WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Maswali
mengi yanaulizwa kuhusu uraia, hasa wakati huu ambapo zoezi la kuwabaini wageni
wanaoishi nchini kinyume cha sheria linaendelea katika maeneo mbalimbali
nchini, yakitaka kujua nani hasa ni raia wa Tanzania.
Kimsingi,
masuala ya uraia duniani kote yanaongozwa na falsafa kuu mbili ambazo ni Haki
za Kidamu (Jus Sanguinis - The rights of blood), ambapo mtu hupata
uraia kutokana na uhusiano wa kidamu na wazazi wenye uraia wa nchi husika. Hii
ina maana kwamba, pamoja na mtu kuzaliwa katika nchi husika anatakiwa pia kuwa
na mzazi ambaye ni raia wa nchi hiyo. Falsafa hii ndiyo inayofuatwa na nchi ya
Tanzania.
Kwa
maana nyingine kuzaliwa pekee nchini Tanzania hakumpi mtu haki ya moja kwa moja
ya kuwa raia wa Tanzania, bali mtu atakuwa raia ikiwa amezaliwa Tanzania
na wakati wa kuzaliwa kwake mzazi wake mmoja sharti awe ni raia wa Tanzania.
Falsafa
nyingine ni (Jus Soli - The right of Soil), ambayo mtu hupata Uraia
kutokana na kuzaliwa kwake katika ardhi ya nchi fulani. Kufuatana na Falsafa
hii, mtu hupata uraia kutokana na kuzaliwa katika nchi husika bila kujali uraia
wa wazazi wake.
URAIA
WA TANZANIA
Masuala
ya uraia nchini Tanzania yanasimamiwa na Sheria ya Uraia ya Tanzania ya mwaka
1995 Sura 357 kama ilivyorejewa mwaka 2002, pamoja na kanuni zake za mwaka
1997. Sheria hii imeanisha aina tatu za uraia wa Tanzania ambazo ni;
1.
Uraia wa Tanzania kwa kuzaliwa
2.
Uraia wa Tanzania kwa kurithi
3.
Uraia wa Tanzania kwa Tajnisi, au kujiandikisha.
Uraia wa Tanzania wa kuzaliwa:
Utambuzi
wa nani ni raia wa Tanzania unazingatia vipindi mbalimbali vya historia ya
Tanzania, yaani kabla na baada ya uhuru wa Tanganyika, kabla na baada ya
Mapinduzi ya Zanzibar na baada ya Muungano wa Tanzania. Pia, mahali alipozaliwa
na alizaliwa na nani kama inavyoainishwa hapa chini:
Mtu aliyezaliwa
Tanganyika kabla ya Uhuru alitambulika kuwa ni raia wa Tanganyika wa kuzaliwa,
ikiwa mmoja wa wazazi wake alizaliwa Tanganyika na anatokana na Raia wa
Uingereza,makoloni yake au nchi zilizokuwa chini ya udhamini wa Uingereza
Mtu
aliyezaliwa Tanganyika baada ya Uhuru alitambulika kuwa ni raia wa
Tanganyika wa kuzaliwa, ikiwa mmoja wa wazazi wake alikuwa raia wa Tanganyika.
Mtu
aliyezaliwa Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi alitambulika kuwa ni raia wa
Zanzibar wa kuzaliwa.
Ila,
mtu huyo hakutambulika kuwa ni raia wa zanzibar ikiwa wazazi wake
walitokana na mataifa yafuatayo; Australia, Ubeligiji, Kanada, Ceylon (Sri
Lanka), Ufaransa, Italia, New Zealand, Ureno, Jamhuri ya Ireland, Afrika Kusini
na Marekani.
Aliyezaliwa
Tanzania siku na baada ya Muungano wa Tanzania
Mtu
aliyezaliwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku na baada ya Muungano,
atatambulika kuwa ni raia wa Tanzania wa kuzaliwa ikiwa mmoja wa wazazi wake ni
raia wa Tanzania.
Mtu
hawezi kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa kama wakati wa kuzaliwa kwake hapa
nchini, wazazi wake wote hawakuwa raia wa Tanzania; au Baba yake ni Balozi wa
nchi ya kigeni na ana kinga ya kibalozi; au mmoja wa mzazi wake alikuwa ni adui
wa nchi ya Tanzania (enemy) na mtoto huyo alizaliwa katika eneo lililokuwa
likikaliwa na adui.
Sheria
ya Uraia ya Tanzania Sura 357 ya mwaka 1995 (R.E, 2002) ndiyo sheria pekee
inayotambua sheria zote za nyuma, zilizokuwa zinasimamia masuala yote ya uraia
katika vipindi mbalimbali vya historia ya Tanzania.
Kwa
mantiki hiyo mtu yeyote ambaye alikuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa
kuzaliwa, kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 25/04/1964,
ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzaliwa,
mara baada Muungano.
Aidha,
mtu yeyote kama hakutambulika kuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kabla ya
Muungano, hatatambulika kuwa ni raia wa Tanzania mara baada ya muungano.
URAIA WA TANZANIA KWA KURITHI:
Raia
wa Tanzania kwa kurithi ni mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania, na anatambuliwa
kuwa raia wa Tanzania kutegemeana na kipindi alichozaliwa na uraia wa wazazi
wake wakati wa kuzaliwa kwake kama ifuatavyo:
Mtu
aliyezaliwa nje ya Tanganyika kabla ya uhuru (akiwa ametokana na raia wa
Uingereza na Makoloni yake au himaya ya Mwingereza) alitambuliwa kuwa ni
raia wa Tanganyika kwa kurithi endapo baba yake alikuwa raia wa Tanganyika.
Mtu
aliyezaliwa nje ya Tanganyika baada ya Uhuru na kabla ya Muungano alitambuliwa
kuwa ni raia wa Tanganyika kwa kurithi, ikiwa baba yake alikuwa raia wa
Tanganyika.
Sheria
ya Uraia ya Tanganyika ya mwaka 1961 haikutoa fursa kwa mama kumrithisha uraia
mtoto wake aliyezaliwa nje ya nchi. Hivyo mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika
katika vipindi tajwa hapo juu hakutambulika kuwa ni raia wa Tanganyika kwa
kurithi kupitia mama yake.
Aidha,
mtu aliyezaliwa nje ya Tanganyika hakutambuliwa kuwa raia wa Tanganyika kwa
kurithi iwapo baba yake alikuwa raia wa Tanganyika kwa kurithi. Kwa tafsiri
rahisi ni kwamba Raia wa kurithi hawezi kurithisha tena uraia huo kwa mtoto
wake aliyezaliwa nje ya Tanganyika.
Mtu
aliyezaliwa nje ya Zanzibar kabla ya Muungano atakuwa raia wa Zanzibar kwa
kurithi endapo baba yake ni raia wa Zanzibar.
Vile
vile, Sheria ya Uraia ya Zanzibar (The Zanzibar Nationality Decree, CAP
39, 1952)haikuruhusu mama raia wa Zanzibar kurithisha uraia kwa mtoto wake
aliyezaliwa nje ya Zanzibar. Kwa maana nyingine, mtu aliyezaliwa nje ya
Zanzibar katika kipindi hicho hakutambuliwa kuwa ni raia wa Zanzibar kwa
kurithi kupitia kwa mama yake.
Ieleweke
pia kuwa mtu aliyezaliwa nje ya Zanzibar hakutambuliwa kuwa raia wa Zanzibar
kwa kurithi ikiwa Baba yake alikuwa raia wa Zanzibar kwa kurithi. Kwa tafsiri
rahisi ni kwamba Raia wa Zanzibar kwa kurithi hawezi kurithisha tena uraia huo
kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Zanzibar.
Mtu
aliyezaliwa nje ya Tanzania siku na baada ya Muungano atakuwa raia wa Tanzania
kwa kurithi endapo mzazi wake mmoja ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa au
kuandikishwa/tajnisi.
Ni
vyema ieleweke kuwa mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania hawezi kuwa raia wa
Tanzania kwa kurithi iwapo baba/mama yake ni raia wa Tanzania kwa kurithi.
Sheria
ya Uraia Sura ya 357 ya mwaka 1995 (R.E, 2002) imetoa fursa kwa mama
ambaye ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa, tajnisi/kuandikishwa kurithisha uraia
wa Tanzania kwa mtoto wake aliyezaliwa nje ya Tanzania.
Aidha,
mtu yeyote ambaye alikuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa kurithi, kabla ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 25/04/1964 ataendelea kuwa raia wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ile ile mara baada Muungano.
Mtu
yeyote kama hakutambulika kuwa raia wa Zanzibar au Tanganyika kwa kurithi kabla
ya Muungano, hatatambulika kuwa raia wa Tanzania kwa kurithi mara baada ya
muungano.
Haya
yameainishwa katika Sheria ya Uraia ya Tanzania Na.6, 1995 (Sura 357, Rejeo la
2002) kifungu cha 30.
URAIA WA TANZANIA KWA TAJNISI
(NATURALIZATION)
Mtu
yoyote ambae siyo raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzaliwa au
kurithi anaweza kuomba uraia wa Tanzania wa tajnisi kwa mujibu wa Sheria ya
Uraia Sura 357 ya mwaka 1995, (R.E,2002).
Kwa mujibu
wa sheria hiyo, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala ya uraia
nchini (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya
kumpa au kutompa uraia wa Tanzania Mgeni mwenye sifa anayeomba uraia.
Sifa za Kuomba Uraia wa Tajnisi;
Mgeni
anaetaka kuomba uraia wa Tanzania anapaswa kuwa na sifa zifuatazo:
(i)
Mwombaji awe na umri kuanzia miaka 18 na uwezo wa kufanya maamuzi
yanayokubalika kwa mujibu wa sheria za nchi,
(ii)
Awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wa miezi 12
mfululizo kabda ya kutuma maombi ya Uraia,
(iii)
Katika muda wa miaka kumi kabla ya miezi kumi na mbili hiyo awe ameishi ndani
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kihalali kwa muda usiopungua miaka saba.
(iv)
Awe anafahamu vizuri lugha ya Kiswahili au Kiingereza,
(v)
Awe na tabia njema,
(vi)
Awe na manufaa kwa taifa, yaani awe alichangia na anaendelea kuchangia katika
ukuzaji wa uchumi, sayansi na teknolojia na utamaduni wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na
(vii)
Awe anakusudia kuishi moja kwa moja ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ikiwa ombi lake la uraia litakubaliwa.
Mgeni
yeyote mwenye nia ya kuomba uraia wa tajnisi mwenye umri wa miaka 18 na
kuendelea anatakiwa kufuata taratibu zifuatazo;
(i)
Mwombaji anatakiwa kujaza fomu za maombi ya uraia ambazo zinapatikana katika
ofisi zote za Uhamiaji za Wilaya, Mikoa, Afisi kuu ya Uhamiaji Zanzibar na
Makao Makuu ya Uhamiaji Dar es Salaam.
(ii)
Mwombaji anatakiwa kutoa matangazo ya nia yake ya kuomba Uraia wa Tanzania mara
mbili mfululizo kwenye magazeti yaliyosajiliwa Tanzania.
Mchakato
wa Kushughulikia Maombi ya Uraia
Ili
kuhakikisha kuwa wageni wanaopewa uraia ni wale wenye manufaa kwa Taifa, maombi
yote yanapaswa kupitia na kujadiliwa katika vikao vya Kamati za Ulinzi na
Usalama za:
Ngazi
ya Kata au Shehia (kwa upande wa Zanzibar)
Katika
ngazi ya Kata au Shehia anayoishi mwombaji, ambapo atahojiwa na maombi yake
kujadiliwa na kikao hicho na hatimaye ombi lake kupelekwa ofisi ya Uhamiaji
Wilaya kwa hatua zaidi.
Katika
ngazi hii, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya itajadili maombi ya uraia
yaliyowasilishwa kutoka ngazi ya Kata au Shehia, hatimaye maoni na mapendekezo
yake hupelekwa katika ngazi ya mkoa.
Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nayo itajadili maombi yaliyowasilishwa na kutoa
maoni na mapendekezo yake kuhusiana na ombi husika na hatimaye hutumwa kwa
Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, ambaye atatoa ushauri na mapendekezo yake kwa Mhe.
Waziri mwenye dhamana ya masuala ya uraia wa Tanzania kwa maamuzi.
Ombi
la Uraia wa Tajnisi kwa Mwanamke aliyeolewa.
Mwanamke
mgeni ambaye ameolewa na raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wowote
wa uhai wa ndoa yake, anaweza kuwasilisha maombi ya uraia wa Tanzania kwa
tajnisi.
Ombi
la uraia kwa mwanamke aliyeolewa linatakiwa kuwasilishwa pamoja na
viambatanisho vifuatavyo;
(i)Cheti
cha ndoa kilichosajiliwa na Mamlaka husika nchini
(ii)
Pasipoti ya taifa lake ambayo haijaisha muda wake
(iii)
Kibali cha kuishi nchini ambacho hakijaisha muda wake (Hati ya Mfuasi)
(iv)
Vielelezo vinavyothibitisha kuwa mume wake ni raia wa Tanzania.
Ombi
la Uraia wa Tajnisi kwa Mtoto
Sheria
ya Uraia ya mwaka 1995 Sura 357 (RE 2002), inatoa fursa kwa mzazi au mlezi
halali wa mtoto (asiye raia) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kumuombea
mtoto huyo Uraia wa Tanzania. Baada ya maombi rasmi kuwasilishwa, Waziri mwenye
dhamana ya uraia anaweza kuruhusu mtoto huyo aweze kupata uraia wa tajnisi.
Waziri
mwenye dhamana na masuala ya uraia nchini (Waziri wa Mambo ya Ndani) ndiye
mwenye Mamlaka ya mwisho ya kutoa au kutotoa uraia wa Tanzania kwa mwombaji
yoyote kwa mujibu wa Sheria ya Uraia ya mwaka 1995 Sura 357, rejeo la 2002.
Makala hii imeandaliwa na
Timu ya Habari ya Operesheni Kimbunga -
Oktoba, 2013
0 comments:
Post a Comment