Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome akifafanua kwa waandishi wa habari (hawapo
pichani) juu ya upangaji wa viwango vya alama, matumizi ya alama endelevu ya mwanafunzi
na ufaulu leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Kamishna wa Elimu Profesa
Eustella Bhalasesa.
Baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Sifuni
Mchome (hayupo pichani).
Waandishi wa habari na maafisa wa Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome(hayupo pichani). Picha zote na Eliphace Marwa (MAELEZO).
======== ======= ========
UPANGAJI
WA VIWANGO VYA ALAMA, MATUMIZI YA ALAMA ENDELEVU YA MWANAFUNZI NA UFAULU
UTANGULIZI
Wizara imekusanya maoni ya Wadau
wa Elimu kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama (Grade Ranges) katika Mitihani ya
Kuhitimu Kidato cha Nne na cha Sita pamoja na Matumizi ya Alama za Tathmini
Endelevu ya Mwanafunzi (Continuous Assessment ama CA) kwa ajili ya kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi. Maoni ya
wadau yamekusanywa kwa sababu kwa muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya alama
vinavyotumika na utaratibu wake katika mitihani ya kuhitimu Kidato cha Nne na
Kidato cha Sita umekuwa haufanani pamoja na kwamba mitihani hiyo yote ni ya
elimu ya sekondari. Pia mfumo masuala mbalimbali ya mitihani katika elimu ya
sekondari umekuwa na miundo tofauti ikiwemo ule unaotumika shuleni na ule wa
Baraza la Mitihani la Taifa. Kwa sasa kuna miundo mikuu miwili katika mfumo
huo.
Muundo wa Kwanza ni upangaji wa
viwango katika ngazi ya Shule ambapo Alama Mgando (Fixed Grade Ranges)
zifuatazo hutumika kupanga madaraja: A = 81 – 100; B = 61 – 80; C = 41 – 60; D
= 21 – 40 na F = 0 – 20. Muundo huu umetumika kwa muda mrefu na umezoeleka kwa
walimu na wanafunzi wa elimu ya sekondari kwa ujumla.
Muundo wa Pili ni wa viwango
vinavyotumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa ambapo ambapo kabla ya mwaka 2012
muundo wa viwango nyumbufu (flexible
grade ranges) ulitumika. Katika muundo huu uwigo wa alama ulibadilika
badilika kulingana na hali ya matokeo ilivyokuwa kwa mwaka husika. Lakini
kuanzia mwaka 2012, Serikali iliamua kutumia mfumo wa Upangaji wa Alama Mgando
(Fixed Grade Range) kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita. Katika mtihani wa
Kidato cha Nne mwaka 2012 Baraza lilitumia mfumo huu wa alama mgando ambapo: A
= 80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49, F = 0 – 34. Kwa upande wa
Kidato cha Sita Baraza lilitumia mfumo wa A = 80 – 100; B = 75 - 79; C = 65 –
74; D = 55 – 64; E = 45 – 54; S = 40 – 44 na F = 0 – 39. Mifumo hii ya Baraza
haikuwa inafahamika kwa wadau na hivyo kuwa sehemu ya malalamiko katika sekta
ya elimu na mafunzo.
Vilevile, Sera ya Elimu na
Mafunzo ya mwaka 1995 imeelekeza kwamba katika kuamua kiwango cha ufaulu wa
mwanafunzi wa elimu ya sekondari, Alama za CA
zitachangia asilimia hamsini (50%) na Mtihani wa mwisho utachangia asilimia
hamsini (50%). Kwa upande wa Zanzibar, CA
zimekuwa zikiandaliwa kwa mfumo wa asilimia arobaini (40%) na mtihani wa mwisho
asilimia sitini (60%). Pamoja na kwamba Baraza halijawahi kuutumia mifumo hii
tangu ilipowekwa, kumekuwa na mitazamo, maoni na mapendekezo tofauti katika
muundo na matumizi ya alama za CA.
Kuna mawazo pia kwamba mfumo wa CA
kuchangia matokeo ya mwisho ya mwanafunzi pia utumike kwa watahiniwa wa
kujitegemea (private candidates). Kwa
sasa matokeo ya mitihani ya watahiniwa hawa yamekuwa yakitumia alama za mtihani
wa mwisho tu na hivyo kutafsiriwa kama utaratibu ambao unamwonea mwanafunzi
ambaye anahamu ya kujiendeleza kielimu lakini anakwama kwa sababu mfumo
unaotumika siyo rafiki kwa mtahiniwa.
Kwa mantiki hii, Wizara
imedhamiria kufanya harmonization ya
masuala ya alama katika mitihani ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita ili
kupata muundo mmoja na ulio wazi kwa wadau wote wa elimu ya sekondari. Lakini
pia serikali imedhamiria kuhakikisha tathmini za wanafunzi katika ngazi
mbalimbali zinakwenda sambamba na matarajio ya mitaala inayotumika na ambayo
inahuishwa mara kwa mara ili iendane na wakati na mahitaji ya elimu katika
ngazi mbalimbali.
VIWANGO
NA UTARATIBU KUANZIA MWAKA 2013 KWA KIDATO CHA NNE NA
MWAKA
2014 KIDATO CHA SITA
Baada ya kufanya tathmini ya maoni mbalimbali ya
wadau, misingi ifuatayo ilizingatiwa katika maamuzi kuhusu makundi ya alama na
muachano wake:
a) Alama
zitakazotumika zitakuwa A, B, C, D, E na F. Muachano
wa alama kati ya kundi moja hadi jingine utafanana, isipokuwa tu pale ambapo
itaonekana kuna sababu na hakuna athari za kuwa na muachano tofauti na ule
ambao umetumika katika makundi mengine.
b) Makundi ya
alama hayatakuwa na clusters
isipokuwa pale ambapo itaonekana kufanya hivyo kunaleta tija katika kupata
picha ya wahitimu kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Kwa mantiki hii
(i) makundi ya alama A, C, D, E na F yabaki na cluster moja moja bali kundi la alama B litakuwa na clusters mbili.
Kundi la kwanza litakuwa la wale ambao wamepata alama kati ya 50 mpaka 59 na
litaitwa B na lingine litakuwa la wale ambao wamevuka uwigo wa 50 hadi 59 na
kuelekea uwigo wa 60 hadi 74 na hili litaitwa B+ (angalia jedwali hapo chini).
(ii) Pamoja na kuwa na muachano wa alama 26
kama jedwali linavyoonesha hapo chini, alama A kwa miaka
mingi imekuwa ikianzia alama 75 hadi 100 na kwamba pamoja na uwigo huo bado
wanaofaulu kwa kiwango hicho ni wachache sana. Kwa mantiki hii, hakuna haja ya
kubadilisha uwigo ila juhudi ziendelee katika ufundishaji na ujifunzaji ili
kiwango cha ufaulu kiongezeke na kupata wanafunzi wengi zaidi wanaofaulu katika
kundi hili.
(iii)
Pia, pamoja na kuwa na muachano wa alama
20 kama jedwali linavyoonesha hapo chini kwa miaka mingi, huko shuleni
mwanafunzi aliyepata alama 21 na hadi 30 alihesabiwa kuwa na ufaulu wa
chini
kabisa au hafifu kwa kiwango cha alama D na ingawa
ilikubalika ufaulu wa aina hiyo kwa mazingira ya nchi yetu unaridhisha.
Alama F ilikuwa ni kwa wale waliopata chini ya hapo. Hivyo, alama F
itaendelea kuwepo na itaanzia alama 0 hadi 19 na E itaanzia
alama 20 hadi 29 na D – 30 -39. Lengo la muundo huu
ni kuwa alama mbalimbali, isipokuwa kwa makundi machache, zianzie kwenye
0 yaani
0, 10, 20, 30, 40 na kuendelea badala ya kuanzia kwenye moja yaani 1,
11, 21,
31, 41 na kuendelea. Hii ni kwa ajili ya kuleta mtizamo unaofanana
katika ngazi
mbalimbali za elimu ambapo kwa sasa ngazi ambazo siyo za elimu msingi na
sekondari zinatumia muundo wa kuanzia kwenye 0 badala ya 1.
c) Uwigo wa
jumla wa alama kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita utaendelea kuwa wa alama 0
hadi 100 na kila kundi katika uwigo huu limepewa tafsiri kwa ajili ya kuamua
mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya mwanafunzi kulingana na malengo ya
mtihani husika. Kimsingi, tafsiri zifuatazo zitakatumika
(i) Alama A itakuwa na
maana ya ufaulu uliojipambanua (distincion
or outstanding performance),
(ii) Alama B+ itakuwa na
maana ya ufaulu bora sana (excellent
performance),
(iii) Alama B itakuwa na
maana ya ufaulu mzuri sana ( very good
perfomance),
(iv) Alama C itakuwa na
maana ya ufaulu mzuri (good performance);
(v) Alama D itakuwa na
maana ya ufaulu wa wastani (low
performance),
(vi) Alama E itakuwa na maana ya ufaulu hafifu (very low performance), na
(vii) Alama F itakuwa na
maana ya ufaulu usioridhisha (unsatisfactory
performance).
Wataalamu katika maeneo
mbalimbali ya elimu na ulimwengu wa kazi, kwa kushirikiana na Wizara, watatoa
maana ya tafsiri hizi kiutendaji katika maeneo yao kulingana pia na mahitaji
yao.
d) Alama C iwe ndiyo alama ya ufaulu mzuri ambao hauhitaji urekebu wa lazima,
wakati alama D na E ni alama za ufaulu unaohitaji urekebu kadri mwanafunzi atakavyokuwa
anaendelea na masomo ili kuthibitisha kama mlengwa anaweza na kulingana na
mahitaji ya eneo husika (targeted
remediation). Alama F iwe alama
ya eneo linalohitaji urekebu wa hali ya juu (intesive remediation) ili mwanafunzi huyo aweze kumudu masomo kadri
anavyoendelea kukua kielimu ama atakapoingia katika ulimwengu wa kazi.
e) Makundi ya
alama yatajumuisha CA kwa kiwango cha asilimia
isiyozidi 40 na mtihani wa mwisho kwa asilimia isiyozidi 60 kwa makundi yote ya
watahiniwa ikiwemo wale wa kujitegemea (private
candidates). Hii ni kwa kuzingatia kwamba CA siyo vizuri
izidi uwigo wa alama ya ufaulu mzuri unapoanzia ambayo ni C au 40.
f) CA kwa upande wa Kidato cha Nne zitokane na mtihani wa
Kidato cha Pili (alama 15), matokeo ya Kidato
cha Tatu (alama 5 kwa kila muhula, na hivyo jumla ya alama 10), mtihani
wa Mock (alama 10) na kazi mradi au Projects (alama 5). Kwa upande wa Kidato
cha Sita, CA iendelee kutokana na muundo unaotumika sasa.
g) CA zitumike pia kwa watahiniwa wa kujitegemea. Kwa
upande wa watahiniwa wa kujitegmea ambao wanarudia Mitihani, CA zao zitumike
zile zilizotumika kutoa matokeo yake ya mitihani ya awali. Kwa watahiniwa wa kujitegemea waliopitia
mfumo wa Qualifying Test (QT), matokeo
ya QT yatumike kama CA na mtihani
wa mwisho uchangie alama 60.
h) Kwa vile
alama endelevu kwa mwaka 2013 kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne tayari
zimeshawasilishwa Baraza la Mitihani
Tanzania, alama hizo zichangie asilimia 40 katika mtihani wa Kidato cha
Nne mwaka 2013.
i)
Muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Points Average ama GPA)
utaandaliwa na kuanza kutumika pale utakapokuwa tayari na wadau wataelimishwa
kuhusu muundo huo ili wapate kuufahamu na manufaa yake katika elimu ya
sekondari.
j)
Muundo huu mpya wa alama utatumika kwa mzunguko wa
miaka minne kabla haujahuishwa tena ili kuupa muda wa kutosha kuona aina ya
changamoto zinazojitokeza na jinsi ya kuzishughulikia. Aina hii ya muda
itaruhusu vidato vinne vya elimu ya sekondari ya kawaida na nane ya elimu ya
sekondari ya juu kupimwa. Hata hivyo, uhusihaji wa masuala ya mitihani unaweza
ukafanyika iwapo matokeo ya uhuishaji wa mitaala kwa ujumla utahitaji pia eneo
la mitihani liguswe na kuhuishwa pia.
Kwa mantiki hii, viwango vya alama na ufaulu ni kama
inavyooneshwa kwenye jedwali la 1 hapa chini:
Jedwali Na 1
MUUNDO WA ALAMA NA UFAULU
ALAMA
|
UWIGO WA ALAMA
|
IDADI YA ALAMA
|
TAFSIRI
|
A
|
75 - 100
|
26
|
Ufaulu
Uliojipambanua
|
B+
|
60 - 74
|
15
|
Ufaulu
bora sana
|
B
|
50- 59
|
10
|
Ufaulu
mzuri sana
|
C
|
40 - 49
|
10
|
Ufaulu
mzuri
|
D
|
30 - 39
|
10
|
Ufaulu
Hafifu
|
E
|
20 - 29
|
10
|
Ufaulu
hafifu sana
|
F
|
0 - 19
|
20
|
Ufaulu
usioridhisha
|
Kwa aina hii ya muundo wa alama, na kwa kuwa muundo
wa GPA utaanza kuandaliwa na wadau kuelimishwa kabla haujaanza kutumika, katika
kipindi hiki mpaka wakati huo, muundo wa madaraja utakuwa kama inavyooneshwa
kwenye jedwali la 2 hapa chini.
Jedwali Na 2
MUUNDO WA MADARAJA
MUUNDO
WA ZAMANI
|
MUUNDO
MPYA
|
MAELEZO
|
||
POINTI
|
DARAJA
|
POINTI
|
DARAJA
|
|
7-17
|
1
|
7-17
|
I
|
Kundi la
ufaulu uliojipambanua na bora sana
|
18-21
|
II
|
18-24
|
II
|
Kundi la
ufaulu mzuri sana
|
22-25
|
III
|
25-31
|
III
|
Kundi la
ufaulu mzuri na wa wastani
|
26-33
|
IV
|
32-47
|
IV
|
Kundi ufaulu hafifu
|
34-35
|
0
|
48-49
|
V
|
Kundi la ufaulu
usioridhisha
|
Wataalamu wa mifumo ya
mitihani watalifanyia kazi zaidi jedwali hili la madaraja ili liweze kutumika
kwa ufanisi katika kipindi hiki cha mpito.
Kwa mantiki hii, Daraja Sifuri linafutwa na kuwekwa daraja
litakalojulikana kama Daraja la Tano na ambalo litakuwa ndilo la mwisho kabisa
katika ufaulu.
HITIMISHO
Mabadiliko haya yamefanyika ili kuendelea kuimarisha
mfumo wetu wa elimu na kuweka wazi taratibu mbalimbali kwa ajili ya mitihani na
masuala mengine. Yako mambo mengi mengine ambayo hayana budi kuendelea
kuimarishwa ikiwemo mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya kujifunzia na
kufundishia pamoja na vitabu na vifaa vingine muhimu katika elimu. Masuala haya
yanaendelea kuangaliwa kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa ama Big Results Now
(BRN). Ushirikiano wa wadau wote ili kuleta tija kwenye elimu ni muhimu sana na
hivyo wizara itaendelea kuwashirikisha wadau wote kwa kadri itakavyohitajika na
wadau pia wanaombwa wasiache kuishirikisha wizara pale watakapokuwa na jambo
lolote ambalo linahitaji ushirikiano ili kwa pamoja tuweze kupata mafanikio
katika sekta ya elimu.
Imetolewa,
KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
0 comments:
Post a Comment