Home »
» Kibanda, Makunga hukumu yao leo
Kibanda, Makunga hukumu yao leo
MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya
uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari,
Absalom Kibanda na wenzake wawili.
Hukumu hiyo itatolewa na Hakimu
Mkazi, Waliarwande Lema, ambaye anasikiliza kesi hiyo. Katika kesi hiyo
washtakiwa wengine ni Meneja Uendelezaji Biashara wa Kampuni ya
Mwananchi Communications Limited (MCL), Theophil Makunga na mwandishi,
Samson Mwigamba.
Makunga na wenzake Absalom Kibanda na Samson
Mwigamba wanakabiliwa na kesi ya uchochezi dhidi ya askari wa majeshi ya
ulinzi kwa kuchapisha makala kwenye Gazeti la Tanzania Daima yenye
maneno yaliyolenga kuwashawishi wasitii viongozi wao.
Makala hiyo ya
Novemba 30, 2012 ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho;"Waraka maalumu
kwa askari wote." Makala hiyo iliandika na mshtakiwa wa kwanza,
Mwigamba.
Novemba 25, mwaka jana mahakama hiyo ilifunga utetezi
katika kesi hiyo baada ya washtakiwa kupitia kwa mawakili wao
kuwasilisha kwa maandishi majumuisho ya mwisho ya kuomba mahakama iwaone
hawana hatia.
Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
itatoa uamuzi wa Pingamizi la Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) dhidi
ya maombi ya dhamana ya raia wa China wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu
uchumi kesho kutwa.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi inayowakabili
raia hao wa China, upelelezi umekamilika ambapo watasomewa maelezo ya
awali Februari 4, mwaka huu. Washtakiwa hao ni Huang Gin Xu Fujie, Chen
Jinzha na wanakabiliwa na kesi ambapo kesi hiyo ipo mbele ya Hakimu
Mfawidhi, Isaya Arufani.
Ilidaiwa na wakili wa Serikali, Tumaini
Kweka, kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kukutwa na pembe
za ndovu, shehena ya pinde 706, vyenye uzito wa kilo 1,880 zikiwa na
thamani ya sh. bilioni 5.
Kupitia kwa mawakili wao, Wachina hao
wamewasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,
wakiomba wapewe dhamana, baada ya Mahakama ya Kisutu kuwanyima dhamana
kutokana na kutokuwa na uwezo wa kisheria kusikiliza kesi hiyo.
Katika
maombi hayo ya dhamana namba 14 ya mwaka 2013, Wachina hao kupitia kwa
mawakili wao, Edward Chuwa na Richard Rweyongeza, wanadai kuwa dhamana
ni haki yao kwa mujibu wa Katiba.
Maombi hayo yalitarajiwa
kusikilizwa jana na Jaji Rose Teemba, lakini yalikwama, baada ya kila
upande katika kesi hiyo kuweka pingamizi dhidi ya upande mwingine.
Awali,
DPP aliwasilisha hati ya kupinga dhamana ya washtakiwa hao akiiomba
mahakama hiyo isiwape dhamana, akibainisha kuwa ni kwa maslahi ya Taifa.
Hata hivyo mawakili wa washtakiwa nao waliweka pingamizi dhidi ya
hati ya DPP kuiomba mahakama iitupilie mbali, wakidai kuwa
limewasilishwa mahakamani isivyo halali.
Mawakili hao, Chuwa na Rwe y
o n g e z a kwa n y a k a t i tofauti walifafanua kuwa sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai iliyotumika katika hati hiyo haitumiki
katika kesi hiyo.
Pia mawakili hao walieleza kuwa hati hiyo
imewasilishwa kabla ya wakati, huku wakibainisha kuwa ilipaswa
kuwasilishwa baada ya upelelezi kukamilika. Akijibu hoja hizo, Wakili wa
Serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi alisema kuwa Sheria iliyotumika
katika hati hiyo ni sahihi kwa kuwa sheria zote yaani CPA na Sheria ya
uhujumu uchumi zinaweza kutumika katika shauri hilo.
Pia SSA Nchimbi
alisema kuwa DPP anaweza kuwasilisha hati ya kuzuia dhamana ya
washtakiwa mahakamani wakati wowote na si lazima mpaka upelelezi uwe
umekamilika.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Teemba
aliahirisha shauri hilo hadi keshokutwa, Ijumaa kwa ajili ya uamuzi wa
uhalali wa hati ya DPP kuwepo mahakamani kuzuia dhamana ya washtakiwa
hao, kabla ya kusikiliza maombi ya msingi ya dhamana.
Wachina hao walikamatwa na nyara hizo katika nyumba walimokuwa wakiishi, mapema Novemba mwaka huu.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment