Home » » Kilo 7651 za madawa ya kulevya ya liteketezwa kuanzia 1999

Kilo 7651 za madawa ya kulevya ya liteketezwa kuanzia 1999

Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya nchini, Godfrey Nzowa amesema zaidi ya kilo 7651 za dawa za kulevya zikiwamo heroin zimeteketezwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
 
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, Kamanda Nzowa alisema hali ya dawa za kulevya kwa sasa ipo shwari kwani wamejiwekea mikakati ya kudhibiti tatizo hilo na ndio maana wamefanikiwa kuwanasa watu katika maeneo mbalimbali.
 
Nzowa alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita waliteketeza heroin kilo 1,596, cocain kilo tano, kubeli kilo 105, mbegu za bhangi kilo 3,945 na bhangi kilo 2000.
 
Alisema kuwa mtuhumiwa wa madawa ya kulevya akisha maliza kesi yake, aliyetoa hukumu kama ni jaji ama hakimu huamuru dawa hiyo kuteketezwa wakati huo huo.
 
Kamanda Nzowa alisema dawa hizo huteketezwa kwa kushirikiana na Mkemia Mkuu wa serikali, Maofisa wa mazingira, mpelelezi pamoja na watu wa mahakama kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo.
 
Alisema kinachoteketezwa pale ni dawa hizo na ndio maana wanawashirikisha wahusika hao ili kuweza kushuhudia suala hilo.
 
Pia alisema huwa hawana muda maalumu wa uteketezaji na kwamba kesi zinapomalizika mahakamani dhidi ya dawa za kulevya ndipo huenda kuziharibu kwenye viwanda vya saraji.
 
"Mwaka juzi kilo 95 za heroin, jaji aliamua zikateketezwe kwa kuwa ushahidi umemalizika na sisi tulifanya hivyo," alisema Nzowa.
 
Alisema mikakati yao kwa sasa ni kuhakikisha dawa hizo wanazikamata mapema kabla ya kuwafikia walengo ili kuondoa madhara yatokanayo na dawa za kulevya.
 
Pia alisema kwenye mipaka ya nchi ambayo hutumika kupitishia dawa hizo wamewaweka raia wema ambao hutoa taarifa na kufanikiwa kuwakamata.
 
Kamanda alisema wale wanaojihusisha na biashara hiyo ni bora wakaicha na kutafuta shughuli nyingine la sivyo watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria pale watakapokamatwa.
 
Alisema kuwa hadi sasa ni Watanzania wengi wamekamatwa nje ya nchi kwa dawa za kulevya na kwamba wataendelea kupambana na suala hilo.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa