Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akizungumzia ushiriki wa Tanzania katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa popote pale duniani.
Waziri
Membe akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mahojiano na mwandishi
Fredy Mwanjala (kushoto) na mpiga picha Bi. Fauzia Yusuph (kulia), wote
wanatoka Kituo cha Televisheni cha Channel Ten.
Na TAGIE DAISY MWAKAWAGO
Tanzania itaendelea kushiriki operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa popote pale duniani.
Msimamo
huo wa Tanzania uliwekwa wazi na Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika mahojiano maalum na
Mwandishi Fredy Mwanjala wa Kituo cha Televisheni cha Channel
Ten, yaliyofanyika leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Katika
mazungumzo yao yaliyolenga kutaka kufahamu msimamo wa Tanzania kufuatia
vifo vya askari wake huko Darfur, Sudan na hivi karibuni huko Mashariki
mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC), Waziri Membe
alisema moja ya sera ya mambo ya nje katika awamu ya nne na Mhe. Rais
Kikwete ni ulinzi na amani.
Hivyo,
Tanzania itaendelea kushiriki katika operesheni hizo za kulinda amani
ambazo zimeiletea Tanzania heshima kubwa katika medani ya kimataifa.
Waziri
Membe alisema inawezekana kuwa wanajeshi wa Tanzania wanalengwa na
kundi la waasi la M23, kwa kuwa Tanzania ni mwiba mkali kwa kikundi
hicho kutokana na umahiri wake unaofahamika vyema katika nchi za Maziwa
Makuu.
“Umwagikaji
wa damu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC) ni
chachu kwa Watanzania dhidi ya kikundi cha waasi cha M23,” alisema Mhe.
Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Hivi
karibuni mwezi Agosti, kikosi cha M23 kilishambuliwa na kuteketezwa kwa
mujibu wa taarifa za kiitelijensia zilizoripotiwa na vyombo vya habari.
Lakini inasemekana kuwa kuna kundi lingine limezuka tena hivi karibuni
kwa jina hilo hilo la M23 kama vile chem-chem ya maji, alieleza Waziri
Membe.
“Ni
muhimu ieleweke kuwa Tanzania haitosita kamwe kuendelea kuwa mstari wa
mbele katika kupambana na hizi vita za nchi jirani zisizoisha,” alisema
Waziri Membe. Aliongeza na kusema kuwa Tanzania imekuwa kinara cha
medali za kimataifa katika kutetea na kulinda amani na usalama wa nchi
yetu.
“Sisi
ni taifa ambalo liko tayari kujitolea kupigana na kumwaga damu katika
kutetea amani na kutatua migogoro ya majirani zetu,” alisema Waziri
Membe. Alieza kuwa Tanzania imeshiriki kwa namna moja au nyingine
katika vita vya ukombozi wa amani barani Afrika katika nchi za Msumbiji,
Afrika Kusini, Zimbabwe, Comoro, Uganda, Mashariki ya Kongo-DRC na nchi
nyingine nyingi.
Akizungumzia
kupoteza maisha kwa askari wa Tanzania nchini Kongo-DRC, Waziri Membe
amesema kuwa ni msiba mkubwa wa kitaifa na wa Umoja wa Mataifa.
Alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea
salamu za rambirambi kutoka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Umoja
wa Ulaya (EU), Serikali ya Kongo, Serikali ya Angola, Serikali ya Afrika
ya Kusini na nchi nyingine duniani.
Tanzania
ni mojawapo ya nchi zinazounda Brigedi Maalum ya umoja wa mataifa
(MONUSCO) kulinda na kusimamia amani huko Mashariki ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC). Kuna batalioni moja yenye askari
zaidi ya 1,270 ambao wanaunda sehemu ya Brigedi hiyo Maalum ya MONUSCO.
MICHUZI BLOG
0 comments:
Post a Comment