Home » » UCHAMBUZI KUTOKA TONE MULTIMEDIA: TCRA imetutambua ‘bloggers’, lakini sisi tunajitambua?

UCHAMBUZI KUTOKA TONE MULTIMEDIA: TCRA imetutambua ‘bloggers’, lakini sisi tunajitambua?


Mwezi Julai umemalizika kwa habari njema kwa wamiliki na watumiaji wa mitandao ya kijamii (blogs) baada ya Mamlaka ya Mawasilinao Nchini, (TCRA) kutangaza kutambua rasmi kazi za mitandao hiyo ambayo inaelimisha, habarisha na kuburudsha.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa warsha ya uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha matumizi mazuri ya miandao ya mawasiliano Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dr. Nkoma akatangaza umuhimu wa mitandao hii katika maendeleo ya taifa.
Hatua hii ya TCRA kutambua mitandao ya kijamii si tu imeonyesha uungwana bali imezingatia na kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na watanzania hao katika kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya maswala mbalimbali.
Hapa nawapongeza TCRA kwa kuonyesha demokrasia na uhuru wa kujieleza lakini pia inaonyesha ni kwa jinsi gani TCRA imekubali kasi ya mabadiliko katika sekta ya mawasiliano ambayo yanakuja kwa nguvu kubwa kila kukicha kutokana na kukua kwa teknolojia duniani.
Kwa kuzingatia umuhimu wa blogs katika maisha ya kila siku ya watanzania walio wengi hasa watumiaji wa internet, TCRA wameona ni swala muhimu kutushirikisha katika kampeni hii ya kuhamasisha matumzi mazuri ya mitandao ya mawasiliano.
Kutambuliwa na TCRA ni hatua ya kwanza lakini hatua ya pili ni kwa bloggers kujiambua wao wenyewe, ni kweli tunajitambua kwa kile tunachokifanya? Tunaelewa mchango wetu katika maisha na maadili ya taifa hili? Tunaelewa nini tunataka ku-‘achieve’?
Haya ni baadhi tu ya maswali ambayo kila blogger anapaswa kuyajibu ili kujua mchango wa kazi yake katika jamii anayoitumikia na manufaa yake maana Blog ni biashara nzuri lakini ‘trust me’ hakuna atakayekuja kutangaza kwako kama habari zako ni za uchochezi, udanganyifu na uhuni usiokuwa na maana.
Sina tatizo na wingi wa blogs zinazoanzishwa kila kukucha, lakini tatizo langu ni malengo ya uanzishwaji wa mitandao hii, maana blog nyingi hazina malengo na kama malengo yapo basi ni malengo hasi ambayo hayana manufaa yoyete kwa jamii zaidi ya kuvuruga amani, kuchochea vurugu na chuki, kuchonganisha watu, kusababisha ugomvi, kuwaumiza wengine kwa mambo yasioyo ya ukweli, kupotosha jamii na hata kuvuruga maendeleo kwa ujumla.
Wewe mmiliki na mtumiaji wa mtandao unajua fika unachokifanya na kama kinaangukia katika malengo hayo hapo juu tafadhali kuwa muungwana na ujitambue kwa kuanza kufuta na kutoweka kabisa habari mbaya maana itakuwa ni kazi bure TCRA kukutambua huku ukiendelea kuwalisha ‘uchafu’ huo watanzania.
Hebu tuonyeshe ukomavu, utu, weledi na uungwana wetu katika kuifanya kazi hii, hata kama hujasomea fani ya uandishi wa habari naamini kuna maadili yanayokuongoza ama kutoka katika familia, dini, shule na kadhalika, mbona kuna watu hawajasomea uandishi wa habari na wanazingatia maadili katika kutumia mitandao yao!
Tukatae kutumiwa na wanasiasa na makundi ya watu wachache wenye nia ya kuharibu amani ya nchi kwa maslahi yao binafsi bali tushirikiane katika kufichua kila baya linalolenga kuharibu amani na ustaarabu wa nchi hii
Bloggers Solidarity Forever!
Imeandaliwa na Dotto Kahindi wa tabianchi na blogszamikoa

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa