Home » » Tido Mhando ajitosa Uhuru Marathon

Tido Mhando ajitosa Uhuru Marathon



USAJILI wa mbio za Uhuru Marathon ulioanza kwa kishindo wiki iliyopita pale Spika wa Bunge, Anne Makinda alipowaongoza wabunge kufanya hivyo, unazidi kushika kasi huku Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Tido Mhando, naye akiahidi kujitosa leo ili aweze kushiriki.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Katibu wa Kamati ya Uhuru Marathon, Innocent Melleck, alisema Mhando anatarajiwa kujisajili kushiriki mbio hizo, baada ya kuvutiwa na lengo lake ambalo ni kuimarisha amani, umoja na mshikamano.
Melleck hakutaka kufafanua Mhando anataka kushiriki mbio za kilomita ngapi, ingawa alisema fomu zitatolewa kwa sh 100,000 kwa wale watakaokimbia mbio za kilomita tatu, sh 2,000 kilomita tano, sh 6,000 kwa atakayeshiriki moja kati ya mbio za kilomita 21 na 42.
“Hizi mbio ni muhimu zaidi kwa ajili ya taifa letu, hivyo ni vyema kwa Watanzania wote wakashiriki ili kuipigania amani iliyopo nchini mwetu na ndiyo maana hata Rais Jakaya Kikwete, pia atashiriki. “Kesho (leo), Tido anatarajiwa pia kujisajili kwa ajili ya kushiriki mbio hizo, lengo kubwa ikiwa pia kushawishi Watanzania wengine waweze kushiriki,” alisema.
Mratibu huyo aliongeza kuwa mbio za kilomita 3 zitakuwa maalumu kwa ajili ya viongozi wa kada mbalimbali, wakiwemo pia wale wa dini na zile za kilomita 5 pia zitakuwa za kuchangia kwa ajili ya watu wa mahitaji maalumu.
Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Desemba 8 na zitaanzia na kuishia viwanja vya Leaders, Kinondoni.

Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa