresho ya shirika letu la umeme (TANESCO) na kusaidia
uanzishaji na uimarishaji wa Kitengo cha Rais cha Ufuatiliaji Utekelezaji wa
Programu za Maendeleo (Presidential Delivery Bureau - PDB). Tunamshukuru kwa ahadi yake hiyo
itakayochangia katika jitihada za kujiletea maendeleo.
Ziara
ya Waziri Mkuu wa Thailand Nchini
Ndugu Wananchi;
Tarehe 30
Julai, 2013 tulimpokea Mheshimiwa Yingluck Shinawatra, Waziri Mkuu wa Thailand aliyefanya
ziara ya siku tatu nchini. Lengo la ziara
yake ni kuimarisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Thailand na Tanzania. Katika
ziara hiyo, tumezindua Jukwaa la Wafanyabiashara wa Thailand na Tanzania (Thai-Tanzania
Business Forum) ili kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi zetu. Waziri Mkuu Yingluck Shinawatra alitumia
fursa hiyo kufafanua sera ya Thailand kwa Afrika inayosisitiza kukuza
ushirikiano wa karibu wa kiuchumi na kibiashara. Pia amepata nafasi ya kutembelea Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti kujionea mwenyewe jinsi nchi yetu ilivyobarikiwa kwa kuwa na
kivutio hicho cha aina yake. Alipokuwa
kule nchi zetu zilitiliana saini maelewano ya ushirikiano katika kulinda na
kuhifadhi wanyama pori.
Katika
mazungumzo yangu na yeye, tumekubaliana kuchukua hatua thabiti kukuza
ushirikiano katika nyanja mbalimbali.
Tumetiliana saini mikataba mitano ya ushirikiano kwa mambo
yafuatayo: Kukuza na kulinda vitega
uchumi; kubadilishana wafungwa; ushirikiano wa kiufundi; na ushirikiano kwa
masuala ya madini. Aidha, Waziri Mkuu huyo ameahidi kuwahimiza wawekezaji wa
nchini mwake kuja Tanzania kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi ikiwemo
kilimo, utalii, viwanda nakadhalika. Pia,
Waziri Mkuu wa Thailand ameahidi kuwa Serikali yake itatoa ufadhili kwa vijana 10 kusoma Shahada ya Uzamili nchini
humo. Vile vile, nchi hiyo itaanza
kuleta wataalamu wa afya wa kujitolea kuja kushirikiana na wataalam wetu
kuimarisha huduma ya afya nchini.
Ziara hizi
zinaonesha utayari wa dunia kuunga mkono jitihada zetu za kujiletea
maendeleo. Naomba Watanzania wenzangu
tutumie vizuri utayari huo wa dunia kuongeza kasi ya maendeleo yetu. Tusijikwaze wenyewe.
Ziara
ya Kagera
Ndugu wananchi;
Kuanzia tarehe
24 hadi 29 Julai, 2013, nilifanya ziara Mkoani Kagera. Nilishiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya
Mashujaa na kuzindua jengo jipya la Mahakama Kuu. Pia niliweka jiwe la msingi
la upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Bukoba na kuweka mawe ya msingi ya ujenzi
wa kiwango cha lami kwa barabara za Kigoma – Lusahunga na Kyaka – Kayanga –
Bugene. Vile vile nilizindua Wilaya mpya
ya Kyerwa na kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kuona na kusikiliza
changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ili kuzitafutia majawabu.
Sherehe za
Kumbukumbu ya Mashujaa zilifana sana.
Niliwapongeza viongozi wa Jeshi na wa Mkoa kwa maandalizi mazuri ya sherehe
hizo. Pia nilirudia kumpongeza Mkuu wa
Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange, kwa uamuzi wake wa busara wa kufanya
sherehe za kumbukumbu za mashujaa wetu pale Kaboya badala ya kufanyikia Dar es
Salaam tu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Ni uamuzi muafaka na wa busara kwani pale Kaboya ndipo walipolala mashujaa wetu waliopoteza maisha yao kutetea
mipaka na uhuru wa nchi yetu dhidi ya Nduli Iddi Amin. Hali kadhalika, kule Naliendele, Mtwara
ambapo sherehe za mashujaa zilifanyika mwaka wa juzi, ndipo walipozikwa
mashujaa wetu waliopoteza maisha kuisaidia nchi jirani na rafiki ya Msumbuji
kutetea Uhuru wake dhidi ya wakoloni, makaburu na vibaraka wao wa ndani ya
Msumbiji.
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba
yangu pale Kaboya niliwakumbusha Watanzania wenzangu kwamba katika kuwakumbuka
mashujaa wetu wale na wale sisi tulio hai, hatuna budi kutambua wajibu wetu wa
kuwa tayari kujitolea muhanga kwa ajili ya kulinda uhuru wa mipaka ya nchi
yetu. Nilisisitiza utayari wa nchi yetu
kulinda mipaka yake na kwamba mfano wa mashujaa waliolala pale ni fundisho kwa
mtu ye yote anayetamani kumega kipande cho chote cha ardhi ya nchi yetu. Atakiona cha mtema kuni kilichomkuta Nduli
Iddi Amini au hata zaidi.
Nimesikia kuwa
kauli yangu ile imetafsiriwa visivyo na kupotoshwa na baadhi vyombo vya habari
na hata majirani zetu. Tafsiri hizo ni
potofu. Sikumtaja mtu ye yote au nchi yo
yote. Nilikuwa nazungumzia wajibu wa
majeshi yetu na raia wa nchi yetu wa kulinda uhuru na mipaka yetu na kwamba
hatutamruhusu mtu au nchi yo yote kutupokonya wala kuichezea haki yetu hiyo ya
msingi. Tuko tayari kuitetea hata kama
gharama yake ni maisha yetu kama walivyofanya mashujaa waliolala Kaboya.
Mahakama
Kuu
Ndugu Wananchi;
Katika
ufunguzi wa Mahakama Kuu ya Bukoba nilisisitiza dhamira na utayari wa Serikali yetu
kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kuwa na Mahakama Kuu katika kila Mkoa. Baada ya kukamilika kwa Mahakama Kuu ya
Bukoba bado kuna Mikoa 14 hainazo.
Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14 tumetenga fedha za kujenga
Mahakama Kuu katika Mikoa 7 na nilirudia ahadi yangu kuwa katika mwaka ujao wa
fedha tutatoa fedha za kumalizia Mikoa 7 iliyosalia. Niliamua tuongeze kasi ya kujenga Mahakama
Kuu hizo ili kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kutimiza ipasavyo wajibu wake wa
kutoa haki nchini.
Maendeleo
ya Mkoa wa Kagera
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa
Kagera nilifurahishwa na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya
kiuchumi na kijamii. Taarifa za Mkoa na
Wilaya zimefafanua kwa kina mambo mazuri yaliyofanyika na yanayoendelea
kufanyika Mkoani. Wameelezea furaha yao
kwa mafanikio yaliyopatikana ambayo baadhi nimeyashuhudia au hata kushiriki kuyazindua
na kuweka mawe ya msingi. Taarifa hizo
pia zimelezea mambo mengi zaidi wanayotaka yafanyike na matatizo mapya na hata
ya zamani ambayo wanataka yapatiwe ufumbuzi.
Katika
mazungumzo yangu na viongozi na wananchi, yapo mambo ambayo yako kwenye uwezo
wao kijijini, Wilayani na Mkoani kuyapatia ufumbuzi. Tulikubaliana na kuelekezana nini
kifanyike. Yapo mengine mengine ambayo yanahitaji
nguvu ya taifa tumeyachukua kuja kuyafanyia kazi. Kuna baadhi yaliwahusu Mawaziri ambao
nilikuwa nao ziarani waliyasemea na kuyafanyia kazi palepale yalipojitokeza.
Ulinzi
na Usalama
Ndugu Wananchi;
Kuna mambo
matatu yahusuyo usalama ambayo yalizungumzwa na wananchi kwa uchungu mkubwa
ambayo niliamua tuyashughulikie kitaifa.
Mambo hayo ni ujambazi wa kutumia silaha kuteka magari, kupora mali na
watu kuuawa. Jambo la pili ni wahamiaji
kutoka nchi jirani wanaoingia, kuishi na kufanya shughuli nchini kinyume cha
sheria. Na tatu, mifugo kuingizwa kwa
wingi nchini bila kufuata taratibu husika na mingine kuingizwa katika hifadhi
za wanyama.
Ndugu wananchi;
Nilitoa
maagizo kwa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama yaani JWTZ, Polisi, Usalama
wa Taifa na Uhamiaji watengeneze mpango kabambe wa kuyashughulikia matatizo
hayo. Watayarishe na kutekeleza
operesheni maalum itakayo au zitakazokomesha ujambazi, kuondoa wahamiaji
wasiokuwa halali na kuondoa mifugo iliyoingizwa nchini kinyume na utaratibu na
ile iliyoko kwenye maeneo yasiyo stahili.
Aidha,
niliwataka majambazi wajisalimishe na wasalimishe silaha zao ndani ya wiki mbili
na siku hizo zinaanzia tarehe 29 Julai, 2013 nilipomaliza ziara yangu Mkoani humo. Kwa wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha
sheria nimewataka watumie muda huo kuondoka nchini au kuhalalisha ukaazi
wao. Hivyo hivyo kwa mifugo iliyoingizwa
nchini kinyume na sheria au ile iliyoko kwenye maeneo yasiyostahili. Ndani ya muda huo watu wote waondoe mifugo
yao au wajitokeze kufuata taratibu zilizopo.
Ndugu Wananchi;
Nilisema
nilipokuwa Mkoani Kagera na narudia tena leo kuwa baada ya siku 14 kupita,
vyombo vya ulinzi na usalama vitaendesha operesheni maalum ya kushughulikia
matatizo hayo. Nilisema kuwa operesheni
hiyo itafanyika katika Mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita kwa wakati mmoja. Napenda kuwahakikishia kuwa hapatakuwa na
mahali pa kukimbilia wala kujificha.
Nawashauri wale wote wanaohusika na ujambazi, uhamiaji haramu na
uingizaji haramu wa mifugo waamue kuchukua hatua muafaka sasa. Wasisubiri operesheni iwakute, wala
wasifikirie kuwa hili ni jambo la kupita.
Safari hii itakuwa endelevu.
Ndugu Zangu;
Hatuwezi
kukubali hali hii niliyoikuta Mkoani Kagera ikaachwa kuendelea. Italeta madhara makubwa zaidi siku za
usoni. Haiwezekani raia katika nchi yake,
akose uhuru na usalama wa kutembea peke yake mpaka asindikizwe na Polisi. Na, baya zaidi hata Polisi nao wanashambuliwa
na kuuawa watakavyo majambazi. Uhalifu
huu lazima ukomeshwe, uishe na usijirudie tena.
Pia, haiwezekani
hali ya watu kutoka nchi jirani kuingia nchini, kuishi na kufanya shughuli na
kutoka watakavyo. Hatuzuii watu kuingia
na kuishi Tanzania lakini wafuate sheria na taratibu za kuhamia na kuishi
katika nchi yetu. Nchi yetu ina sifa na
ukarimu huo. Hakuna uthibitisho mkubwa zaidi ya ule wa mwaka 1982, Rais Julius
Nyerere wakati ule alipowaruhusu wakimbizi wanaopenda kuwa raia wa Tanzania
wafanye hivyo. Wakimbizi 30,000 tu waliitumia fursa hiyo. Mwaka 2010 tuliwapa uraia wakimbizi 160,000 wa kutoka Burundi. Kwa sababu hiyo hatuoni sababu ya
watu kufanya wanayoyafanya sasa kule Mkoani Kagera. Hatuwezi kuacha hali hiyo iendelee ilivyo.
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa
Mkoani Kagera nilielezea kusikitishwa kwangu na vitendo vya baadhi ya watendaji
na viongozi wa vijiji na wananchi kuwaruhusu watu kuingia na kuishi nchini
kinyume cha sheria. Nimewataka waache
mtindo huo. Nimeagiza na wao wajumuishwe
katika operesheni ijayo. Watakaobainika
kujihusisha na vitendo hivyo haramu wachukuliwe hatua zipasazo kisheria. Aidha, niliwataka Maafisa wa Uhamiaji
watimize ipasavyo wajibu wao. Ukweli ni
kwamba, mambo haya kuendelea kwa muda mrefu kiasi hiki ni kwa sababu ya udhaifu
wa mamlaka husika. Vile vile, nimewataka
TAKUKURU nao watimize wajibu wao. Hapa
kuna uthibitisho tosha wa kuwepo kwa vitendo vya rushwa vinavyohusisha
wahamiaji hao na maofisa wa vijiji na idara husika za Serikali. Mimi naamini kama TAKUKURU ikiwabana na
Uhamiaji wakichemka vya kutosha tatizo hili lingepungua sana au hata kutokuwepo
kabisa.
Uhusiano
na Nchi ya Rwanda
Ndugu wananchi;
Katika kipindi
cha miezi miwili sasa hususan tangu mwishoni mwa mwezi Mei, 2013, uhusiano
baina ya nchi yetu na Rwanda unapitia katika wakati mgumu. Kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yangu na
nchi yetu ni ushahidi wa kuwepo hali hiyo.
Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu na ndugu zetu wa Rwanda kuwa
mimi, Serikali ninayoiongoza na wananchi wa Tanzania tunapenda kuwa na uhusiano
mzuri na ushirikiano wa karibu na Rwanda kama ilivyo kwa nchi zote jirani. Kama majirani kila mmoja anamuhitaji mwenzake,
hivyo lazima tuwe na uhusiano mwema na ushirikiano mzuri.
Napenda kusisitiza
kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au
vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi yo yote jirani au yo yote duniani. Hatuna sababu ya kufanya hivyo kwani ni mambo
ambayo hayana tija wala maslahi kwetu.
Ndugu Wananchi;
Ukweli ni
kwamba wakati wote tumekuwa tunajihusisha na mambo ya kukuza na kujenga ujirani
mwema na kufanya mambo ambayo yatasaidia kuimarisha uhusiano wetu kwa maslahi
ya nchi zetu. Hiyo ni moja ya nguzo kuu
ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania. Huo ndiyo ukweli kuhusu uhusiano wetu na
nchi ya Rwanda kabla na hata baada ya sintofahamu iliyojitokeza sasa. Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa Rwanda
kuwa kwa upande wetu hakuna kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na
ushirikiano wetu. Mambo yapo vile vile. Kwa upande wangu, binafsi, sijasema lo
lote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye
vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu.
Siyo kwamba siambiwi yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la
hasha. Sijafanya hivyo kwa sababu sioni
faida yake. Kwangu mimi sioni kama kuna
mgogoro wa aina yo yote. Busara
inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo.
Waingereza wanasema “two wrongs do
not make a right”.
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo
uhusiano wetu na Rwanda umekuwa mzuri kwa miaka mingi. Tunashirikiana na kusaidiana kwa mambo mengi
baina ya nchi zetu kitaifa na katika kanda yetu ya Afrika Mashariki na Nchi za
Maziwa Makuu, katika Umoja wa Afrika na hata kimataifa. Uhusiano unaelekea kupata mtikisiko baada ya
mimi kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao. Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa
kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo
njia hiyo ni vyema itumike. Isitoshe, ushauri
ule niliutoa pia kwa Serikali ya Kongo na kwa Serikali ya Uganda. Katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni wa
Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais wa Rwanda hakusema cho chote pale
mkutanoni. Baada ya kurudi nyumbani
ndipo tukaanza kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia.
Kwa kweli
nimestaajabu sana na jinsi walivyouchukulia ushauri wangu na
wanayoyafanya. Havifanani kabisa, completely out of proportion and out of
context. Mimi nilifanya vile kwa kuzingatia mila na desturi zetu za
miaka
mingi katika ukanda wetu. Tumekuwa
tunakutana katika mikutano na vikao mbalimbali tunazungumza na
kushauriana kwa
uwazi juu ya njia za kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila
yanapotokea. Wakati wote tumeyachukulia
kuwa ni mambo yanayotuhusu sote hivyo kupeana ushauri ni wajibu wetu
wote. Na mara nyingi ushauri kwa wanaogombana
kuzungumza tunautumia sana. Iweje leo
mtu kutoa ushauri ule lionekane jambo baya na la ajabu. Jambo la
kushutumiwa na kutukanwa! Siyo sawa hata kidogo!! Ushauri si shuruti,
ushauri
si amri. Una hiyari ya kuukubali au
kuukataa. Muungwana hujibu: “Siuafiki ushauri wako”. Hakuna haja ya
kutukana wala kusema maneno
yasiyostahili wala kusema yasiyokuwepo na ya uongo.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kurudia kusema kuwa mimi binafsi na Serikali yetu ya Tanzania hatuna ugomvi
wala nia yo yote mbaya na Rwanda.
Tunapenda tuendelee kuwa na uhusiano mzuri na Rwanda. Labda wenzetu wanalo lao jambo dhidi yetu
ambalo sisi hatulijui. Maana na sisi
tunasikia mengi yanayozungumzwa na kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi
yangu na nchi yetu. Hatupendi kuyaamini moja
kwa moja tunayoyasikia lakini hatuyapuuzi.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya
kumaliza, naomba kutumia nafasi hii pia kuwatakia Waislamu wote nchini heri na
baraka tele katika kukamilisha ibada muhimu ya kufunga mwezi Mtukufu wa
Ramadhan. Naomba tuendelee kuwatakia heri
ili wamalize salama na tuweze kusherehekea kwa furaha na bashasha tele siku kuu
ya Idd el Fitr pindi itakapowadia.
Mwisho kabisa,
nawaomba Watanzania wenzangu wote tuendelee kushirikiana na kuishi kwa upendo,
umoja na mshikamano kama ilivyo kawaida yetu.
Mungu
Ibariki Tanzania!
Mungu
Ibariki Afrika!
Asanteni
Sana Kwa Kunisikiliza.
0 comments:
Post a Comment