
Kaimu Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Bw. Mbaraka Batega(kushoto)
akieleza kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu udhibiti wa wahamiaji
haramu kwenye maeneo yaliyopo nje ya mikoa ya “operesheni kimbunga”,wakati wa
mkutano uliofanyika katika ukumbi wa idara ya Habari(MAELEZO) Leo Jijini Dar es
Salaam.Kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Frank Mvungi.Picha Na Eliphace Marwa
---
JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
IDARA
YA UHAMIAJI

Idara ya Uhamiaji ni moja ya Vyombo vya
Ulinzi na Usalama vyenye jukumu la kuhakikisha kwamba Ulinzi na Usalama wa nchi
unaimarishwa. Katika kusimamia jukumu hilo kikamilifu, Idara ya Uhamiaji
inatekeleza majukumu makuu ya Msingi yafuatayo:
i.
Kuwezesha na kudhibiti uingiaji na utokaji
wa watu nchini
ii.
Kutoa huduma ya pasipoti au hati nyingine
za safari kwa Watanzania wanaosafiri nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali.
iii.
Kutoa huduma ya Vibali vya kuishi nchini pamoja
na Pasi mbalimbali kwa wageni wanaokuja nchini kwa shughuli mbalimbali.
iv.
Kufanya misako, doria, kubaini na
kuwakamata wahamiaji haramu nchini na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria
zilizopo.
v.
Kuratibu mchakato wa maombi ya wageni
wanaoomba uraia wa Tanzania na kumshauri ipasavyo Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi kwa hatua ya uamuzi.
Majukumu hayo ndiyo yanaipatia Idara ya
uhamiaji wajibu wa kulinda na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi, sambamba na
Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.
Uwezeshaji
na Udhibiti wa wahamiaji nchini
Tanzania ni nchi inayofahamika sana
duniani kwa ukarimu wa watu wake, ardhi yenye rutuba, rasilimali mbalimbali na vivutio
vingi vya aina yake kwa watalii. Tanzania pia kutokana na historia yake ya
amani na utulivu pamoja na imani ya viongozi wake kuwa binadamu wote ni sawa na
Afrika ni moja, Tanzania imekuwa ni kimbilio salama la wakimbizi wengi na
wapigania uhuru kutoka mataifa mbalimbali Barani Africa.
Tanzania pia inazidi kuwa kivutio kwa
wageni wengi kutokana na kuwa na fursa nyingi za uwekezaji katika sekta
mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, madini, utalii n.k. Hata hivyo, si wageni
wote wanaoingia nchini wanafuata taratibu za kiuhamiaji katika kipindi chote
cha kuwepo hapa nchini. Hivyo, Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani
inakabiliwa na changamoto ya kuwepo wahamiaji haramu.
Wahamiaji haramu hao wanatokana na makundi
makuu yafuatayo:
Wahamiaji
haramu walioingia nchini kabla ya uhuru pamoja na vizazi vyao.
Wengi walikuja kama manamba katika mashamba ya
wakoloni. Ingawa wengi wao wamefariki, lakini vizazi vyao bado vipo. Wahamiaji
haramu wa aina hii wengi wanapatikana katika mikoa mingi ya mpakani, Tanga,
Pwani na Morogoro. Hawa kwa mujibu wa historia yao ni miongoni mwa wahamiaji
“walowezi” hapa nchini. Kazi kubwa inayofanywa na Idara ya Uhamiaji ni
kuwatambua, kuwaandikisha na baadae kuishauri Serikali ipasavyo kuhusu hatua za
kuchukua.
Wahamiaji
haramu wanaotokana na kuwepo kwa makambi ya wakimbizi na wapigania uhuru
nchini.
Baada ya nchi nyingi kupata uhuru,
wapigania uhuru wengi waliondoka, lakini baadhi vizazi vyao bado vipo hapa
nchini na baadhi ya vizazi hivyo vinaishi isivyo halali nchini.
Aidha, wengine ni wale walioishi
nchini kama wakimbizi na baadae kutorejea nchini kwao pamoja na vizazi vyao.
Wengi wa wahamiaji haramu hao wapo katika Mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora,
Rukwa, Mtwara Ruvuma, Morogoro.
Katika kuwashughulikia Wahamiaji haramu wa
aina hii, Idara imeweka utaratibu wa kuwatambua kwa kuwaandikisha katika
madaftari maalum ili kuwa na kumbu kumbu zao sahihi na baadae kuishauri
Serikali kuhusu hatua za kuchukua. Madaftari haya yameisaidia Serikali
kuwatambua Wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kagera na Kigoma wakati wa
Operesheni “Kimbunga” inayoendelea hadi sasa.
Wahamiaji
wanaozidisha muda wa ruhusa ya kuwepo nchini.
Hawa ni Wahamiaji wanaoingia nchini
kihalali na kupewa muda maalum wa kuwepo nchini. Baadhi yao muda huo unapokwisha
hawaondoki, wanaendelea kuishi kwa kujificha na kuukimbia mkono wa sheria.
Wahamiaji haramu wa aina hii wanashughulikiwa kwa kukamatwa na kuchukuliwa
hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani na kuwaondoa
nchini.
Wahamiaji
haramu wanaoingia nchini kinyume cha sheria.
Hawa ni wale ambao wanaingia nchini bila
kufuata taratibu zozote za Uhamiaji. Wengi wao wanatumia njia zisizohalali
wakati wa kuingia nchini. Kundi hili linahusisha Wahamiaji haramu wengi waliopo
katika maeneo ya mipaka yetu na nchi jirani pamoja na makundi ya Wahamiaji
haramu wanaoingia nchini kutoka nchi za Pembe ya Afrika (Somalia na
Ethiopia).
Wahamiaji haramu wa aina hii wanashughulikiwa
kwa kuwasaka, kuwakamata na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni
pamoja na kuwafikisha mahakamani na kuwaondoa nchini.
Udhibiti
wa Wahamiaji haramu katika maeneo yaliyopo nje ya Mikoa ya “Operesheni
Kimbunga”
Wakati wa utekelezaji wa agizo la Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete la kuwataka
majambazi, majangili na wamiliki wa silaha kinyume cha sheria kujisalimsha na
Wahamiaji haramu walipo katika Mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita kurudi nchini
kwao kwa hiari, Idara ya Uhamiaji iliendelea na shughuli za udhibiti wa wageni katika
kipindi hicho kwenye Mikoa iliyopo nje ya eneo la operesheni. Katika shughuli
hizo za udhibiti wa wageni, Jumla ya wahamiaji haramu 6,653 kutoka mataifa mbalimbali wamekamatwa na kuchukuliwa hatua
mbali kwa mujibu wa sheria. Mataifa ya Wahamiaji hao haramu na idadi yao kwenye
mabano ni kama ifuatavyo:- Malawi (3,778), Burundi (696), Congo DRC (1,739),
Kenya (147), Uganda (20), Pakistan (12), Somalia (31), Nigeria (23) na Msumbiji
(20). Wengine ni India (16), China (09), Rwanda (40), Ethiopia (97), Komoro
(10), Uturuki (03), Afrika Kusini (02), Bukina Faso (01), Liberia (02), Italia
(01), Singapore (01), Libya (01), Bulgaria (01), Ghana (02) na Syria (01).
Wengi wa Wahamiaji haramu hao wameondolewa
nchini, wengine wamefikishwa mahakamani wakati wengine uchunguzi dhidi yao bado
unaendelea. Aidha, wapo walio halalisha ukaazi wao nchini wakati wengine
wameorodheshwa kwa ajili ya hatua zaidi.
Watanzania
Wahamiaji haramu katika nchi nyingine.
Wakati Tanzania ikiendelea na udhibiti wa
Wahamiaji haramu nchini, takwimu zilizopo zonaonesha kwamba wapo watanzania
ambao nao wanakiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi mbalimbali wanazokwenda,
ikiwemo kuingia na kuishi katika nchi hizo wakiwa Wahamiaji haramu.
Katika kipindi cha mwaka 2012, Jumla ya
watanzania 1,263 walirejeshwa nchini kutoka mataifa mbalimbali. Aidha, katika
kipindi cha Januari-August, 2013 jumla ya watanzania 715 wamerejeshwa nchini
kwa makosa ya kukiuka taratibu za Uhamiaji katika nchi walizokwenda, hususan
Afrika Kusini.
Kwa kuwa sasa tunaishi katika ulimwengu
ambao watu wanasafiri kutoka nchi moja hadi nyingine kuliko kipindi chochote
kile katika historia ya binadamu, tunapenda watanzania nao wasafiri nje ya nchi
kwa ajili ya kunufaika na fursa mbalimbali na tumekuwa tukiwawezesha kufanya
hivyo. Pamoja na nia hiyo njema ya Serikali, tunatoa wito kwa watanzania
wenzetu kuheshimu Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo katika nchi wanazo
kwenda, kama ambavyo tunapenda wageni nao waheshimu Sheria, Kanuni na Taratibu
zilizopo hapa nchini. Kufanya hivyo sio tu kwamba kutatujengea uaminifu na
uadhilifu katika jamii ya watu tunaoishi nao ugenini, bali pia kutajenga jina
zuri na heshma kwa nchi yetu miongoni mwa mataifa mengine.
Sote tufahamu kuwa hakuna nchi yoyote
duniani inayoweza kuvumilia Wahamiaji haramu, bila kujali wanatoka taifa gani.
Kila nchi inajitahidi kukabiliana na changamoto hii ya Wahamiaji haramu.
Tofauti ni mbinu zinazotumika kulingana na mazingira na uwezo wa nchi husika.
Ndio maana kwa mazingira ya jiografia ya nchi yetu, mapambano dhidi ya
Wahamiaji haramu ni endelevu bila kujali kama kuna operesheni maalum au ni
katika hali ya utendaji kazi wa kawaida.
Hitimisho:
Suala la ulinzi na usalama wa nchi yetu ni
la kila mwananchi. Vyombo vya Ulinzi na Usalama peke yake haviwezi kutekeleza
jukumu hili bila ushirikiano wa karibu na wananchi. Wahamiaji haramu hawana
kisiwa chao wenyewe, bali wanaishi ndani ya jamii. Tunawashukuru wote waliotupatia ushirikiano
katika kutekeleza majukumu yetu na tunaomba tuendelee kushirikiana kuanzia
mwananchi mmoja mmoja, viongozi wa ngazi mbalimbali, wanahabari pamoja na
vikundi mbalimbali vya kijamii.
0 comments:
Post a Comment