Dar es Salaam.Taasisi
za Fedha nchini zimepoteza kiasi cha Sh34.4 bilioni kuanzia kipindi cha
Oktoba mwaka jana hadi Oktoba mwaka huu kutokana na wizi wa fedha
katika taasisi hizo,ripoti mpya imebainisha.
Utafiti huo uliofanyika katika nchi za Kenya,Tanzania na Uganda
umebainisha kuwa,Taasisi za Fedha za Afrika Mashariki zimepoteza zaidi
ya Sh471 bilioni sawa na (USD 30 milioni) kwa mwaka.
Hata hivyo benki hizo ziliweka wazi upotevu wa Sh126.9 bilioni tu ambao
ni robo ya upotevu huo wa zaidi ya Sh471 bilioni kwa kile kinachodaiwa
kuhofia kupoteza wateja.
“Taasisi za fedha zinapoteza fedha nyingi kutokana na teknolojia na
watendaji wa ngazi za juu kuhusika kwa kiwango kikubwa lakini hazitaki
kukiri kwa sababu ya kuhofia kukosa wateja,” alisema Robert Nyamu,
Mkurugenzi wa Delloite, Afrika Mashariki.
Msemaji wa Benki Kuu ya Tanzania,Loy Nabeta hakuwa tayari kuzungumzia
upotevu huo na kusema kuwa ni suala linalohitaji majadiliano ya kina na
utendaji wa ngazi za juu.
Wimbi la wizi wa fedha katika benki lilianza kupata umaarufu mwaka 2010
na Oktoba 2012 hadi Februari 2013, inakadiriwa kuwa jumla ya Sh700
milioni zimeibwa katika benki mbalimbali kwa nyakati tofauti.
Ripoti hiyo ya Uhalifu wa Kiuchumi ya mwaka 2013 iliyotolewa na Kampuni
ya Uchunguzi wa Huduma ya Delloite imebaini kuwa watendaji wa ngazi za
juu wanahusika zaidi na uhalifu huo ukilinganisha na watendaji wa ngazi
za chini.
“Wanapofanya uhalifu hujua namna ya kuuficha na kuujadili na wasimamizi
wa ndani bila kubainika.Wanajua mbinu na mifumo yote ya kifedha na
wanatumia fursa hiyo kuiba,” alisema Nyamu.
Watendaji waliotajwa kuhusika zaidi na wizi huo wa fedha ni wale wa
ngazi za juu wakiwamo wakurugenzi watendaji, ofisa operesheni,
wakurugenzi wa fedha, vitengo vya teknolojia na wakuu wa vitengo
wanatumia nafasi zao kufanya uhalifu wa fedha ukilinganisha na
wafanyakazi wa kati na ngazi za chini.
Wizi unaofanyika zaidi katika nchi za Afrika Mashariki unatajwa kuwa ni
wa fedha halali ambao ni zaidi ya asilimia 70 ya uhalifu wa aina zote wa
kifedha.
Hata hivyo Nyamu alisema watendaji wa ngazi za chini wanaweza kufanya
uhalifu wa kiasi kikubwa cha fedha iwapo wanajua namna ya kufanya hivyo.
Mtaalamu wa Uchumi na Mhadhiri wa Chuo cha usimamizi wa Fedha(IFM), Dk
Eliamani Sedoyeka alisema ni kweli kuwa watu wa ngazi za juu wanatumia
nafasi zao kufanya uhalifu wa kifedha kwa sababu wanaelewa kwa undani
mfumo unavyofanya kazi na kutolea mfano i wizi wa Benki ya Stanbic .
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment