Home » » Kampuni Dar zakwepa kodi bilioni 50/- kila mwakaKampuni Dar zakwepa kodi bilioni 50/- kila mwaka

Kampuni Dar zakwepa kodi bilioni 50/- kila mwakaKampuni Dar zakwepa kodi bilioni 50/- kila mwaka

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imesema Manispaa za Temeke na Kinondoni zinapoteza jumla ya Sh. bilioni 50 kila mwaka kutokana na kampuni nyingi kukwepa kulipa kodi ya huduma.
 
Wakizungumza katika kikao cha pamoja kati ya wabunge wanaounda kamati hiyo, ikiongozwa na Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed, na viongozi wa Manispaa hizo, walitaja baadhi ya kampuni zinazoongoza kwa vitendo hivyo kuwa ni zile za mitandao ya simu na vituo vya mafuta.
 
Wakionekana kusikitishwa na jambo hilo, Mbunge wa Msalala, Ezekiel Mahige (CCM), alisema kampuni hizo zinasaidiwa na baadhi ya watendaji kutoka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutekeleza mpango huo.
 
'DILI' LINAVYOFANYIKA
Akizungumza kwenye kikao hicho, Maige, alisema kampuni hizo zinatakiwa kulipa kodi ya huduma (Service Levy)  ya asilimia 0.3 ya mapato yote, lakini hazifanyi hivyo na badala yake inalipa pale zinapotaka.
 
Alisema, halmashauri za Temeke na Kinondoni, zingekuwa na uwezo wa kutekeleza miradi yake bila kusaidiwa na serikali kutokana na kuwa na kampuni nyingi.
 
"Kinyume chake kampuni hizo zinalipa kodi tofauti na gharama halisi inayotakiwa, hili jambo lazima liangaliwe na kusiwepo na kigugumizi," alisema Maige.
 
Aliongeza kwamba jambo la kusikitisha, mtendaji mmoja kutoka Tamisemi amegeuka kuwa kizuizi cha Halmashauri nchini kuchukua kodi hiyo kutoka kampuni za mafuta baada ya kueleza malipo hayo yanayofanyika kwenye makao makuu zao zilizopo jijini Dar es Salaam.
 
"Kuna siku nitamtaja huyu mtu, nakumbuka hata Halmashauri ya Nzega imeshindwa kutoza kodi ya huduma katika vituo vya mafuta, akisema tusichukue kwani wanalipa huku Dar es Salaam, lakini ukiangalia katika mtiririko wa vyanzo vya mapato kampuni hizi hazionekani kulipa," alisema.
 
Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Suleiman Zed, Mbunge wa Bukene (CCM), alisema anashangaa kuona kampuni za simu zinalipa Sh. milioni 700 kwa mwaka, kiwango ambacho ni kidogo sana ukilinganisha na mapato yao halisi.
 
Alisema kampuni moja pekee inaingiza zaidi ya Sh. bilioni 30 kwa mwezi kutokana na kadi za muda wa maongezi, hivyo Manispaa husika inapaswa kulipwa Sh. milioni 900 kwa mwezi.
 
Alifafanua kwamba kinachofanyika kampuni hizo hazionyeshi vielelezo vya mapato yao wakati zinapokokotoa, badala yake zinalipa kiholela kama msaada.
 
"Huu ni wizi wa mchana, lazima viongozi wa halmashauri watafute takwimu sahihi ili walipwe pesa zao, naamini wakifanikiwa hili wataweza kujitegemea," alisema Zed.
 
Alisema kwa kodi hiyo pekee kila manispaa inaweza kukusanya Sh. bilioni 50 kwa mwaka, pesa ambazo zinapotea kutokana na ukwepaji huo.
 
Naibu Waziri wa Tamisemi, Kassim Majaliwa, alisema serikali imepokea kauli hizo za wabunge na itazifanyia kazi haraka.
 
Alisema kwa kusikia kilio cha halmashauri kukosa vyanzo vya mapato, serikali imerudisha jukumu la kutoza kodi za majengo kufanywa na mamlaka hizo.
 
TEMEKE YAFAGILIWA
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Rajab Mbarouk Mohamed, aliipongeza Manispaa ya Temeke, kwa kufanikiwa kudhibiti upotevu wa pesa za umma baada ya kuanzisha mfumo maalum wa ulipaji wa kodi mbalimbali.
 
Alisema mfumo huo wa kieletroniki umesaidia kukua kwa mapato kutoka Sh. bilioni 18.3 mwaka 2012 hadi Sh. bilioni 28.1 mwaka 2013.
 
"Jambo hili tunawapongeza kwani imesaidia wengine kujifunza kwamba ukiwa na jitihada na kujitoa lazima utapata mafanikio ya kushangaza," alisema Mbarouk. 
CHANZO: NIPASHE 

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa