Home » » Mabadiliko ya leseni kuikosesha serikali mapato

Mabadiliko ya leseni kuikosesha serikali mapato

Mfumo mpya unaotaka wafanyabiashara wote kuomba upya leseni za biashara na kulipa ada kila mwaka, hautasaidia kukua kwa sekta ya biashara nchini, wadau mbalimbali katika sekta hiyo wamebainisha.
Wadau hao wamesema mabadiliko hayo, yatasababisha wafanyabiashara wadogo kutoweka wazi biashara zao na kuzuia ajira na ukuaji wa sekta hiyo.
Wadau hao wamesema kutokana na uamuzi huo, Serikali itakosa mapato, kwani wafanyabiashara wengi wataamua kutojisajili na hivyo mzigo wa kulipa kodi kubaki kwa wafanyabiashara wachache.
Wizara ya Viwanda na Biashara imesema hivi karibuni kwamba utoaji wa leseni bila kulipia ada umefutwa tangu Juni 30, mwaka huu.
Wadau wamesema kwamba kwa mfumo huo mpya, nchi itakuwa na ushindani dhaifu wa biashara na itakuwa inafanywa katika mazingira yasiyosawihi kibiashara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wasindika Maziwa nchini, Edmund Mariki anasema Serikali imekurupuka katika uamuzi wake huo.
Anasema Serikali hivi sasa ilipaswa kuboresha mazingira ya biashara badala ya kuchukua uamuzi huo ambao unasababisha kikwazo kwenye ukuaji wa biashara.
Anasema kwa kuondoa au kupunguza vikwazo visivyo muhimu katika uendeshaji wa biashara utasaidia kushawishi wafanyabiashara wengi kuorodhesha biashara zao serikalini na kuongeza ukusanyaji wa kodi na kutengeneza nafasi nyingi za ajira.
“Hii inasikitisha sana, tumekuwa tukishawishi mazingira bora ya kufanya biashara, lakini serikali inarejea katika utamaduni wa zamani ambao unakwamisha kukua kwa sekta ya biashara,” anaeleza Mariki.
Anaeleza kuwa hana shaka na juhudi za Serikali za kutanua wigo wa ukusanyaji kodi, lakini anafikiri kwamba kama Serikali ikitoa leseni za biashara bure zitashawishi wafanyabiashara wengi kujiunga na kuongeza ukusanyaji kodi.
Kwa mujibu wa Mariki, asilimia 3 tu za biashara katika sekta ya maziwa, wajasiriamali wake wana leseni na hivyo kutambulika rasmi.
“Badala ya kuhakikisha kwamba asilimia 97 zilizobaki zinaomba leseni, serikali inachukua hatua ambayo itawakimbiza wengine kujiorodhesha ili kuchukua leseni, hali hii itasababisha wengine waendelee kufanya biashara bila kujisajili.

CHANZO;MWANANCHI

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa