Home » » WABUNGE WA VITI MAALUM WAMJIBU JUU WAZIRI SITTA.

WABUNGE WA VITI MAALUM WAMJIBU JUU WAZIRI SITTA.

 
MHE SAMWEL SITTA.
SPIKA WA BUNGE ANNA MAKINDA.
  Akizungumza jana kwenye mkutano wa Chama cha Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG), kujadili mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Esther Bulaya alisema wanafanya kazi nchi nzima kuwashinda wabunge waliochaguliwa.
“Mara nyingi hawa wabunge waliochaguliwa na wananchi wanalalamikiwa kwamba hawapatikani, lakini sisi wa viti maalumu muda mwingi tuko na wananchi kuangalia changamoto zinazowakabili na kuziwasilisha sehemu husika ili zitatuliwe,” alisema Bulaya. 
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zarina Madabida alisema wana michango mizuri, pia uwezo wa kuzunguka nchi nzima kutatua kero zinazowakabili wananchi. 
Madabida alisema kauli ya Waziri Sitta siyo sahihi akitamba kuwa wanafanya kazi na wakati mwingine kuf ika maeneo ambayo wabunge waliochaguliwa na wananchi hawafiki.
Hata hivyo, alitaka uandaliwe utaratibu mzuri wa kuwapata wabunge hao bila ya kujali itikadi za siasa ili watakaochaguliwa wawe ni wachapa kazi.
Mbunge mwingine wa Viti Maalumu (CCM), Ritha Kabati alisema hawaonekani kama wanafanya kazi kwa kuwa hawashirikishwi kwenye Mfuko wa Jimbo jambo linalowanyima fursa ya kutoa michango yao.
Hata hivyo, Kabati alihojiwa na gazeti hili siku chache baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa rasimu yake ikifuta viti hivyo na kusema: “Ni bora Tume ya Warioba walivyoondoa viti maalumu. 
Vilikuwa vinatudhalilisha, watu walikuwa hawatupi thamani halisi kama wabunge.” Awali, akifungua mkutano huo, Spika wa Bunge,
Anne Makinda aliwataka wabunge hao kujipanga na kutokufanya makosa kufikia uamuzi kuhusu Rasimu ya Katiba.
“Hii ni fursa ya kipekee na muhimu kwenu wabunge wanawake na Taasisi ya Bunge kwa jumla. Hatuna budi kujipanga vizuri katika kutoa maoni yetu.
“Miaka 50 baada ya uhuru, wanawake hatuna tena sababu na msamaha wa kutokushiriki kwenye zoezi hili muhimu kikamilifu... wanawake tumepata uzoefu wa kutosha, tunayo elimu ya kutosha na tunayo sauti. Kubwa zaidi ya yote tunajiamini.”
“Sisi wachache tuliokusanyika hapa tumebahatika. 
Ni mithili ya taa za mbele za gari ambazo ndizo humwongoza dereva wakati wa giza. Hivyo, tuna wajibu wa kuyasema matatizo na changamoto zinazowakabili wanawake na makundi mengine kama vile watoto na walemavu hususan wakati huu tunapoandika Katiba Mpya.”
“Bado kuna masuala ambayo sisi kama taasisi tungependa yaingizwe kwenye Rasimu ya Katiba. Ni vizuri tunapoandika Katiba Mpya, mihimili hii hususan Mahakama na Bunge iwiane ili kuleta heshima na kuaminiana zaidi.” MWANANCHI

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa