Home » » JWTZ waanza kuwajengea makazi waathirika mafuriko

JWTZ waanza kuwajengea makazi waathirika mafuriko

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono Auction Mart & Co Ltd, Scholastika Kavela (kushoto), akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Elias Tarimo misaada kwa ajili ya waathirika wa mafuriko wa vijiji vya Magole na Mateteni. 
 
Kikosi  cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam,  kimepiga  kambi katika vijiji vya Magole na Mateteni  vya wilayani hapa Mkoa wa Morogoro, vilivyokumbwa na mafuriko wiki mbili zilizopita kwa ajili ya kuanza ujenzi wa makazi ya muda kwa waathirika wa mafuriko hayo.
Akizungumza wakati wa kupokea misaada ya vyakula kutoka Kampuni ya Yono Auction Mart & Co Ltd , Mkuu Wilaya ya Kilosa, Alias Talimo,  alisema kikosi hicho kina zaidi ya askari 60 na  kwamba kimeanza kazi hiyo ya ujenzi.

Talimo alisema kazi ya kwanza iliyofanywa na kikosi hicho ni kupitia maeneo yote yaliyopata athari na kuweka mipango ya ujenzi wa maeneo ya makazi ya muda.

Alisema makazi hayo yatajengwa kwa kutumia mabati ambayo yaliahidiwa kutolewa na Serikali kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete alipokwenda kuwafariji na kuwapa pole wathirika hao.

Hata hivyo, aliishukuru Yono Auction Mart & Co Ltd kwa kutoa msaada huo wa vyakula,sabuni na mafuta na kuzitaka kampuni nyingine kuiga mfano huo kwa kuwa bado kuna mahitaji ya vyakula.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Scholastika Kavela, alisema wametoa msaada huo baada ya kuguswa na athari walizopata wakazi wa vijiji hivyo.

Aliwataka wadau wengine kuangalia namna ya kuwasaidia waathirika hao kwa kuwa misaada bado inahitajika .
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa